RAIS John Magufuli amepokea taarifa ya maafa yaliyosababishwa na
tetemoko la ardhi lililotokea katika mkoa wa Kagera na mikoa jirani ya
Mwanza, Geita na Kigoma kutoka kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo ya maafa na michango kwa
ajili ya waathirika wa maafa hayo, Rais Magufuli aliwashukuru wote
waliojitoa kusaidia waathirika akiwataja marais wa nchi za Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC), Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais wa Kenya,
Uhuru Kenyatta na Rais wa Rwanda, Paul Kagame, kuwa wamempigia simu za
kumpa pole na tayari wametoa misaada yao.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa Dar es Salaam jana ilisema pamoja na
kupokea taarifa hiyo, Rais Magufuli alipokea mchango wa fedha taslimu
Dola za Kimarekani 200,000 sawa na takribani Sh milioni 437 kutoka kwa
Rais Museveni.
Pia Rais Magufuli alipokea taarifa ya mchango wa mabati,
blangeti na magodoro vyenye thamani ya Sh milioni 115 kutoka kwa Rais
Kenyatta kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani
Kagera.
Pia alizishukuru nchi mbalimbali, mashirika, wafanyabiashara,
watumishi wa umma na watu binafsi waliochangia na kusema michango hiyo
ina umuhimu mkubwa katika kukabiliana na athari za maafa haya.
Post A Comment: