Wenyeviti Wa Vijiji Wadai Posho,Wachoka Kuitwa Waheshimiwa Wakiwa Mkono Mtupu

 

Baadhi ya wenyeviti wa vijiji vya tarafa ya Makambako wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuwasilisha kero zao kwa mbunge wa jimbo la Lupembe

Baadhi ya wenyeviti wa vijiji tarafa ya Makambako wakimsikiliza mbunge wa jimbo la Lupembe Edwirn Swale mara baada ya kuwasilisha kero zao katika utendaji kazi.

Mbunge wa jimbo la Lupembe Edwirn Swalle Katikati akifafanua baadhi ya hoja za wenyeviti namna atakavyozitafutia ufumbuzi huku akiwaahidi kuwafikisha bungeni.


Na Amiri Kilagalila,Njombe

 

Wenyeviti wa serikali za vijiji vya tarafa ya Makambako jimbo la Lupembe mkoani Njombe wamesema wamechoka kuitwa waheshimiwa bila kulipwa hata posho wakati wamekuwa na majukumu makubwa ya kuwatumikia wananchi.

 

Mbele ya mbunge wa jimbo la Lupembe Edwin Swalle alipozulu katika tarafa hiyo kwa lengo la kukutana na wenyeviti wote wa vijiji na kusikiliza changamoto za maeneo yao ya kiutawala baadhi ya wenyeviti hao akiwemo Eliud Kaduma kutoka Kichiwa,Fredrick Damian kutoka Mihale Ninga na Ayub Kipuge kutoka kijiji cha Tagamenda wamesema wanashangaa kuona diwani,mbunge hadi Rais ambao nao ni viongozi wa kuchaguliwa kama wao wanalipwa mishahara na posho lakini wao hawapati hata posho kwa miaka mingi sasa.

 

“Tumekuwa tukifanyia sifa,hii sifa ya kuitwa mwenyekiti tumechoka maana hatuli na hali ni mbaya na ukizingatia kuna wengine wanapata posho na wengine wanazo lakini wanalalamika kwamba mi chache hasa sisi ambao hatuna kabisa ni shida lakini kazi tunafanya na sisi ndio wajenga nchi”alisema Eliud Kaduma mwenyekiti wa kijiji cha kichiwa Kichiwa

 

“Sisi wenyeviti wa vijiji tunachaguliwa kama mbunge na Mh,Rais lakini kwenye posho tumesahauliwa.Wenzetu wabunge wanapata na madiwani wanapata sasa sijajua tuna dhambi gani wenye viti wa vijiji tuliyoitenda kwenye nchi hii.Kama tunasimamia maendeleo na amani ya vijiji halafu tukatupwa kiasi hicho”alisema Ayub Kipuge kutoka kijiji cha Tagamenda

 

Wengine wamepaza sauti zao wakidai changamoto za miundombinu ya barabara,afya,elimu na maji na kwamba wanamuomba mbunge huyo awasaidia namna ya kuzitatua.

 

Akitolea ufafanuzi wa changamoto hizo mbunge wa jimbo la lupembe Edwin Enosy Swalle amesema atakwenda kuzifanyia kazi kero hizo huku akiahidi kuwaalika bungeni mwezi wa sita mwaka huu wenyeviti wote ili pia wakakutane na waziri wa Tamisemi awasikilize kilio chao.

 

“Hili jambo la posho ninalifahamu ninaomba nikatafutie majibu yake kwasababu nimeshalifanyia utafiti kidogo”Alisema Swalle

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )