WORLD VISION TANZANIA YAWAKOMBOA KIUCHUMI WANANCHI WA BABATI NA MONDULI

Na,Jusline Marco:Arusha

Shirika la World Vision Tanzania kupitia mradi wa Pamoja Project unaotekelezwa katika Wilaya za Babati Mkoani Manyara na Monduli Mkoani Arusha,limetoa zaidi ya mizinga 100 kwa wafugaji wa nyuki Wilayani Monduli ili kuwawezesha wafugaji hao kufuga kisasa na kuzalisha asali yenye ubora na viwango vinavyohitajika katika soko la ndani na nje ya nchi.

Mradi huo ambao umelenga kupandisha mnyororo wa  thamani ya mazao ikiwemo Asali,Kuku,Mbaazi,Ndizi na Mbogamboga,umeweza kuwanufaisha wananchi katika wilaya hizo kuwainua kiuchumi kupitia mazao wanayoyazalisha kwa kupata fedha na kuondokana na umaskini.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wafugaji na wakulima wamelishikuru shirika hilo kwa hatua waliyoitekeleza ya kuzisaidia jamii za wafugaji na wakulima kufahamu njia bora za kifugaji na kilimo ambazo zimeweza kuwapa manufaa makubwa kwao na kwa jamii zinazowazunguka.

Bi.Nesirieni Mungaya ni mjasiriamali wa zao la asali kutoka katika kikundi cha Napona kilichopo katika  kijiji cha Mswakini Wilayani Monduli  amekiri kunufaika na uzalishaji wa zao la nyuki ambalo imemuwezesha kusomesha watoto wake pamoja na kuchangia majukumu ya familia yale huku akieleza kuwa kupitia elimu ya kujitambua waliyopewa na shirika hilo jamii ya kimaasai imeweza kuondokana na mfumo dume na mila kandamizi ambazo zimekuwa zikiwanyima haki wanawake na fursa katika uletaji wa maendeleo.

“Shirika la world vision limeweza kutufungua akili zetu na kutufananisha wote kwani tumeweza kutambua haki zetu na haki za mtoto,sasa hivi kila mwanamke katika kijiji chetu anashirikiana na mume wake kwenye ufugaji wa nyuki pia ile mila ya kukeketa watoto wa kike na kuwaozesha tumeshaiacha sasa hivi tunawasomesha watoto wetu.”Alisema Nesirieni

Naye mwalimu wa vikundi vya ufugaji nyuki katika kata hiyo Bwn.Lengishon Minyali amesema kuwa mradi huo umekuwa mkombozi katika jamii yao kwani wameweza kuendesha maisha yao binafsi na familia zao kutokana na fedha wanazozipata kupitia asali wanayoivuna na kuiuza katika masoko yao.

Awali akizungumza na waandishi wa habari wakati alipotembelea moja ya miradi inayotekelezwa na shirika hilo Afisa mwezeshaji na msimamizi rasilimali za maliasili,Deogratius Martine amesema mradi huo unafanya kazi na vikundi vya uzalishaji wa asali vipavyo 26 kwenye vijiji 33 ambavyo mradi unahudumia ambapo shirika liliamua kutoa elimu ya ufugaji nyuki kwa wananchi hao ili kwa pamoja waweze kuingia katika kilimo cha kisasa cha ufugajj nyuki kitakacho waingizia kipato ambacho wataweza kuhudumia familia zao.

“Ufugaji huo wa kisasa utamuwezesha mfugaji kupata kilo 6 hadi 10 kwa mvuno 1 ambapo mfugaji anaweza kuvuna mara 4 hadi 5 kwa mwaka mmoja  tofauti na hapo awali ambapo mfugaji alikuwa akipata kilo 2 hadi kilo 2 na nusu kwa mwaka hali iliyokuwa ikiwafanya wapate kipato kidogo kisichokidhi mahitaji yao.”Alisema mwezeshaji huyo.

Sambamba na hayo Mradi wa Pamoja Project umeweza kufikia vijiji 24 vilivyomo wilayani Babati na vijiji 9 vilivyomo Monduli katika uzalishaji wa migomba iliyoboreshwa ambapo kijiji cha Gidabagara ni moja kati ya vijiji 23 vilivyofikiwa na mnyororo wa thamani wa migomba ambayo hulimwa na kuboreshwa.

Akieleza namna mradi huo ulivyowakomboa wakulima wa zao la migomba Afisa mwezeshaji na msimamizi wa mazingira kutoka World Vision,Labu Dawi amesema kwa wastani mkulima wa zao la ndizi huvuna kati ya mikungu 10 hadi 20 kwa siku katika shamba la hekari moja ambapo kwa mwala mmoja huvuna mikungu 1350 ambapo pamoja na uzalishaji huo kuwa mkubwa bado kuna changamoto ya uhitaji mkubwa wa soko.

Joseph Robert ni mmoja kati ya wanakikundi wa kikundi cha Mshikamano kinachijishughulisha na ulimaji wa zao la Ndizi amesema kupitia kilimo hicho njaa na umaskini katika kijiji chao imekuwa historia kwani kila mwana kijiji amehamasika kulima zao hiyo ambayo linawaingizia kipato kwa muda mfipi na wakati wote.

Pamoja na hayo Afisa Kilimo kutoka katika shirika hilo Ndg.Stanford Mwambola amesema mradi huo ambao ulianza mwaka 2013 ulilenga kuinua kipato cha  jamii ya wakulima na wafugaji katika wilaya za Babati na Monduli ambapo walilenga kuwafikia wananchi 9000 pamoja na kuangalia ustawi wa mtoto wa kike kwa kupinga mila kandamizi ikiwemo ukeketaji wa mtoto wa kike na ndoa za utotoni.

Hara hivyo mradi huo ulianzishwa kwa lengo la kuinua kiuchumi vijiji vilivyosahaulika kwa kupandisha mnyororo wa thamani katika mazao ili kuweza kuvikwamua vijiji hivyo kiuchumi kwa kumuwezesha mfugaji na mkulima kuondokana na kilimo na ufugaji wa kienyeji kisha kuzalisha kisasa na kwa tija zaidi.

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )