Home
Kitaifa
Serikali yatenga Bil 100 ukarabati viwanja vya ndege
SERIKALI
ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk John Magufuli imetenga kiasi
cha sh. Bil. 100 katika bajeti ya mwaka 2016/17 kwa ajili ya ukarabati
na upanuzi wa viwanja mbalimbali vya ndege nchini.
Rais Dk.
Magufuli alisema hayo juzi katika sherehe za uzinduzi wa ndege mbili za
Shirika la ndege la Tanzania (ATCL) aina ya Bombardier Dash 8 Q400
zilizonunuliwa na serikali, kwenye Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha
Julius Nyerere (JNIA), ambapo viwanja hivyo vitaboreshwa ili kuwezesha
ndege hizo kutua bila wasiwasi.
Mhe. Rais
akifafanua zaidi, alisema , kiwanja cha ndege cha Nduli kilichopo
umbali wa kilometa 13 Kaskazini Mashariki mwa Manispaa ya Iringa,
ambacho kipo kwenye kiwango cha lami kitakarabatiwa, ili ndege hizo
zitue na kupaa bila tatizo.
Dk.
Magufuli alisema, kiwanja cha Nduli Iringa ni kiunganishi kikubwa na
JNIA na kitatumika kupeleka watalii wanaokwenda kutembelea mbuga ya
wanyama ya Ruaha, wakitokea Mataifa mbalimbali duniani.
Alisema
mbali na kiwanja hicho cha Nduli, pia kiwanja cha Musoma kitawekwa lami,
ili nacho kiwe moja ya maeneo ndege hiyo itakwenda, na kurahisisha
usafiri wa watalii watakaokwenda kwenye mbuga ya wanyama ya Serengeti.
Kwa sasa kiwanja cha Musoma kipo katika kiwango cha changarawe na
kinatumika kwa ndege mbalimbali kutua na kupaa.
Kwa
mujibu wa Meneja wa Kiwanja cha ndege cha Nduli, Bi. Hannah Kibopile,
kiwanja hicho kinapokea ndege ndogo zaidi ya saba zenye uwezo wa kubeba
abiria 13, na kati ya hizo tatu zipo kwenye ratiba maalum ya kila siku
na zilizosalia ni za kukodishwa na nyingine zinakwenda mbuga ya wanyama
ya Ruaha.
Bi. Kibopile alisema ndege zinazotua kwenye kiwanja hicho zinatoka Jijini Dar es Salaam, Sumbawanga, Songea na Mbuga ya Ruaha.
Naye
Kaimu Meneja wa Musoma, Bi. Faraja Mayugwa amesema kiwanja hicho
kinapokea ndege zaidi ya nne kwa siku na nyingi zinakuwa za kukodi
zinazopeleka watalii mbugani.
Katika
hotuba yake, Rais Magufuli alisema “Hii ndege inaweza kutua katika
kiwanja cha aina yeyote; na serikali itaendelea na ukarabati wa viwanja
vya ndege vya pembezoni, ili viwe katika kiwango, ambacho ndege hizi
zitatua na kuruka bila wasiwasi,”.
Akifafanua
zaidi Dk. Magufuli alisema serikali inatarajia kununua ndege nyingine
kubwa mbili zenye uwezo wa kubeba abiria 160 na 242, ambazo zitaanzia
safari zake kwenye JNIA kwenda sehemu mbalimbali duniani kama China au
Marekani moja kwa moja, ikiwa ni lengo la kupata abiria hao, ambao wengi
wao watakuwa watalii wanaokuja nchini kutembelea vivutio mbalimbali.
Bombardier inauwezo wa kubeba abiria 76.
Naye
Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Prof Makame
Mbarawa awali wakati akimkaribisha Mhe. Rais kuzungumza na wananchi
katika ghafla hiyo ya uzinduzi wa ndege, alisema kwa kuanzia ndege hizo
zitatua kwenye viwanja 11 vya ndege, ambavyo ni Kiwanja cha Kimataifa
cha Julius Nyerere (JNIA), Kilimanjaro (KIA), Zanzibar (AAKIA), Mwanza,
Dodoma, Arusha, Bukoba, Kigoma, Tabora, Mbeya na Mtwara. Pia ndege
hiyo itakwenda Comoro.
Mhe.
Prof. Mbarawa ameiagiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA),
kuendelea kufanya upembuzi yakinifu kwa kuangalia viwanja vingine vya
ndege, ambavyo ndege hizi zitakwenda.
Back To Top
Post A Comment: