Na,Jusline Marco;Arusha
Chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Arusha (APC) kimeipongeza halmashauri ya Jiji la Arusha kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo iliyotekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan madarakani.
Akitoa pongezi hizo, Mwenyekiti wa Chama hicho Claud Gwandu amesema ziara hiyo ya siku tano imesaidia kuwafanya waandishi wa habari kuwa mashuhuda wazuri kwa jamii kupitia vyombo vya habari kwa kile walichokiona kwa kuzingitia usemi usemao kuwa “kuona ni kuamini”
“Jamii imezoea kuona vyombo vya habari vikitafuta makosa zaidi ya kupongeza, lakini siyo kweli, sisi kama Chama cha Waandishi wa habari Mkoa wa Arusha tunasema wazi kuwa halmashauri ya Jiji mnastahili pongezi, tumeona shule za sekondari za maghorofa, hospitali zenye vifaa vya kisasa pamoja na huduma bora na maduka ya dawa yanayoendeshwa na serikali” Alisema Gwandu na kuongeza
Gwandu amesema pia wamezungumza na wananchi wanaopata huduma katika vituo vya afya na kukiri kuwa wanaridhishwa na huduma wanazopata hususani upatikanaji wa dawa kwa kuzingatia kuwa kwenye baadhi ya hospitali kuna maduka ya dawa ya serikali yanayouza dawa kwa bei nafuu ikiwa ni pamoja na huduma bure kwa wajawazito na wanaojifungua.
Ameongeza kuwa hospitali zote zina vifaa vya kisasa kama vile friji za kuhifadhia damu, mashine ya kupima damu, mashine ya vipimo vya maini na figo pamoja na mashine ya kung’oa kusafisha pamoja na kuziba meno. Mashine nyingine ni mashine za X-Ray kwa ajili ya mifupa, mashine ya ECO kwa ajili ya kupima valvu za moyo pamoja na mashine za ECG kwa ajili ya kupima umeme wa moyo.
Amesema pia wameshuhudia wanafunzi wamekaa madarasani kwa uwiano mazuri kwa maana ya chini ya wanafunzi 50 kwenye darasa moja ambapo wanafunzi hao waliahidi kufanya vizuri kitaaluma kutokana na kusoma katika mazingira bora.
Kwa upande mwingine Mwenyekiti huyo ametoa pongezi wa Jiji hilo kwa ukusanyaji mzuri wa mapato hali inayochochea maendeleo yanayoonekana kwa macho huku akishauri kuwepo kwa sheria ndogo za kuwataka wote wanaoomba vibali vya ujenzi kulazimika kupanda kiti kadhaa ili kuifanya Arusha kuwa kijani.
“Kupitia uongozi wako tumeona mabadiliko makubwa sana tofauti na awali, lakini ningependa kushauri kwamba mngetunga sheria ndogo za kuwataka wote wanaoomba vibali vya ujenzi kupanda miti katika eneo lake, ili mtu akitaka kujenga apande miti kadhaa kulingana na idadi mtakayosema, hii itasaidia Arusha kuwa ya kijani” Alishauri Gwandu.
Akizungumza na waandishi hao, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha John Pima (Ph.D) amesema Jiji la Arusha limevuka malengo la ukusanyaji wa mapato kwa zaidi ya asilimia mia ambapo kwa kipindi cha mwaka 2021/2022 walikusanya kiasi cha shilingi billion 23 ambapo kwa mwaka wa fedha wa kuanzia mwezi Julai mwaka huu wana lengo la kukusanya shilingi bilioni 30.
Amesema kupitia fedha za mradi wa IMF Mhe. Rais Samia aliipatia halmshauri hiyo kiasi cha shilingi bilioni 2.1 ambayo ilitumika kujenga vyumba vya madarasa 105, kutengeneza madawati 5250 pamoja na matundu 44 ya vyoo ambapo mradi huo umeshakamilika na kuanza kutumia tangu mwezi Disemba mwaka jana.
Anasema pia Mhe. Rais amewapandisha madaraja walimu 1,800 pamoja na kuajiri walimu wa masomo ya Sayansi hali iliyochochea ufauli kwa shule za msingi ambapo Jiji la Arusha limeshika nafasi ya kwanza kitaifa katika matokeo ya darasa la saba mwaka jana kwa shule za serikali.
Kwa upande wa sekta ya afya Dkt Pima amesema malengo ya serikali ni kuifanya hospitali ya wilaya ya Arusha kuwa hospitali ya Kiutalii ambayo itawatibu hadi watalii wanaofika jiji la Arusha ambapo zaidi ya shilingi milioni 500 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na serikali kuu imetoa shilingi bilioni moja ambapo malengo ni kutumia shilingi bilioni 1.5 ikiwa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha afya cha Mkonoo kitakachogharimu kiasi cha shilingi milioni 550.
Amesema ununuzi wa madawa na vifaa tiba kwa sekta ya afya umefikia asilimia 98 ikiwa ni upatikanaji na utoaji wa dawa muhimu zilizopo katika orodha ya serikali na vifaa tiba ambapo pia halmashauri hiyo kwa kushirikiana na Baraza la Madiwani umetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya vinne vya Kikanda vitakavyotoa huduma zote zinazostahili kwenye kutolewa kwa ngazi ya vituo vya afya.
“Hospitali zitasaidia kuondoa adha kwa wananchi kufuata huduma mbali, kwani tutakuwa na Kanda ya Muriet, Kanda ya Moshono, Kanda ya Olmot pamoja na Kanda ya Kaloleni, na hospitali hizi zitatoa huduma sawa ikiwa ni pamoja na rufaa ya kwenda hospitali ya Mt. Meru” Alisema Dkt Pima na kuongeza.
“Pongezi hizo nazipokea kwa niaba ya wenzangu, kwani mafanikio haya yanatokana na ushirikiano mkubwa kati ya ofisi yangu, Ofisi ya Meya kwa maana ya Baraza zima la madiwani, Mbunge wa Arusha mjini Mrisho Gambo, Mkuu wa wilaya pamoja na Mkuu wa Mkoa, lengo ni kulifanya Jiji la Arusha kuwa Jiji la mfano nchini, na kama nilivyosema awali kuwa tunafanya kazi kama timu ni imani yangu kuwa tutafanikisha” Alisema Dkt Pima.
Waandishi hao walitembelea miradi ya elimu kwenye shule ya sekondari Kaloleni, Shule ya sekondari Themi, shule ya sekondari Muriet, shule ya sekondari Arusha pamoja na shule ya sekondari Arusha Terrat.
Miradi mingine waliotembelea ni pamoja na mradi wa afya kwenye kituo cha afya Kaloleni, hospitali ya Jiji iliyopo eneo la Njiro, kikundi cha vijana cha Alinyanya wanaoshughulisha na utengenezaji waya, senyenge pamoja na kukunja bati pamoja na kikundi cha walemavu cha Muendelezo.
Post A Comment: