Rais Magufuli Ashiriki Ibada Ya Jumapili Kuadhimisha Siku Ya Bwana Ya 19 Baada Ya Pentekoste Kanisa La Mtakatifu Albano Jijini Dar Es Salaam Sept 25,2016
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo
asubuhi tarehe 25 Septemba, 2016 ameungana na Waumini wa Kanisa la
Anglikana la Mtakatifu Albano lililopo Posta Jijini Dar es Salaam kusali
ibada ya Jumapili ya kuadhimisha Siku ya Bwana ya 19 baada ya
Pentekoste.
Akizungumza
na Waumini wa Kanisa hilo baada ya kumalizika kwa Ibada, Rais Magufuli
aliyeongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amewashukuru Viongozi na
Waumini wa Kanisa la Anglikana na Madhehebu mengine ya Dini hapa nchini
kwa kuendelea kuliombea Taifa na kudumisha amani na utulivu.
Dkt.
Magufuli amesisitiza kuwa Viongozi wa Dini wanafanya kazi kubwa na
muhimu katika Taifa na kwamba Watanzania wote bila kujali dini zao,
itikadi za kisiasa, makundi na kanda zao wana wajibu wa kuungana na
Viongozi hao ili nia hiyo njema iendelee kufanikiwa.
“Ninawashukuru
kwa sababu mnaendelea kuliombea Taifa hili, ninawashukuru kwa sababu
siku zote mmekuwa mkipiga magoti na kumtanguliza Mungu mbele,
ninawashukuru kwa sababu mnaendelea kuombea amani ya nchi yetu na upendo
udumu ndani yetu sisi sote.
“Makanisa yote, Madhehebu yote, Dini zote, Vyama vyote, upendo tukiujenga ndio tutaiendeleza vizuri Tanzania yetu” Amesema Rais Magufuli.
Kwa
upande wake Padre Jackson Sostenes aliyeongoza Ibada hiyo amemshukuru
Rais Magufuli kwa kuungana na waumini wa Kanisa hilo katika Ibada ya
Jumapili na ameahidi kuwa Viongozi na Waumini wa Kanisa hilo wataendelea
kumuombea na kuliombea Taifa.
Katika Ibada hiyo Rais Magufuli ametoa Shilingi Milioni 1 kuchangia vikundi vya kwaya vya kanisa hilo.
Post A Comment: