📍 Seoul, Korea Kusini
Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amesema kuwa kutokana na kuongezeka kwa mahitaji na matumizi ya Madini Muhimu duniani, Tanzania ina dhamira ya dhati ya kuendeleza Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na Madini Mkakati hapa nchini kwa kuimarisha ushirikiano na Nchi ya Korea ya Kusini kwa lengo la kuleta mageuzi yenye kuleta tija zaidi kupitia sekta hiyo.
Ameyasema hayo leo Machi 25, 2025 jijini Seoul, Korea Kusini wakati akizungumza katika Mkutano wa Madini Muhimu kati ya Tanzania na Korea yaliyoandaliwa jijini humo.
Dkt. Kiruswa amesema kuwa, kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA) ya mwaka 2023, matumizi ya lithiamu yameongezeka kwa asilimia 30, huku mahitaji ya nikeli, kobalti, kinyewe (graphite), na madini adimu yakiongezeka kati ya asilimia 8 hadi 15 na kwamba hali hiyo inatoa fursa kubwa kwa Tanzania kushirikiana na mataifa yenye teknolojia za kisasa kama Korea katika uchimbaji, uongezaji thamani, na biashara ya madini haya.
Aidha, Dkt. Kiruswa amesisitiza kuwa, Tanzania ni nchi yenye utajiri mkubwa wa madini yanayohitajika kwa teknolojia za kisasa, hususan nishati mbadala.
“Tanzania ina hifadhi kubwa ya madini kama vile grafiti, nikeli, kobolti, lithiamu, madini adimu (REE), shaba, manganese, zinc, dhahabu, na vito vya thamani, ambavyo vinahitajika kwa maendeleo ya viwanda vya teknolojia na nishati safi,” amesema Dkt. Kiruswa.
Sambamba na hilo , Dkt. Kiruswa amebainisha kuwa, katika jitihada za kuhakikisha sekta ya madini inawanufaisha Watanzania, Tanzania inalenga kuongeza thamani ya madini yake ndani ya nchi kabla ya kuuza nje. “Tunatambua uwezo mkubwa wa Korea katika teknolojia za uchimbaji, utafiti, na uchenjuaji wa madini. Ushirikiano wetu utaleta manufaa kwa pande zote mbili,” ameongeza Naibu Waziri.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa amepongeza Kampuni za Kikorea kama POSCO International, inayoshiriki katika mradi wa Mahenge Graphite, na Yulho, ambayo imewekeza katika uchimbaji wa nikeli kusini mwa Tanzania na kwamba uwepo wa Kampuni hizo hapa nchini ni ushahidi kwamba Tanzania ni mahali salama na sahihi kwa uwekezaji wa madini.
Katika mkutano huo, Ujumbe wa Tanzania umesheheni wadau muhimu wa Sekta ya Madini, ikiwa ni pamoja na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Tume ya Madini, Kampuni za uchimbaji na usafirishaji wa madini, mabenki, na wataalam wa sheria ili kutoa taarifa na kujibu maswali ya wawekezaji wa Kikorea.
“Tupo hapa kuhakikisha kuwa kila mwekezaji anapata majibu sahihi na kuelewa fursa zilizopo Tanzania. Tuko tayari kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi ya Korea ili kufanikisha uwekezaji wa muda mrefu wenye tija kwa nchi zetu zote mbili,” amesisitiza Dkt. Kiruswa.
Naibu Waziri Dkt. Kiruswa amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa katika Mkutano wa Korea-Afrika, akisema kuwa Tanzania iko tayari kuchukua hatua madhubuti ili kuhakikisha kuwa sekta ya madini inachangia kikamilifu maendeleo ya kiuchumi.