Waziri Biteko : Wizara ya Madini Imejenga Mfumo unaofanya kazi

Waziri wa Madini Doto Biteko amesema anajisikia fahari kutokana na utendaji  ulioonesha matokeo Chanya kwenye Sekta ya Madini ambao umechangiwa na  Watumishi wa Wizara na Taasisi zake na kuongeza kuwa, suala hilo limewezesha kujengwa kwa mfumo unaofanya kazi,  na hivyo  kuifanya Sekta  husika kuchangia  kiuchumi  katika maendeleo ya Taifa tofauti na ilivyokuwa awali.

Waziri Biteko ameyasema hayo wakati wa kikao na Watendaji wa Wizara na Taasisi ikiwa ni sehemu  ya maandalizi ya kuelekea kuwasilishwa Bajeti ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 inayotarajiwa kuwasilishwa Bungeni  Aprili 20 na 21,  jijini Dodoma.

Ametumia fursa hiyo kuwashukuru na kuwapongeza  watumishi wote wa wizara na taasisi zake kwa ushirikiano  ambao  umewawezesha wao kama viongozi wakuu wa wizara kutekeleza majukumu yao kikamilifu  katika  Mwaka wa Fedha 2019/2020.

“ Ninawashukuru sana kwa kunisaidia, Tume ya Madini, Wizara, STAMICO na Taasisi zote, ninayo mengi ya kuzungumza kuliko ninyi, mmenifanya nijisikie fahari sana. Kila mmoja amewajibika kwa upande wake na ile tabia ya kulalamika imepungua na mmefanya kazi kubwa,” amesisitiza  Waziri Biteko.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo ameipongeza Tume ya Madini kutokana na Usimamizi wa Sekta ya Madini, ukusanyaji wa maduhli, utoaji leseni na kueleza kuwa, utekelezaji thabiti wa majukumu hayo umechangia kuleta mabadiliko kwenye sekta ya madini na kuongeza, “Ninawaomba watumishi wote muendeleze mshikamano huo,’’.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amechukua fursa hiyo kuwapongeza  na kuwashukuru Waziri na Naibu waziri kwa ushirikiano  ambao wamempatia katika utekelezaji wa majukumu yake kama Katibu Mkuu na kueleza kuwa, ushirikiano huo umeiwezesha wizara kupunguza kero sugu za wananchi katika sekta ya madini. Pia, amewapongeza  watendaji wa wizara, taasisi na watumishi wote kwa ushirikiano ambao wameuonesha katika kipindi chote ambacho amekuwa kiongozi katika wizara hiyo.

Akitoa shukrani katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula amewashukuru viongozi wakuu wa wizara kwa kutambua mchango na kazi za Tume ya Madini na kuongeza kuwa, mafanikio ya taasisi hiyo pia yamechangiwa na taasisi hiyo kuwajengea ari ya kujiamini watumishi wake.

Kwa upande wa Viongozi wengine walioshiriki kikao hicho, wamepongeza ushirikiano, umoja na mshikamano uliooneshwa na viongozi wa Wizara na kueleza kuwa, ulifanya utekelezaji wa majukumu kuwa mwepesi.

Mbali na kikao hicho kujadili masuala ya bajeti, pia,  viongozi wakuu wametumia fursa hiyo kujadili masuala kadhaa ikiwemo suala la ugonjwa wa virusi vya corona (COVID 19)  na uhusiano wake katika sekta husika, biashara ya madini katika kipindi hiki cha ugonjwa huo pamoja na namna ya kuiendeleza zaidi sekta ya madini ili iweze kuchangia zaidi katika pato la taifa.

Vilevile, wakuu wa Idara na Taasisi wameshauriwa kuwahimiza wote walio chini yao kuendelea kuzingatia maelekezo ya kujikinga na virusi vya corona kama yanavyotolewa na Wizara ya Afya.

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )