Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama mkoani Arusha limejidhatiti kuimarisha usalama zaidi hususani wakati huu ambao mkoa huo uko kwenye maandalizi kabambe ya kilele cha siku ya wafanyakazi Duniani (Mei mosi) inayofanyika kitaifa mkoani humo Mei 01.2024 kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha

Akizungumza na wanahabari muda mfupi baada ya kukamilika kwa kikao kazi cha maandalizi ya sherehe hizo kilichofanyika leo, Jumamosi Aprili 27.2024 kikiongozwa na Mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Makonda, Kamanda wa Polisi mkoani humo ACP Justine Masejo amesema katika kuhakikisha usalama unaimarika kabla, wakati na hata baada ya sherehe hizo pamoja na mambo mengine Jeshi hilo limekuwa likifanya doria za miguu na magari kwenye kila kona ya mkoa huo hivyo kutoa wito kwa wakazi na wageni wanaoingia mkoani humo kufanya shughuli zao kwa uhuru, amani na utulivu 

Amesema suala la ulinzi linaanza na mtu mmoja mmoja kisha jamii kwa ujumla hivyo kutoa wito kwa wananchi pale wanapoona viashiria vya uvunjifu wa amani kwa namna yoyote ile kutoa taarifa haraka kwenye maeneo husika ili hatua stahiki zichukuliwe 

Katika hatua nyingine ACP Masejo ametoa wito kwa wakazi wa mkoa wa Arusha na viunga vyake kuchangamkia fursa zitokanazo na uwepo wa sherehe hizo kwenye mkoa huo kwa kuwa nafasi kama hizo hutazamwa kwa mrengo chanya kwenye jicho la kiuchumi.

 


Upo umuhimu mkubwa kwa wananchi kuzitunza barabara pamoja na alama za barabarani ili kuzifanya barabara kuwa salama kwa watumiaji wakati wote, imeelezwa.

Hayo yamebainishwa na Meneja wa  Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilayani Ngara Mkoani Kagera Mhandisi Makoro Magori wakati akielezea mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhandisi Magori alisema ili barabara ziweze kuishi muda mrefu wananchi wanao wajibu wa kuzitunza na kuzilinda, hivyo kusaidia Serikali kuokoa gharama za matengenezo ya mara kwa mara.

“Kuepuka ajali za barabarani kila mwananchi anapaswa kulinda miundombinu ya barabara pamoja na alama zake ili watumiaji wa vyombo vya moto kuwa salama,” alisisitiza.

Kwa upande wa bajeti Mhandisi Magori alisema kwamba katika kipindi cha miaka mitatu chini ya uongozi wa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Wilaya ya Ngara kwa mwaka 2023/2024 ilipata Shilingi bilioni 2.5 ukilinganisha na Shilingi bilioni 1.2 miaka ya nyuma.

Alisema fedha hizo zimeweza kuboresha barabara za vijijini na mijini ambazo zimeweza kupitika wakati wote na kufungua uchumi wa wananchi na wilaya kwa ujumla.

 


Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mh. Paul Christian Makonda amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Arusha kutenga barabara maalumu katikati ya jiji, itumike kwaajili ya Maonesho ya kibiashara kwa wajasiriamali wa mavazi ya asili, Picha, Vinyago na bidhaa nyingine za Urembo kuelekea kwenye kilele cha siku ya wafanyakazi duniani.

Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa amemuagiza Mkuu wa Wilaya Mh. Felician Gasper Mtahengerwa kuwa barabara hiyo iwe pembezoni mwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, uwanja uliotengwa kwaajili ya kutumika kwenye sherehe za Mei Mosi, akitaka ianze kutumika Jumatatu ya wiki ijayo.

Mkuu wa Mkoa Ametoa kauli hiyo leo Aprili 27,2024 wakati kikao kazi na viongozi wa Chama cha Wafanyakazi na kamati mbalimbali za maandalizi ya sherehe za wafanyakazi ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mh. Makonda amesema wananchi wa Mkoa wa Arusha wanapaswa kunufaika na shughuli mbalimbali za kitaifa zinazofanyika Mkoani hapa na hivyo kuwataka wananchi kujiandaa kutumia fursa zinazotokana na ugeni ambao tayari umeshaanza kuwasili Jijini Arusha kujiandaa na sherehe hizo.

Katika hatua nyingine Mh. Mkuu wa mkoa amewahakikishia usalama wa kutosha wakazi wa Arusha na wageni wote wanaofika mkoani Arusha kwenye shamra shamra za kuelekea kwenye Kilele cha siku ya wafanyakazi duniani.

Mheshimiwa Mkuu wa mkoa ametumia fursa hiyo pia kuwaomba wananchi wa Arusha na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi katika sherehe hizo za Mei Mosi kama sehemu ya kuwaenzi na kuenzi kazi nzuri zinazofanywa na watumishi na wafanyakazi mbalimbali.

Katika Kikao hicho Mkuu wa mkoa pia ametangaza kuanza kwa shamra shamra za kuelekea siku ya wafanyakazi ikiwemo michezo ya sarakasi na vikundi mbalimbali vya sanaa ambavyo vitakuwa vikizunguka maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha.

Kwa Upande wake Rais wa Vyama vya wafanyakazi TUCTA Bw.Tumaini Nyamhokya amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ubunifu wake kwenye kukoleza shamra shamra za Mei Mosi mwaka huu akiutaja ujana wake kama silaha muhimu iliyoongeza mambo mengi mapya kwenye sherehe za mwaka huu jijini Arusha.

Nyamhokya ametumia fursa hiyo pia kutangaza kuhusu mbio za marathoni zitakazozinduliwa kesho jumapili Aprili 28, 2024 na kuwaalika wananchi kushiriki kama sehemu ya shamrashamra za kuelekea kilele cha Mei Mosi.

  


Mkuu wa mkoa wa Arusha Paul Makonda ametoa wito kwa wakazi wa mkoa huo na viunga vyake kujitokeza kwa wingi kushiriki kwenye kilele cha siku ya wafanyakazi Duniani (Mei mosi) inayotarajiwa kufanyika kitaifa Mei 01.2024 kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha

Makonda ametoa wito huo leo, Jumamosi Aprili 27.2024 alipokuwa kwenye kikao kazi cha maandalizi kuelekea siku ya wafanyakazi Duniani kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Arusha ambapo amesema uwepo wa shughuli hiyo ya kitaifa mkoani humo ni fursa kubwa kwa wakazi wake, na kwamba  katika kuchangamkia fursa hiyo uongozi wa mkoa huo umeandaa eneo maalumu (Barabara) kando ya uwanja wa Sheikh Amri Abeid kwa ajili ya kutumiwa na wajasiriamali mbalimbali kufanya biashara zao

Amesema uwepo wa siku hiyo (Mei mosi) unaashiria uhuru na haki za wafanyakazi mahala pa kazi hivyo ni vyema wananchi wakatambua kuwa ushiriki wao utawaongezea morali watumishi katika kuihudumia jamii, ambapo katika hilo amewapongeza viongozi wa shirikisho la wafanyakazi nchini (TUCTA) kwa kazi kubwa wanayoifanya kuhakikisha siku hiyo inafana

Kwa upande wake Rais wa shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania (TUCTA) Tumaini Nyamhokya amemshukuru Mkuu wa mkoa huyo kwa kuitisha kikao kazi hicho ambacho amedai kuwa kimeongeza msukumo na kasi kwa watumishi na wananchi kushiriki kikamilifu kwenye shughuli mbalimbali zinazofanyika mkoani humo kama sehemu ya shamrashamra za kuelekea siku ya wafanyakazi Duniani 

Ametaja baadhi ya shughuli zinazofanyika kuwa ni pamoja na mashindano ya michezo ya aina mbalimbali yanayoendelea kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, maandalizi ya riadha maalumu ya Mei mosi, pamoja na maonesho yanayoendelea kwenye viwanja vya General Tyre yaliyoandaliwa na Wakala wa usalama na afya mahala pa kazi (OSHA - Occupational Safety and Healthy Authority) ambayo yanatarajiwa kufungwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko Aprili 28.2024

Naye, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha ACP Justine Masejo amewaeleza wanahabari kuwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama mkoani humo linaendelea kuimarisha usalama kwenye kila kona ya mkoa huo hivyo wananchi hawapaswi kuwa na mashaka yoyote ya kiusalama wakati huu ambao idadi ya watu imeongezeka maradufu kwenye jiji la Arusha na mkoa wote kwa ujumla wake.



Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi hususan shule binafsi ili kuboresha sekta ya elimu nchini.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi Nchini (TAPIE), leo Aprili 27, 2024 jijini Dar es salaam Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan haiwezi kuacha Wadau wa Elimu wakilalamika, kwa kuwa uwepo wao unaisaidia Serikali.

“Nataka niwahakikishie kuwa Serikali imeendelea kukutana na TAPIE mara kwa mara, na hapa namuelekeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. Jenista Mhagama kuratibu mkutano wa pamoja kati ya TAPIE na Wizara za Ardhi, Fedha, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kujadiliana kwa pamoja na kupata suhulu ya changamoto zinazowakabili”, amesema Dkt. Biteko.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewaasa TAPIE kuzingatia masharti yaliyoainishwa katika barua na vyeti vya usajili wa asasi zao, kwa kuwa kuna baadhi hukiuka masharti hivyo kusababisha migongano isiyo ya lazima na mamlaka zilizokasimiwa kusimamia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya uendeshaji wa asasi za elimu nchini.

Vilevile, amewataka kufuata sheria na kanuni za utoaji elimu, kuhimiza na kuimarisha maadili, nidhamu na malezi bora kwa watumishi na wanafunzi walio chini ya asasi zao. Pia, amesema kuwa suala la uadilifu katika shughuli za uendeshaji na usimamizi wa mitihani ya Kitaifa lisisitizwe na kutiliwa mkazo ili kupata wataalam wenye sifa stahiki.

Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda amezipongeza shule binafsi kwa kufanya uwekezaji mkubwa ambao sasa unavutia baadhi wanafunzi kutoka nchi zingine kuja kusoma hapa nchini

“Tunapozungumza kuwa tunaenda na elimu ya miaka 10 tunaamini sekta binafsi ina msaada mkubwa katika hili kwa sasa tutanza na ujenzi wa shule 100 za sekondari za ufundi na ni imani yangu kuwa tutashirikiana vizuri na sekta binafsi”, amesisitiza Prof. Mkenda.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mhe. Husna Sekiboko amesema kuwa Serikali imeweka mazingira wezeshi katika sekta binafsi na sasa kuna zaidi ya shule 500. Pia, amempongeza Rais Mhe. Dkt.  Samia kwa kutoa maelekezo ya kuboresha sekta ya elimu nchini.

“Tunaipongeza sekta binafsi kwa kutoa ajira na Bunge tunatambua mchango wa TAPIE, tutawaunga mkono katika kuboresha sekta hii ya elimu. Kuhusu leseni ya kuanzisha shule, Kamati yangu inaungana na TAPIE tunaoomba Serikali izungumze na wadau ili kusaidia kupiga hatua ya utekelezaji wa mitaala iliyowekwa”, ameeleza Mhe. Sekiboko.

Sambamba na hayo, ameitaka TAPIE kulinda mikataba ya watumishi walio chini ya Taasisi zao ikiwa ni pamoja na kuwasilisha michango yao katika Mifuko ya Hifadhi za Jamii.

 


MICHUANO ya Michezo ya Mei Mosi 2024 imefikia hatua ya nusu fainali katika michezo ya mpira wa miguu na netiboli ambapo kwa mwaka huu taasisi 54 zinashiriki mashindano hayo.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ya Mei Mosi Taifa Bi. Roselyne Massam wakati akiongea na waandishi wa Habari kuhusu michuano hiyo inayoendelea jijini Arusha ikiwa ni shamrashara za kuelekea maadhimisho ya sikukuu  ya Wafanyakazi Duniani

 “Tunategemea kilele cha michezo hii kufanyika Aprili 29, 2024 ambapo tutapata washindi wetu watakaopewa zawadi na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi)" amesema Bi Massam.

Kwa upande wa mpira wa miguu, timu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeichapa Wizara ya Maliasili na Utalii magoli 2-0, huku timu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wamewafunga Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa magoli 4 -1, nayo Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wamewaliza timu ya Wizara ya Maji kw bao 1 – 0 na timu ya  Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi imesonga mbele kwa kuwashinda Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa penalti 4–2. Timu hizo zilitoka suluhu katika dakika za kawaida.

Katika mchezo wa netiboli, timu ya Ofisi ya Rais Ikulu wameifunga  Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa jumla ya magoli 64 – 20, nayo Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi imewashinda TAMISEMI kwa magoli 46–22; huku  Wizara ya Ulizi na Jeshi la Kujenga Taifa wameichezesha kwata Wizara ya Uchukuzi kwa kuwafunga  magoli 63–18 na Wizara ya Afya wameifunga timu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa magoli 76 – 21.

Katika kuimarisha undugu na ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao ya kila sekta binafsi, Bi Massam amewahimiza waajiri kuwaruhusu watumishi wao kufanya mazoezi wakati wote wanapokuwa kwenye vituo vyao vya kazi hatua itakayowafanya kuleta ushindani wakati wa mashindano ya Mei Mosi na mashindano ya mashirikisho ya SHIMIWI, BAMATA, SHIMISEMITA na SHIMMUTA.








 


Na Eleuteri Mangi, Arusha

Timu ya Viongozi wa vilabu vinavyoshiriki michuano ya Mei Mosi Taifa 2024 ambao ni mashabiki wa vilabu vya Simba na Yanga wametoa burudani kwa wakazi wa jiji la arusha katika mchezo wa mpira wa miguu na netiboli kuthibitisha umwamba wa vilabu vyao wanavyoshabikia hapa nchini.

Akizungumzia michezo hiyo iliyofanyika Aprili 26, 2024 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha, Katibu wa Kamati ya Michezo ya Mei Mosi Taifa Bw. Alex Temba amesema kuwa wanamichezo hao ambao ni viongozi mashabiki wa timu ya Simba katika mpira wa miguu wameibuka kidedea kwa kuwafunga viongozi mashabiki wa Yanga kwa magoli 2 - 0 wakati kwa upande wa netibili viongozi wa timu ya Yanga wameibuka kidedea.

“Kwa kweli mechi ilikuwa nzuri imefurahisha, unaona mashabiki na wananchi wa jiji la Arusha walivyojitokeza kwa wingi, hizi timu zetu mbili zina mkusanyiko mkubwa sana wa watu. Tunawakaribisha wananchi wa Arusha waje kupata burudani ya michezo mbalimbali na kuwaona wanamichezo wa Rais Mama Samia wanavyojikinga na magonjwa na maradi yasiyoambukizwa kwa njia ya michezo” Bw. Temba. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mashabiki wa Simba na Katibu wa Mawasiliano Sports Klab Bw. Aliko Mwaiteleke amesema wanaamini timu yao ya Simba bado ni imara na mengine ni ya kupita. 

“Sisi tumejiandaa kama Simba, ndiyo maana unaona tumejiandaa kama Simba na tumeshinda goli 2 – 0, watu wetu bado wana moyo sana na Simba sports Klab, angalia jezi zetu, ni lazima tuoneshe thamani ya timu yetu ndiyo maana tunasema Simba Nguvu Moja” Bw. Aliko.

Naye Mratibu wa mashabiki wa Yanga na Katibu wa Timu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Kamna Shomary amesema viongozi wameamua na kupanga siku moja ya wao kucheza bonanza ambalo wamelitumia kama njia ya kufahamiana na kuimarisha udugu.

Kwa upande wa netiboli, viongozi mashabiki wa timu ya Sim ana Yanga na wakiongozwa na Jacqueline Sikozi shabiki wa timu ya Simba na Nyabuchwenza Metusela, Mwenyekiti wa timu ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wamewasisitiza wachezaji na watumishi wa umma kuendelea kufanya mazoezi kwa kuwa michezo ni furaha, tiba, udugu n ani namna ya kuimarisha afya zao ili wanaporudi kazini wakafanye kazi kwa tija zaidi.


Na Mapuli Kitina Misalaba

Shirika la kuhudumia viwanda vidogo (SIDO) Mkoa wa Shinyanga leo Ijumaa Aprili 26,2024 limefunga mafunzo ya kutengeneza Vihenge ambapo jumla ya vijana 58 kutoka mikoa mbalimbali wakiwemo wa Shinyanga, Geita, Mwanza, Simiyu na Tabora wamenufaika na mafunzo hayo.

Mgeni rasmi katika hafla ya kufunga mafunzo hayo ni kaimu Meneja wa SIDO Mkoa wa shinyanga Bwana Joseph Taban ambaye amewapongeza vijana  kwa kuhitimu mafunzo huku akiwataka kuwa mabalozi wazuri katika jamii kwa kuhakikisha wanatumia ujuzi na maarifa waliyoyapata kuleta matokeo chanya katika jamii.

Mafunzo hayo yalianza Februari 26, 2024 kwa kundi la kwanza washiriki walikuwa 19, kundi la pili washiriki walikuwa 23 na kundi la tatu washiriki walikuwa 16 na kwamba yamefikia kilele leo Aprili26,2024 ikiwa jumla ya wahitimu 58 ambao wamehitimu na kuchukua vyeti vyao.

Bwana Taban amewasihi wahitimu hao kuendeleza umoja na ushirikiano katika kufanikisha ndoto zao kupitia ujuzi wa kutengeneza Vihenge ili kuinuka kiuchumi.

“Ni matumaini yangu kuwa mmepata dozi nzuri ya taaluma na mbinu mbalimbali za kutengeneza Vihenge, mmefundishwa masuala ya ujasiliamali, utengenezaji wa Vihenge kwa nadharia na vitendo, nadharia ya masoko, usimamizi wa fedha na urathimishaji wa biashara”.

“Ni matumaini yangu kuwa mafunzo mliyoyapata mtayatumia kwa vitendo kuhakikisha kuwa lengo la mafunzo haya linatimia, pia natarajia kuwa mafunzo haya yatawawezesha kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja, kaya na taifa kwa ujumla”.

“Mafunzo haya yametolewa kwa vijana wachache lakini wengi wangependa kupata mafunzo haya hivyo nitumie nafasi hii kuwaomba mkawe waalimu wa kufundisha vijana wenzenu kwenye maeneo yenu ya kazi ili kwa pamoja tuweze kupambana kwa vitendo kupunguza kama siyo kuondoa kabisa Sumukuvu”.

“Nitumie nafasi hii kuwapongeza kwa kuwa miongoni mwa vijana wachache waliopata bahati ya kupata mafunzo haya”.

Baadhi ya vijana ambao wamepata mafunzo hayo wamelishukuru na kulipongeza shirika la kuhudumia viwanda vidogo SIDO Mkoa wa Shinyanga kwa kutoa mafunzo hayo na kwamba wamesema yatawasaidia kwa kiasi kikuwa kuboresha utendaji wa kazi na kuzalisha bidhaa za Vihenge (Silos) na nyinginezo kwa tija ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya taifa la Tanzania.

Akisoma risala ambayo imeandaliwa na wahitimu wa mafunzo ya mradi wa kuthibiti Sumukuvu nchini kutoka kituo cha SIDO Mkoa wa Shinyanga Wanjala Daud amesema kwenye mafunzo hayo wamejifunza kwa nadharia na mada mbalimbali ikiwemo ujasiliamali, utengenezaji wa Vihenge kwa vitendo (Silos), nadharia ya masoko na huduma kwa wateja, usimamizi wa fedha pamoja na urasimishaji wa biashara.

“Tunapenda kushukuru uongozi wa SIDO na Wizara ya Kilimo kwa kutoa fursa ya mafunzo haya hakika yametujengea uwezo wa kujiamini na kuamsha ari ndani yetu ya kujiajiri na kuachana na kasumba ya kusubiri ajira”.

“Pamoja na ari na molari ya kujiajiri iliyojengeka ndani yetu tunakabiliwa na changamoto ya mitaji kwa ajili ya kununua vifaa au vitendea kazi vya kuanzisha shughuli mbalimbali kutoka na fani tulizojifunza hivyo tunaomba serikali ituangalie kwa jicho la kipekee ili tuweze kujikwamua na changamoto hii na hatimaye tuweze kujiajiri wenyewe hivyo kuchangia uchumi wetu na jamii huku tukitokomeza kabisa Sumukuvu kwa taifa letu hili la Tanzania”.

SIDO Mkoa wa Shinyanga imetekeleza mradi wa kuzuia Sumukuvu wa ‘Tanzania initiative for preventing aflatoxin contamination’ (TANIPAC) ambao upo chini ya Wizara ya Kilimo na kwamba mradi huo umelenga kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuimarisha usalama wa chakula na kuimarisha Afya ya jamii.

Mradi wa TANIPAC pia umelenga kuwezesha jamii kutumia njia sahihi na za kisasa za uhifadhi wa nafaka hususan Mahindi kutokana na Sumukuvu.

Serikali imeingia gharama kuhakikisha kuwa vijana wanapatiwa ujuzi wa kutengeneza vifaa vya kisasa na vinavyo dumu kwa muda mrefu (Vihenge) ili kutimiza adhima ya kupunguza Sumukuvu.

SIDO inawapatia wajasiliamali wadogo na wa kati huduma mbalimbali ikiwemo teknolojia na uendelezaji viwanda, mafunzo na usimamizi wa Mikoa, masoko na uwekezaji pamoja na huduma za fedha.

Kaimu Meneja wa SIDO Mkoa wa Shinyanga Bwana Joseph Taban akiwa katika zoezi la kukagua Vihenge vilivyotengenezwa na vijana ambao wamehitimu mafunzo ya kutengeneza Vihenge kupitia mradi wa kuthibiti Sumukuvu  wa ‘Tanzania initiative for preventing aflatoxin contamination’ (TANIPAC) ambao upo chini ya Wizara ya Kilimo.