Watumishi waliokwamisha maendeleo ya miaka mitatu ya Halmashauri kuwajibishwa

Mkuu wa mkoa
wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Nkasi kuwawajibisha watumishi wote walioisababishia halmashauri hiyo kupata
hati yenye shaka na kumpatia taarifa ya hatua alizochukua kwa watumishi hao
ndani ya siku saba kabla ya mabaraza ya madiwani kuvunjwa.

Amesema kuwa
kwa mujibu wa maelekezo ya Katibu Mkuu Ofisi ya Raisi Tawala za Miko ana
Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) yaliyotolewa tarehe 24, April, 2020 kuhusu
kushughulikia hoja na mapendekezo ya CAG, pamoja na mambo mengine imeelekezwa
kuwa Halmashauri zilizopata Hati yenye Shaka zimepoteza sifa za kupatiwa fedha
za utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika kipindi cha miaka mitatu ijayo na
hivyo kuchelewesha maendeleo kwa wananchi.
“Kwa kupata
hati yenye shaka, halmashauri ya wilaya ya Nkasi inapoteza sifa za kupatiwa
fedha za utekelezaji wa miradi ya kimkakati ambayo lengo lake ni kupoteza
mapato katika halmashauri, hii ni adhabu kubwa sana katika halmashauri yetu,
haipendezi, pengine wengine walikuwa wanaichukulia kijuu juu, miradi ya
kimkakati ni miradi mukubwa ambayo halmashauri zimepewa nafasi ya kubuni na
kupatiwa fedha ya kutekeleza, kama ni stendi za mabasi, maghala au kumbi
zamikutano,” Alisema.
Na kuongeza
kuwa ,” Hawa waliotufikisha hapa, hawawezi kuachwa hivi hivi, ni lazima
wachukuliwe hatua kali za kinidhamu na Mkurugenzi nimekupa siku saba, uwe
umetoa adhabu hii, nipate taarifa ndani ya siku saba, iwe nimepata taarifa ya
namna hawa watu watakavyoshughulikiwa kinidhamu, hatuwezi kuendelea namna hii
watu wanafanya mzaha, wanafanya uzembe, halafu halmashauri inabeba mzigo wa
hawa watu wachache wazembe kwanini?” Alikemea.
Wakati
akieleza miongoni mwa sababu zilizosababisha halmashauri hiyo kupata Hati ya
Mashaka kwenye hesabu za kuishia tarehe 30, Juni 2019 Mkurugenzi Mtendaji wa
halmashauri hiyo alisema kuwa Ukaguzi wa mtiririko wa fedha (Cash Flows
Statements) kwenye kitabu cha hesabu ulionesha kuwa na upungufu wa shilingi
2,528,347,000/=.
“Ukaguzi wa
Mtiririko wa fedha kwenye kitabu cha hesabu ilibainika kuwa Halmashauri
imeonesha mtiririko wa fedha uliotoka kuwa Shilingi 16,827,818,000 ikiwa ni
mishahara, malipo ya vibarua na haki mbalimbali za watumishi, hata hivyo kwenye
mchanganuo ilionekana madai ya watumishi yamepungua kwa Shilingi 383,690,000 hivyo
kufanya madai ya watumishi kuoneshwa pungufu kwa jumla ya Shilingi
2,528,347,000/=,” Alifafanua.
Aliongeza
kuwa kwa upande wa magari na pikipiki, mali za halmashauri, halmashauri
ilionesha jumla ya Shilingi 554,292,000/= lakini baada ya daftari la mali za
kudumu kupitiwa ilionesha jumla ya shilingi 612,940,420 na khivyo kuonesha
upungufu wa Shilingi 58,648,420/=.
Kwa upande
wake Afisa Serikali za Mitaa mkoa wa Rukwa Albinus Mgonya alisema kuwa kati ya
Halmashauri 185 zilizokaguliwa kwa hesabu zilizoishia 30 Juni 2019, Halmashauri
176 zilipata Hati Inayoridhisha na Halmashauri 9 zilipata Hati yenye Shaka
ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi huku hoja zilizoibuliwa kwa kipindi cha
mwaka wa fedha 2018/2019 ni hoja 32 na hoja za nyuma zilizokuwa bado hazijafungwa
ni 52.
CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )