WAKAZI wa mji wa Mpemba Wilaya ya Momba mkoani Songwe wamejikuta katika wakati mgumu baada ya Jeneza la mtoto mdogo kutelekezwa na watu wasiojulikana likiwa na vitu vinavyodhaniwa kuwa ni hirizi.

Jeneza hilo lilikutwa nyumbani kwa Mchungaji wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi, Jamson Mwiligumo juzi majira ya asubuhi wakati watoto wakienda shule.

Wakizungumzia tukio hilo baadhi ya majirani walisema Jeneza hilo lilitelekezwa usiku na kukutwa na watoto waliokuwa wakienda shule asubuhi ambapo baada ya kufunua lilikutwa linavitu vinavyohusishwa na ushirikina.

Walisema kutokana na hali hiyo kila mtu alishikwa na butwaa ambapo walitoa taarifa kwa mwenye nyumba ambaye ni mchungaji anayeishi jijini Mbeya hivyo wakati wa tukio hakuwepo.

Kwa upande wake Mchungaji Mwiligumo alipoulizwa na sakata hi;lo alikiri kuwa ni kweli na kwamba alipata taairfa za uwepo wa jeneza hilo ambali lilikutwa nyumbani kwake asubuhi na watoto wanaoishi pale.

“Ni kweli kuna jeneza lilikutwa nyumbani kwangu na watoto waliokuwa wakienda shule na wamesema lilikuwa na hirizi ndani sasa sijui malengo yao ni yapi kwani mimi naishi Mbeya sio Mpemba walikopeleka”alisema Mchungaji.

Alisema walitoa taarifa Polisi ambao walifika na kulichukua Jeneza hilo kisha nae akaitwa kutoa maelezo ambapo alisema aliulizwa na jeshi la Polisi kama kuna ugomvi alionao na baadhi ya watu lakini aligoma kuwa tangu ajenge nyumba hiyo hajawahi kugombana na mtu.

Mchungaji huyo alienda mbali zaidi na kusema kama kuna vita inaanzishwa dhidi yake hawataweza kwani yeye anapigana vita za kiroho ambayo ili mtu ashinde inahitaji maombi zaidi.

Nao baadhi ya majirani na Mchungaji huyo walisema inawezekana ni vitisho kuelekea mkutano mkuu wa Sinodi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 16 mwaka huu wa Kanisa la Moravian Jimbo la Kusini Magharibi ambapo kupitia mkutano huo pia hufanyika uchaguzi.

Wakizungumza na Mbeya yetu kwa sharti la kuficha majina, walisema Kanisa la Moravian limeingiliwa na mgogoro wa muda mrefu hivyo kupitia mkutano waSinodi ujao vitu vingi vinaweza kuibuka hivyo njama zinatumika kuwatisha baadhi ya wajumbe.

Walisema Mchungaji huyo ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Mafunzo ya Jimbo na kusimamishwa kutokana na mgogoro wa kanisa hivyo kuna njama za kumtisha ili akate tama ya kupigania haki yake na wachungaji wengine kupitia kumwekea majeneza.

Kwa muda mrefu kumekuwa na mgogoro wa Kanisa la Moraviani Jimbo la Kusini Magharibi kati ya Askofu wa Jimbo Alinikisa Cheyo na Mwenyekiti aliyesimamishwa kazi Mchungaji Nosigwe Buya.
Share To:

msumbanews

Post A Comment: