WAZIRI UMMY MWALIMU AKUTANA NA WADAU WA MCHANGA JIJINI DAR ES SALAAM.

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira Mhe. Ummy Mwalimu akizungumza katika mkutano wa  wadau wa uchimbaji mchanga wa Mkoa wa Dar es Salaam (hawapo pichani). Mkutano huo umefanyika   katika ukumbi wa Impala Mbezi Beach Makonde jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Mhe. Daniel, chongolo akitoa ufafanuzi wakati wa Mkutano huo ulioshirikisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira na Wadau wa uchimbaji mchanga wa Mkoa wa Dar es Salaam (Hawapo pichani), uliofanyika ukumbi wa Impala Mbezi Beach Makonde jijini Dar es Salaam.

Mbunge wa Jimbo la Kawe Mhe. Josephat Gwajima, akitoa ufafanuzi wa jambo katika mkutano wa wadau wa uchimbaji mchanga wa Mkoa wa Dar es Salaam (hawapo pichani, uliofanyika katika ukumbi wa Impala Mbezi Beach Makonde jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Mhandisi Samuel Gwamaka.


Sehemu  ya Wadau wa uchimbaji mchanga wa jijini Dar es salaam wakimsikiliza kwa makini  Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira Mhe. Ummy Mwalimu (hayupo pichani) katika Mkutano huo.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mh. Ummy Mwalimu ameziagiza Halmashauri zote Nchini kusimamia kwa karibu usafishaji wa mito kwa kuondoa mchanga katika maeneo yao ili kutunza mito. Amesema hayo alipokua kwenye kikao cha pamoja na wadau wa uchimbaji mchanga katika jiji la Dar es Salaam kilichofanyika jijini humo katika ukumbi wa Impala Mbezi Beach.

 Aidha  amewaruhusu wachimbaji hao  kuendelea kusafisha mito kwa kuchimba mchanga na ameomba wampatie siku saba ili kuweza kutoa muongozo stahiki juu ya usafishaji mito. Waziri Ummy pia amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam kuitisha kikosi kazi ili kutengeneza muongozo wa jinsi ya kusafisha mito.

 ‘Tutaendelea kusafisha mito kwa kuondoa mchanga, kwani mito lazima isafishwe ili kuruhusu mtiririko mzuri wa maji na kuepuka mafuriko. Naomba siku saba za kutoa Mwongozo wa njia sahihi za kusafisha mito bila kuathiri Mazingira.’ Alisema Waziri Ummy. Katika kipindi hiki cha kusubiri mwongozo shughuli za usafishaji wa Mto Mpiji juu na Mto Mpiji chini zitaendelea kama kawaida kwa wale wenye vibali.

 Waziri Ummy ameliambia jeshi la Polisi kutokamata wachimbaji wadogo wa  mchanga ikiwa wana vibali vyote vinavyotakiwa. ‘Msikamate wala kumuonea  Mchimbaji ambaye tayari ana vibali kutoka Mamlaka za Serikali’ alifafanua Waziri Ummy.

 Naye Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Daniek Chongolo akiongea katika Mkutano huo wakati anamkaribisha Waziri Ummy kuzungumza na Wachimbaji hao alisema kuwa Wadau hao wa kuchimba mchanga wako tayari kupokea maagizo na maelekezo  ya Waziri kuhusiana na biashara hiyo ya mchanga.

 Sambamba na hilo Waziri Ummy ameiagiza Mamlaka ya Bonde la Wami Ruvu kutoa ramani ya Mito, kingo zake na historia ili kuwezesha usimamizi bora wa mito hii.

 Akiongea katika Mkutano huo Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Usimamizi na Hifadhi ya mazingira Dkt Samuel Mafwenga alisema kuwa NEMC ni kama askari wa mazingira sababu wao ndo wasimamizi wakubwa wa mazingira na sheria yake. 

Aliendelea kusema kuwa sheria ya mazingira hairuhusu shughuli zozote za kudumu kufanyika kwenye maeneo ya mito. Akifafanua sheria hio ya Mazingira inavyoainisha kuhusu uchimbaji wa Mchanga  alisema kuwa kinachofanyika katika mabonde ya Mito ni kusafisha Mto na sio kuchimba mchanga.

   “Ukisema unachimba mchanga umevunja sheria kwasababu hauna leseni ya kuchimba mchanga, lakini unaposafisha mto, mwenye mamlaka ya kukupa vibali ni bonde husika  na vibali lazima viendane na taratibu na masharti ya usafishaji wa ile mito, kusafisha mito lazima kuendane na uhifadhi wa mazingira alisema Injinia Mafwenga.

 Aidha akichangia katika Mkutano huo mmoja wa Wachimbaji hao  wa mchanga wamesema kuwa Serikali inatakiwa kuwathamini wachimbaji hao kama wachimbaji wakubwa. Lakini pia  amesema upo mgongano wa Taasisi za Serikali  kwa kuweka urasimu na kusababisha vibali kuchelewa.

 Mkutano huo umeandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Kawe Mh. Joseph Gwajima ili kuweza kuwasilisha kero za Wananchi wake ambao ni wachimbaji wa mchanga wadogo kwa Waziri mwenye dhamana ya Mazingira.


CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )