ZAIDI YA MILIONI 800 ZATUMIKA KUKARABATI NA KUONGEZA MIUNDOMBINU CHUO CHA UALIMU BUSTANI

Zaidi ya sh milioni 800 zimetumika kukarabati Chuo cha Ualimu Bustani kilichopo Halmashauri ya Mji Kondoa mkoani Dodoma.

Akizungumza mara baada ya kukagua miradi ya maendeleo chuoni hapo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema Serikali imetoa kipaumbele kwenye sekta ya elimu kwa kurabati, kujenga miundombinu ya taasisi za elimu ikiwa ni pamoja na kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia ili kuboresha dhana nzima ya ufundishaji na ujifunzaji.

Kuhusu  ukarabati na ujenzi unaoendelea kwenye vyuo vya ualimu Waziri Ndalichako amasema serikali inaboresha miundombinu  ya vyuo hivyo kwa awamu ambapo awamu ya kwanza imehusisha vyuo 10, awamu ya pili vyuo 8 na awamu ya tatu vyuo 9 na chuo cha Bustani kikiwemo na kufanya idadi  kufikia 27 kati ya Vyuo 35 vya Elimu nchini.

“Huu ni uwekezaji mkubwa ni vizuri miundombinu hii ikatunzwa kwa sababu serikali inatumia fedha nyingi kurudisha hadhi ya vyuo hivi. Fedha iliyoletwa katika Chuo cha Ualimu Bustani mwezi Februari ni sh milioni 874 kwa ajili ya  kukarabati na kuongeza majengo mapya ambayo ni bweni nyumba za walimu ikiwemo ya mkuu wa Chuo na kuongeza baadhi ya majengo kama Hosteli za wanafunzi wa kike,”alisema Waziri Ndalichako

Amewataka wanafunzi kuwa wazalendo, kuipenda nchi yao,  kujitambua na huku wakiilinda tunu za Taifa zilizoachwa na waasisi wa nchi hii.

“Vijana uzalendo ni pamoja na kueleza mazuri yanayofanywa na serikali yenu, hata haya yanayofanyika hapa chuo cha Bustani, myaseme kwani hali ya miundombinu kabla ya ukarabati na baada ni tofauti sana  ni jukumu lenu kueleza mafanikio ya serikali ndani ya Taasisi zenu na hata nje,” alisisitiza Waziri Ndalichako

Waziri Ndalichako ametumia fursa hiyo kuwatakia kila lakheri walimu tarajali wa mwaka wa pili wanaokwenda kuanza  mitihani ya elimu ya ualimu  Juni 29, 2020. 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Sezaria Makota ameishukuru serikali kwa namna ambavyo inapelekea miradi katika halmashauri ya Kondoa na hasa Chuo cha Ualimu Bustani na ujenzi wa ofisi za uthibiti Ubora wa Shule. Ameeleza miaka miwili iliyopita wizara ilipelekewa mradi wa maji ambao umekua msaada mkubwa kwenye  chuo hiko.

Nae Mkuu wa Chuo cha ualimu Bustani Joina Chanafi amemueleza Waziri Ndalichako kuwa chuo hicho kina jumla ya  watumishi wakufunzi 31 na kwamba hali ya itoaji elimu katika chuo hicho inaendelea vizuri bila changamoto yoyote.

Chanafi ameishukuru Serikali kwa kukarabati miundombinu ya chuo hicho ili kurejesha hadhi yake lakini pia kukiletea chuo  kwa wakati fedha za uendeshaji ugharamiaji wa maji chakula na umeme.

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )