Waziri Jafo aipongeza Taasisi ya Dk. Msuya Foundation

UZALENDO! Ndio kauli ambayo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo ameitumia kuipongeza Taasisi ya Dk Msuya Foundation kwa kuwezesha kusaidia ukarabati samani za Shule ya Sekondari Ibihwa iliyopo wilayani Bahi, Dodoma.

Waziri Jafo ameipongeza taasisi hiyo inayoongozwa na Dk. Ombeni Msuya kwa moyo wao wa kizalendo uliowezesha ukarabati huo wa Viti 76 na Meza 45 kwenye shule hiyo ikiwa ni kuunga mkono juhudi za serikali za kuinua elimu nchini.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa samani hizo na Dk Msuya, Waziri Jafo amesema kitendo kilichofanywa na taasisi hiyo ni cha kizalendo na kinapaswa kuungwa mkono na kwamba serikali itaendelea kushirikiana nae katika kuwahudumia watanzania.

Jafo ameipongeza taasisi hiyo kwa namna ambavyo imekua ikiguswa kushirikiana na serikali kwenye kuleta maendeleo ambapo hata katika janga la Corona walikabidhi vifaa vya kujikinga na Ugonjwa huo wilayani Mwanga, Kilimanjaro pamoja na maeneo mengine nchini.

” Nikushukuru sana Dk Msuya, nafahamu ulikuja na tafiti yako kuangalia jinsi gani changamoto tulizonazo tunaweza kuzifanyia kazi ili kukuza sekta yetu ya elimu na ukaja na majibu ya kufanyia ukarabati samani zetu na leo unatukabidhi hapa kwa ajili ya watoto wetu kutumia.

Hii si kwa sababu una kipato kikubwa sana bali ni moyo wa kizalendo na wenye imani ulionao kwa watanzania wenzako. Ungeweza kupeleka kwenu Mwanga lakini ukasema hapana, hawa watoto wa Bahi nao ni watanzania wenzangu, nakupongeza na nikusihi uendelee na moyo huohuo,” Amesema Waziri Jafo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Dk Ombeni Msuya amesema waliguswa na kazi kubwa inayofanya na Rais Dk John Magufuli katika kuwatumikia watanzania hivyo nao wakaona wamuunge mkono kwenye sekta ya elimu.

Amesema watanzania wanapaswa kuwa na utaratibu wa kufanya ukarabati wa samani kwenye taasisi kwani fedha nyingi zinaweza kuokolewa kwa kutengeneza samani zilizoharibika kuliko kununua mpya.

” Mhe Waziri tunashukuru sana kwa namna ambavyo Wizara yako na uongozi wa Wilaya kupitia Mhe DC ulitupa ushirikiano katika kufanikisha jambo hili, tunaamini samani hizi zitakua msaada kwa watoto wa kitanzania wenye ndoto za kufanikiwa kupitia elimu.

Serikali yetu chini ya Rais Magufuli imefanya kazi kubwa kwenye kila nyanja, ni jukumu letu kama watanzania kuonesha uzalendo wetu katika kumuunga mkono, niahidi hapa kwamba taasisi yetu itaendelea kukarabati samani kwenye shule zetu nchini lengo likiwa kumtia moyo Rais kwa kazi kubwa anayofanya,” Amesem Dk Msuya.

Amesema kukamilika kwa ukarabati maana yake wanafunzi 76 ambao walikua hawana viti sasa watapata na wengine 45 waliokua hawana meza sasa watanufaika ma meza hizo.

” Ukarabati huu Mh Waziri pia unaokoa fedha nyingi, tulipata taarifa kutoka kwa Mkuu wa Shule kwamba ununuzi wa kitu kimoja unagharimu Sh 60,000 sasa ukiangalia idadi ambayo sisi tumekarabati utaona tumeokoa kiwango kikubwa cha fedha kingeenda kufanyia shughuli nyingine.

Hivyo tunachotaka kusema leo ni kwamba kuna uwezekano mkubwa katika taasisi zingine zote kuchukua uamuzi wa kukarabati maana ni nafuu pia. Sisi tumetumia kiasi kisichozidi Sh Milioni Moja kwa sababu tumetumia Sh 934,000 hivyo nitoe rai kwa watanzania kuwa na utaratibu huu, ” Amesema Dk Msuya.

Nae Mkuu wa Shule hiyo, Aldin Mnaro ameishukuru Serikali kwa kuamua kurejesha masomo ifikapo Juni 29 na tayari washaanza kuandaa mazingira ya kuwapokea wanafunzi huku wakichukua tahadhari ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid19.

” Niipongeze serikali kwa kazi kubwa wanayofanya kwenye sekta ya elimu, lakini pia niishukuru taasisi ya Dk Ombeni Msuya kwa ukarabati huu walioufanya ambao sasa unaifanya Shule yetu isiwe na upungufu wa samani na kuahidi kuvitunza kwa muda mrefu zaidi, ” Amesema Mwl Mnaro.

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )