WATUMISHI WA UMMA WANAOINGIZA KWA MAKUSUDI MIFUGO KWENYE HIFADHI NA KUNYANYASA WAFUGAJI WAONYWA

 

 


Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na baadhi ya
wafugaji katika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kituo cha
Wilaya ya Siha, wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili
Mkoani Kilimanjaro na kuwataka wafugaji wafuge kisasa na kuwahakikishia
kuwa wizara itaendelea kusimamia maslahi ya wafugaji nchini.Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akisalimiana na baadhi ya
wafugaji wa jamii ya kimaasai mara baada ya kuzungumza nao alipotembelea
Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kituo cha Wilaya ya Siha,
wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani
Kilimanjarao.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa
na uongozi wa Wilaya ya Siha, na baadhi ya kinamama wa jamii ya kimaasai
mara baada ya kuzungumza na baadhi ya wafugaji wa jamii hiyo,
alipotembelea Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) kituo cha
Wilaya ya Siha, wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili
Mkoani Kilimanjarao.Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akifafanua jambo kwa Meneja wa
Ranchi ya West Kilimanjaro Bw. Raymond Lutege (wa kwanza kulia) mara
baada ya Waziri Ndaki kufika katika ranchi hiyo siku ya kwanza ya ziara
yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani Kilimanjaro na kutaka ranchi zote za
taifa kutumia teknolojia ya kisasa katika kudhibiti wizi wa mifugo
katika ranchi hizo.Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (katikati) akipatiwa maelezo ya
mbegu bora za mbuzi na Kaimu Mkurugenzi wa Kanda ya Kaskazini wa Taasisi
ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Dkt. Athuman Nguluma, mara baada
ya Waziri Ndaki kutembelea kituo cha taasisi hiyo kilichopo Wilaya ya
Siha Mkoani Kilimanjaro wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi ya siku
mbili mkoani humo na kuitaka TALIRI ihakikishe matokeo ya tafiti zake
yanakuwa na tija kwa wafugaji.Muonekano
wa duka la kuuzia nyama linalomilikiwa na Ranchi ya West Kilimanjaro
iliyo chini ya Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO), ambalo Waziri wa
Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameitaka kamati ya ulinzi na usalama
ya Wilaya ya Siha kufanya uchunguzi wa utendaji kazi wa duka hilo baada
ya kutoridhishwa na namna linavyoendeshwa tangu kuanzishwa kwake. (Picha na Edward Kondela – Afisa Habari, Wizara ya Mifugo na Uvuvi)Na. Edward Kondela


Waziri
wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema atazungumza na Waziri wa
Maliasili na Utalii kuhusu kitendo cha baadhi ya watumishi wa umma
walio chini ya wizara hiyo ambao wamekuwa wakiielekeza mifugo kwa
makusudi kuingia kwenye hifadhi za taifa ili waikamate na kuwaonea
wafugaji kwa kuwalipisha tozo pamoja na kutaifisha mifugo hiyo.


Waziri
Ndaki amezungumza hayo jana (09.02.2021) wakati akihitimisha ziara yake
ya siku mbili Mkoani Kilimanjaro, kwa kuzungumza na baadhi ya wafugaji
katika Wilaya ya Siha mkoani humo mara baada ya kutembelea Taasisi ya
Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) na Ranchi ya West Kilimanjaro
zilizopo katika wilaya hiyo ili kujionea namna wanavyotekeleza majukumu
yao.


Amesema
kitendo hicho cha kifisadi hakiwezi kuvumilika na kwamba watuhumiwa
wote watatafutwa na kukamatwa ili hatua kali za kisheria ziweze
kuchukuliwa ikiwemo kufukuzwa kazi.


“Ninajua
kuna wakati tunaonewa unakuta ng’ombe wako pembeni ya hifadhi
wanapelekwa kwa lazima ndani ya hifadhi, nimesema nazungumza na
mwenzangu wa maliasili na utalii na kumwambia huo mtindo hapana,
tuwasake watu wako kwa sababu wenye tabia hiyo siyo wafugaji ni watu wa
Wizara ya Maliasili na Utalii, hao tunaanza kuwasaka mmoja mmoja maeneo
yote wanayokaa karibu na wafugaji tutawabaini na wanachokifanya ni
kitendo cha kiharamu na ufisadi kwa sababu una bunduki unamtisha mfugaji
halafu unawapeleka kwa lazima ng’ombe kwenye hifadhi hiyo na kusema
umewakamata ng’ombe kwenye hifadhi hatutaelewana.”
Amesema Mhe. Ndaki


Ameongeza
kuwa kitendo hicho lazima kikemewe kwa kuwa kinarudisha nyuma uwekezaji
katika Sekta ya Mifugo na kutaka watumishi wa umma pamoja na wafugaji
kufuata sheria, taratibu na kanuni za nchi na kwamba lazima kukomesha
hatua hiyo kwa sababu inasababisha migogoro kati ya wafugaji na hifadhi
za taifa na kwamba kuna wakati wafugaji wanaelewa maeneo ya hifadhi,
lakini wakipeleka mifugo karibu na maeneo hayo wananyanyaswa na mifugo
yao kulazimishwa kuingia ndani ya hifadhi ili ionekane wameingiza mifugo
ndani ya hifadhi.


Katika
hatua nyingine, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameitaka
Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kufikia Jumatano ijayo, iwe imeandaa
taarifa ya mifugo iliyopo kwenye ranchi zote hapa nchini, zikiwemo za
kiwango cha mifugo inayozaliwa, kufa na aina ya mifugo iliyopo ili kuona
kinachoendelea katika ranchi hizo.


Amemuagiza
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof.
Elisante Ole Gabriel, kuhakikisha anasimamia zoezi hilo ili taarifa hizo
aweze kuzipata siku hiyo ya Jumatano, ikiwa ni lengo la kuhakikisha
mifugo ya serikali inakuwa na tija kwa taifa.


“Tunataka rasilimali ya mifugo inufaishe taifa na wananchi hawa hatuwezi kuwa na rasilimali ambayo hatujui iko kiasi gani.” Amefafanua Mhe, Ndaki.


Pia
ameitaka NARCO kuhakikisha inatumia teknolojia ya kisasa ya kuwawekea
mifugo iliyopo kwenye ranchi zake ili kudhibiti vitendo vya wizi wa
mifugo ambavyo vimekuwa vikijitokeza katika ranchi zake na kuisababishia
hasara za mara kwa mara.


Kuhusu
uwekezaji wa NARCO katika duka la kuuzia nyama lililopo Kata ya Sanya
Juu Wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Mashimba Ndaki ameitaka kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo
kufanya uchunguzi juu ya utendaji wa duka hilo baada ya kutoridhishwa na
taarifa zilizorekodiwa tangu kuanza kwake kazi ya uuzaji nyama.


Waziri
Ndaki ameongeza kuwa kumekuwa na taarifa za mauzo kidogo ya nyama
ambayo hayalingani na uhitaji wa nyama eneo husika, huku akitaka mmoja
wa mawakala ambaye aliwahi kuwa na utaratibu wa kununua nyama katika
Ranchi ya West Kilimanjaro kwa bei ya jumla na kwenda kuuza kwenye duka
lake kuchunguzwa na kuitaka kamati hiyo kuwachukulia hatua za kisheria
wale wote watakaobainika kuhujumu utendaji kazi wa duka.


Kwa
upande wao baadhi ya wafugaji waliohudhuria mkutano huo wamelalamikia
uvamizi wa wanyamapori ambao wamekuwa wakiingia katika maeneo yao na
kuharibu mazao na malisho ya mifugo hali ambayo imekuwa ikiwarudisha
nyuma katika utendaji wao wa kazi.


Wameongeza
kuwa kitendo hicho kimeathiri kwa kiasi kikubwa malisho ya mifugo na
kuiomba serikali kuangalia hatua ambazo inaweza kuchukua ili kudhibiti
kitendo hicho ambacho kimekuwa kikiwarudisha nyuma mara kwa mara pamoja
na kufanya mikakati mbalimbali ya kuhakikisha dawa na chanjo za mifugo
zinawafikia ili kudhibiti magonjwa ya mifugo ambayo yamekuwa yakiathiri
kwa kiasi kikubwa mifugo yao.


Awali
kabla ya kikao hicho na baadhi ya Wafugaji wa Wilaya ya Siha, Waziri wa
Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa katika Ranchi ya West
Kilimanjaro inayosimamiwa na Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kujionea
utendaji kazi wa ranchi hiyo pamoja na kupokea taarifa ya namna ranchi
hiyo inafanya kazi kutoka kwa meneja wa ranchi hiyo Bw. Raymond Lutege
ambaye amemuambia Waziri Ndaki kuwa ranchi hiyo iko katika hatua
mbalimbali za kuhakikisha mbegu bora za mifugo wakiwemo ng’ombe na
kondoo zinapatikana ili wafugaji waweze kufuga kisasa kwa kuwa na mifugo
bora.


Waziri
Ndaki akiwa katika Taasisi ya Utafiti wa Mifugo nchini (TALIRI) Kituo
cha Wilaya ya Siha, mara baada ya kusomewa taarifa ya kituo na Kaimu
Mkurugenzi wa Kanda ya Kaskazini Dkt. Athuman Nguluma, waziri huyo
ameitaka TALIRI kuhakikisha tafiti inazofanya ziwe na tija kwa wafugaji
na taifa kwa ujumla ili tasnia ya ufugaji iweze kubadilika na kuwa ya
kisasa zaidi.


Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Siha Mhe. Onesmo Buswelu amesema anaimani
kubwa na utendaji kazi wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki
kwa namna alivyoanza kusimamia sekta za mifugo na uvuvi na kuonesha nia
thabiti ya kutatua changamoto zilizopo katika sekta hizo.


Ameongeza
kuwa serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekuwa ikifanya
jitihada kuhakikisha wafugaji wananufaika kwa kiasi kikubwa pamoja na
kuondoa migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )