WAZIRI NDAKI ATAKA KUAINISHWA MIPAKA YA HIFADHI YA BAHARI KUONDOA MIGOGORO NA WAVUVI


Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na baadhi ya wakazi
wa Kata ya Kilindoni iliyopo Wilaya ya Mafia Mkoani Pwani alipofanya
ziara ya kikazi ya siku mbili wilayani humo na kutaka wavuvi waendelee
na shughuli zao kwa kutumia taa kuvua samaki nyakati za usiku wakati
wizara hiyo ikifanya tafiti zaidi za taa bora ambazo hazina madhara
katika shughuli za uvuvi. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)


Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akijadiliana jambo na
Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na
Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah wakati alipofanya
ziara ya kikazi ya siku mbili wilayani humo. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kulia) akipata
maelezo kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah wakati wakiwa kwenye boti
maalum yenye kioo chini ambayo imewawezesha kujionea maeneo ya mazalia
ya samaki yaliyopo kwenye Bahari ya Hindi, wakati Waziri Ndaki
alipofanya ziara ya kikazi ya siku mbili Wilayani Mafia. Pembeni ya Dkt.
Tamatamah ni Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)

Na. Edward Kondela


Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amekitaka Kitengo cha Hifadhi ya
Bahari na Maeneo Tengefu (MPRU) kuhakikisha hadi kufikia Mwezi Agosti
Mwaka 2021 kinaweka alama za mipaka katika maeneo yote ya hifadhi za
bahari ili kuondoa migogoro kati yao na wavuvi.


Akizungumza
jana (23.02.2021) na wananchi katika Kata ya Jibondo iliyopo Wilaya ya
Mafia Mkoani Pwani, Waziri Ndaki ametaka kuwekwa kwa alama za mipaka
hiyo baada ya baadhi ya wananchi kulalamikia kutozwa faini mara kwa mara
kwa tuhuma za kufanya shughuli za uvuvi kwenye maeneo hayo ambayo
hayaruhusiwi kisheria kwa shughuli hizo.


Aidha,
Waziri Ndaki akiwa ameambatana na naibu waziri wa wizara hiyo Mhe.
Pauline Gekul, amewataka wavuvi kuhakikisha pindi wanapokamatwa kwa
makosa mbalimbali ambayo ni kinyume na sheria ya uvuvi kuhakikisha
wanapatiwa risiti inayotambulika na serikali ya kieletroniki (EFD) na
kuonya watumishi wa serikali wanaopokea fedha za faini bila kutoa risiti
hizo.


“Tuweke
mipaka ya hifadhi ieleweke hapa ndiyo mwanzo na hapa ndiyo mwisho, hadi
mwezi wa nane maeneo tengefu yawe na mipaka yake ya hifadhi ya bahari,
pia tushirikishe wananchi na viongozi wao siyo kuweka tu mipaka, pia kwa
mtu anayekutwa na kosa la kwenda kinyume na sheria ya uvuvi akilipa
faini apewe risiti ya serikali ya kieletroniki (EFD).”
Amesema Waziri NdakiPia,
waziri huyo ametaka kufanyika kwa utafiti zaidi ndani ya mwezi mmoja
juu ya matumizi ya aina mbalimbali za nyavu za uvuvi baada ya kupata
malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wavuvi ambao wamekuwa
wakilalamikia baadhi ya nyavu ambazo wanatakiwa kuzitumia kisheria kwa
ajili ya uvuvi kutokuwa na sifa ya kukamata mazao ya samaki katika
maeneo yao.


Amemuelekeza
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt.
Rashid Tamatamah kuhakikisha kufikia Tarehe 23 mwezi Machi Mwaka 2021,
awe amempatia taarifa hiyo ili iweze kutoa mwongozo wa maamuzi ya nyavu
ambazo zina tija kwa shughuli za uvuvi.


Katika
mkutano huo wa hadhara na wananchi wa Kata ya Jibondo Wilaya ya Mafia
Mkoani Pwani, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amepiga
marufuku kitendo cha baadhi ya maafisa uvuvi kuwakamata wafanyabiashara
wa samaki waliyopo mitaani yakiwemo maeneo ya kuuzia vyakula kwa madai
samaki wanaouzwa katika eneo hilo hawana sifa kisheria badala yake
watafute vyanzo vya maeneo ambayo watu wanavua samaki hao.


“Kuna
mambo ambayo sipendi sitaki kabisa kusikia afisa uvuvi anaenda sokoni
kutafuta samaki ambao wapo kinyume cha sheria na kuwanyanyasa akinamama
wanaokaanga samaki, wakiona samaki wa namna hiyo wanapaswa kuwauliza
aliyewauzia ili wapate chanzo halisi cha samaki walipovuliwa badala ya
kumnyanyasa mfanyabiashara ambaye anauza chakula au kununua samaki
anapeleka nyumbani kwa ajili ya mboga.”
Amefafanua Waziri NdakiKuhusu
kilimo cha zao la mwani Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amesema zao hilo limekuwa
likilalamikiwa kwa kuuzwa kwa bei ndogo hali ambayo imekuwa ikiwafanya
wakulima hao wasipate mafanikio na kuwataka wakulima wasiingie mikataba
ya kuuza zao la mwani badala yake wauze kwa wafanyabiashara ambao
wanakuwa na bei nzuri yenye tija kwao.


Dkt.
Tamatamah amesema wizara itahakikisha inasimamia zao hilo kwa kuwa
limekuwa mkombozi mkubwa kwa akinamama wengi katika Ukanda wa Pwani
pamoja na kuwataka waliongezee thamani kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali
zikiwemo sabuni.


Naye
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia Mhe. Juma Salum Ali
amepongeza namna Wizara ya Mifugo na Uvuvi inavyohakikisha inasimamia
maeneo ya hifadhi ya bahari kupitia Kitengo cha Hifadhi ya Bahari na
Maeneo Tengefu (MPRU) huku akitaka kutatuliwa kwa baadhi ya changamoto
ambazo zinaleta hali ya kitengo hicho kushindwa kushirikiana na
wananchi.


Mhe.
Ali amefafanua kuwa baadhi ya watumishi wa kitengo hicho wamekuwa
wakishindwa kufanya kazi kwa kufuata ueledi wa kazi yao na kuweka
maslahi binafsi hali ambayo imekuwa ikizorotesha hali ya uhifadhi
ukizingatia Wilaya ya Mafia bado ina maeneo mengi ambayo yana wingi wa
samaki kwa ajili ya shughuli za uvuvi.


Kwa
upande wao baadhi ya wananchi waliofika katika mkutano huo wamemuelezea
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki changamoto mbalimbali
wanazokabiliana nazo na kuelezea namna walivyo na imani kubwa na waziri
huyo katika kutatua changamoto zao ili waweze kufanya shughuli za uvuvi
bila bughudha na waweze kufuata sheria za nchi.


Aidha,
Waziri Ndaki akiwa katika Kata ya Kilindoni Wilayani Mafia, amezungumza
na baadhi ya wavuvi na kuwataka wafanye shughuli za uvuvi kwa kutumia
taa nyakati za usiku wakati Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikiendelea kufanya
tafiti ya taa bora zaidi ambazo hazina madhara wakati wa kuvua samaki.


Mhe.
Ndaki amelazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya kulalamikiwa na baadhi
ya wavuvi kushindwa kufanya shughuli zao nyakati za usiku kwa kuzuiwa
kutumia taa kama chambo kwa ajili ya kukamatia samaki.


Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amefanya ziara ya kikazi ya siku
mbili katika Wilaya ya Mafia Mkoani Pwani akiambatana na Naibu Waziri
Mhe. Pauline Gekul ambapo Waziri Ndaki amepata fursa ya kuzungumza na
baadhi ya wavuvi na kujionea hifadhi ya bahari na maeneo tengefu.

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )