WAZIRI KAIRUKI ATEMBELEA KIWANDA CHA KATANI KISANGARA,ATAKA VIJANA KUTUMIA MIKOPO INAYOTOLEWA NA HALMASHAURI

Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu -Uwekezaji Angela Kairuki akizungumza jambo wakati akitizama mtambo wa kutengeneza kamba katika kiwanda cha Katani cha Kisangara kinachomilikiwa na mfanyabiashara Mohamed Dewji kilichopo wilayani Mwanga,wengine kutoka kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Mwanga ,Thomas Apson akifuatiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mwanga ,Zefrin Lubuva na kulia ni George Mwamakula -Meneja.
Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu -Uwekezaji Angela Kairuki akitizama bidhaa inayotumika kutengeneza magunia inayotokana na zao la Katani alipotembelea kiwanda cha Katani cha Kisangara wilayani Mwanga kinachomilikiwa na mfanyabiashara Mohamed Dewji,wengine katika picha kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mwanga ,Zefrin Lubuva na kushoto mwa waziri kairuki ni George Mwamakula -Meneja.
Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu -Uwekezaji Angela Kairuki akizungumza jambo na uongozi wa kiwanda hicho.
Baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda cha Katani cha Kisangara wakiendelea na shughuli za ukusanyaji wa bidhaa inayotumika kutenegeneza kamba na magunia.

Na Dixo Busagaga ,Mwanga 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji, Angela Kairuki, amewataka wananchi, kutumia fursa ya mikopo inayotolewa na Halmashauri za Wilaya, kwa ajili ya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu, kuwekeza katika tasnia ya Mkonge, ambayo imeonekana kuwa na chachu kubwa ya maendeleo.

Kairuki, alitoa rai hiyo , mara baada ya kutembelea Shamba la Mkonge la Kisangara,lililoko chini ya Kampuni ya Mohamed Enterprises (METL) Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, na kupewa taarifa ya uwepo wa upungufu wa mashine kwa ajili ya kuchakata zao hilo, ambapo alisema ni fursa kubwa kwa wananchi katika kujipatia kipato

Alisema wananchi wanaweza wakajiunga katika vikundi kama ambavyo imekuwa ikielekezwa na Halmashauri, na kupewa mkopo, ambao watauwekeza katika ununuzi wa Mashine ya kuchakatia Mkonge,ijulikanayo kwa jina maarufu kama Corona na kuweza kupiga hatua kimaendeleo.

“Nimeelezwa  kuwa, kuna upungufu wa mashine za kuchakata Mkonge,hivyo wakati mwingine mkonge upo ila hakuna mashine ya kuchakata, Sasa viongozi wa Halmashauri na hata Mkoa, tuendelee kuwahamasisha wananchi wawekeze katika tasnia ya zao la mkonge, ambako kumeonekana kuwa na fursa nzuri” alisema Kairuki na kuongeza kuwa,

“Tunaweza pia kutumia  fursa ile ya mikopo ya wanawake,Vijana na watu wenye ulemavu,kuona ni namna gani kikundi cha pamoja au vikundi vya ushirika vinaweza kuwekeza katika Corona (Mashine ya kuchakatia Mkonge) wananchi wachangamkie fursa hii,ili kumaliza tatizo la upungufu wa mashine hizi”

Aidha alitumia pia nafasi hiyo, kuwataka Viongozi wa Halmashauri,kutoa elimu kwa wananchi  na kuelezea fursa zilizopo katika Mkonge,ili kupanua wigo wa uwekezaji katika kilimo hicho, kwa kuwa mahitaji ya Mkonge bado ni makubwa nchini na hata duniani.

 “Mahitaji ya Mkonge bado ni makubwa, hivyo tuendelee kuhamasisha wananchi na kuwapa elimu ili wale wenye maeneo yanayofaa kwa kilimo hicho, waweze kuwekeza huko,lakini pia tunaendelea kukaribisha wawekezaji wengine, kuingia katika uchakataji wa zao hili, kwani kwa sasa Vipo viwanda zaidi ya 11 vikubwa na vya kati vya kuchakata mkonge,na viwanda vidogo zaidi ya 70 kwa ajili ya uchakataji wa zao hili”alisema.

Awali akizungumza Meneja wa kituo cha uwekezaji Kanda ya Kaskazini, Daudi Riganda, aliutaka uongozi wa shamba hilo la Mkonge, kuongeza uzalishaji, na kuwekeza zaidi katika zao hilo, ili kuweza kutengeneza faida.

“Bado hatujaridhika na namna ambavyo muwekezaji ameweza kutumia fursa ya uwekezaji katika kilimo hiki cha mkonge,ikilinganishwa na rasilimali ya Ardhi aliyo nayo na hali ya hali ya hewa iliyopo,hivyo ningeshauri,wawekezaji watakaopewa nafasi ya kuwekeza  katika kilimo cha Mkonge, waongeze uzalishaji na kuwekeza kwa tija zaidi”alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Thomas Apson,alisema kwa sasa wanajipanga kutoa elimu na kuhamasisha wananchi, kujiingiza katika Kilimo cha Mkonge,ili kuweza kuboresha maisha yao kwa kutumia fursa zilizopo nhini.

“Kuna haja ya sisi kama Wilaya, kukaa na Idara ya Kilimo na Biashara,kuona ni namna gani tunahamasisha wananchi, kwani changamoto yetu ni kuwapata watu ambao wataitumia mikopo na kuirejesha kwa wakati,sasa tunakwenda kuhamasisha Kilimo na kutoa fursa kwa wananchi, kwani kufanikiwa kwetu kama viongozi ni kuona tunaboresha maisha ya viongozi tunao waongoza”alisema
CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )