WANANCHI MBARALI WATAKIWA KUPANDA MITI

Na Esther Macha, Mbarali

WANANCHI wilayani Mbarali  wametakiwa kupanda miti kwa wingi katika katika maeneo ya wazi pamoja na makazi yao kwani kufanya hivyo kutaifanya wilaya kuondokana na hali ya ujangwa na kuifanya Mbarali kuwa  ya kijani.

Rai hiyo imetolewa na  Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbarali ,Michael Semindu wakati wa zoezi la upandaji miti 200 ya aina mbalimbali  katika Kituo cha Afya cha Kapunga kilichopo Kijiji cha kapunga kata ya Itamboleo wakati wa maadhimisho ya kilele cha upandaji miti kiwilaya.

Semindu alisema kwamba miti hiyo imepandwa kuzunguka eneo la hospitali  kwa lengo la kuboresha mazingira yanayozunguka kituo cha cha afya  pamoja na kuthibiti ukame.

Aidha Katibu Tawala huyo licha ya miti hiyo kupandwa lakini bado wananchi nao wanatakiwa kujenga tabia ya kupanda miti ambayo inasaidia  kuondokana na hali ya ujangwa hasa ukizingatia mara nyingi kumekuwa na tatizo la kuwepo kwa mafuriko mara kwa mara .

“Zoezi la upandaji miti hii liwe endelevu kwa wananchi na viongozi wa vijiji wahakikishe wanasimamia hili kwa kushirikiana na wananchi ,miti ni muhimu sana ndugu zangu tulitambue hilo”alisema Semindu.

“Taasisi zote  za Serikali na zisizo za Serikali zilizopo Wilaya ya Mbarali hakikisheni mnapanda miti katika ofisi zenu, najua wote tunafahamu faida ya kuotesha miti katika  mazingira yetu vilevile naendelea kusisitiza tuendelee kuchukua tahadhari ya ugonjwa wa Corona kwa kufuata maelekezo yote yanayotolewa na Viongozi Wakuu wa Nchi pamoja na Wizara ya Afya”. Alisema.

Kwa upande wake  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali , Kivuma Msangi, aliwataka  wananchi wote Wilaya humo  kuendelea kupanda miti kwa wingi kwenye makazi yao ili iweze kuwatunza kwani siku zote Miti ina faida nyingi ikiwemo  kutunza vyanzo vya maji, kudhibiti hali ya hewa, kivuli, matunda na faida zingine.

Hata hivyo  katika  zoezi hilo  kulitolewa elimu kwa wananchi  dhidi ya tahadhari na hatari ya ugonjwa wa Corona (COVID 19) ilitolewa kwa viongozi na wananchi waliohudhuria na kuwaomba kuwa mabalozi wa kutoa elimu hiyo katika maeneo yao ili waweze kujikinga na kuwakinga wengine.

Mkurugenzi huyo alisema ugonjwa huo ni hatari hivyo ni lazima wananchi na viongozi waendelee kuchukua tahadhari ya ugongwa wa Corona bila kuathili shughuli zingine, zoezi hilo lilihudhuriwa na watu wachache wakiwemo, wajumbe wa Kamati ya Usalama Wilaya, wataalamu kutoka ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuri ya wilaya ya Mbarali, Wazee Maarufu, Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya kata pamoja na baadhi ya viongozi wa kata na vijiji

Mwisho.

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )