Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania TCRA imetangaza hukumu dhidi ya vituo viwili vya Redio
vilivyofungiwa kutokana na kile serikali ilichosema kuwa ni
kuchochea ghasia na kumkashifu Rais John Magufuli.
Vituo
vilivyokuwa vimefungiwa kwa muda usiojulikana kwa tuhuma za kukiuka
Sheria za Utangazaji ni Magic FM cha jijini Dar es Salaam na Redio 5 cha
jijini Arusha .
Kupitia maamuzi yaliyosomwa
na Makamu mwenyekiti wa kamati ya maudhui Joseph Mapunda Kamati
imeikuta Redio 5 na hatia ya kumkashifu rais na kuchochea uvunjifu wa
amani na hivyo imehukumiwa kulipa shilingi milioni 5 za Tanzania.
Aidha, kituo hicho cha redio kimefungiwa kutorusha matangazo kwa miezi mitatu na kuwekwa chini ya uangalizi wa mwaka mmoja.
Wakati
huo huo Radio Magic FM imepewa onyo na kutakiwa kumwomba radhi rais wa
Tanzania pamoja na wasikilizaji wa redio hiyo kwa siku tatu mfululizo.
Tangu
tarehe 29 mwezi Agosti 2016 Waziri wa Habari nchini humo Nape Nnauye
alitangaza kuvifungia vituo hivyo viwili vya redio kwa muda
usiojulikana kwa madai kuwa vilikiuka sheria za utangazaji.
Hukumu
hiyo iliiibua minong'ono miongoni mwa wananchi wa Tanzania wakidai kuwa
huo ni uminyaji wa uhuru wa habari hasa katika kipindi ambacho Tanzania
iko katika vuguvugu kali la mvutano kati ya Serikali na vyama vya
upinzani.
Back To Top
Post A Comment: