Na.Jusline Marco:Arusha
Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji, halmashauri ya Arusha wametakiwa kuzingatia mkakati wa Serikali juu ya masuala ya lishe bora ya wananchi katika maeneo yao kupitia mkataba wa lishe waliosaini lengo likiwa kuondoa hali ya udumavu katika jamii na kuwa na jamii yenye afya bora.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru,Mhandisi Richard Ruyango wakati akifungua kikao kazi cha mkatati wa lishe kilichojumuisha Maafisa Watendaji wa Kata na Vijiji, halmashauri ya Arusha,kilicholenga kufanya tathmini ya hali ya lishe kwa miaka mitano iliyopita na kusaini mkataba wa mkakati wa lishe kwa miaka mitano ijayo.
Mhandisi Ruyango amewaagiza watendaji hao kuwa na mkakati shirikishi utakaowashirikisha wananchi, Wahudumu wa Afya, wahudumu wa Afya ngazi ya jamii pamoja na wadau wa maendeleo kutoa elimu ya lishe kwa jamii ili kuhakikisha wananchi wote wanapata ufahamu juu ya lishe bora hususani kwa wajawazito na watoto.
Aidha Mhandisi Ruyango amewasisitiza Watendaji hao kuhakikisha kina mama Wajawazito katika maeneo yao wanapata lishe bora katika siku 1000 za ujauzito, lishe ambayo inawezesha mtoto aliye tumboni kujenga afya bora ya ubongo na mwili.
Naye Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi amewataka Maafisa watendaji hao, kuhakikisha wajawazito wote katika maeneo yao wanahudhuria kliniki pindi wanapopata ujauzito na wazazi wenye watoto wa umri chini ya miaka mitano kuwapeleka watoto hao kliniki.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Kata ya Ilboru, Wema Sikoi amekiri kupata uelewa mkubwa juu ya masuala ya lishe na kuahidi kufanyia kazi maelekezo yaliyotolewa na serikali kulingana na mkataba waliousani na kuongeza kuwa wataongeza kasi ya kuhakikisha wajawazito wanahudhuria kliniki na wenza wao pamoja na kuwapatia lishe bora katika siku 1000 za ujauzito.
Hata hivyo Afisa Lishe Halmasahuri ya Arusha Doto Milembe, ameyataja makundi ya vyakula yanayopaswa kuliwa ili mtu kuwa na lishe bora kuwa ni vyakula vya nafaka na mizizi, vyakula vya nyama na mikunde, mbogamboga na matunda pamoja na sukari na asali ambapo amebainisha kuwa vyakula vyote hivyo vinapatika katika maeneo mengi ya halmashauri ya Arusha.
Serikali imeandaa mpango wa lishe wa miaka mitano 2022 hadi 2027 unaotaka kila mwananchi kupata lishe bora kwa kula mlo wenye makundi matano ya vyakula kuanzia siku 1000 za mama mjazito, mtoto anapozaliwa mpaka miaka mitano na jamii nzima, mkakati unaoelekeza kuwasainisha mikataba Maafisa Watendaji wa Kata ili kusimamia mkakati huo wa lishe.
Post A Comment: