WANANCHI DAR WAITIKIA AGIZO LA MAKONDA…BARAKOA KILA MAHALI

Na Said Mwishehe, 

WAKAZI wa Jiji la Dar es  Salaam wameitikia mwito wa Mkuu wa Mkoa huo Paul Makonda wa kuvaa barakoa kama hatua mojawapo ya kukabiliana na virusi vya Corona.

Juzi Makonda alitangaza kwamba kuanzia Jumatatu (leo) wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam watatakiwa kuvaa barakoa na kwamba kwa wale ambao watakaidi hatua za kisheria zitachukuliwa.Hata hivyo asilimia kubwa ya wananchi wameitikia mwito huo kwani kila kona ya Jiji hilo wamevaa barakoa.

Michuzi TV na Michuzi Blog leo imeshuhudia mamia ya wananchi kuanzia mtaani, , kwenye vituo vya daladala, kwenye mikusanyiko ya watu pamoja na maofisini wakiwa wamevaa barakoa.

Baadhi ya wananchi ambao wamezungumzia uamuzi wa kuvaa barakoa wamesema wanaipongeza Serikali kwa hatua ambazo inachukukua kukabiliana na ugonjwa huo kwani badala ya kutoa maagizo ya kuwafungia ndani imeamua kutumia busara za kuruhusu watu kuendelea na shughuli zao lakini waki
wa wamechukua tahadhari za kujikinga na Corona.

Juma Shaban Mlosa ambaye ni Mkazi wa Kipawa jijini Dar es Salaam amesema amefurahishwa na maelekezo ambayo yametolewa na Makonda kwani unanesha namna ambavyo Mkoa umedhamiria kuwalinda watu wake.

Wakati uvaaji wa barakoa ukiwa umeshamili, mafundi nguo katika Jiji la Dar es Salaam wamejikuta wakipata neema ya fedha kutokana na kuitengeneza barakoa za vitambaa ambapo barakoa moja inauzwa kati ya Sh.1000, 1500 na Sh.2000.

Baadhi ya mafundi juzi na jana wamejikuta kutwa nzima wakitengeneza barakoa kwa ajili ya kuuza.Utengenezaji wa barakoa ulisababisha baadhi ya mafundi kuweka kando utengenezaji wa nguo za wateja na hivyo kutumia muda mwingi kwenye barakoa.

Mmoja wa mafundi aliyejitambulisha kwa jina la Rajab alisema kuwa yeye anatengeneza barakoa ambazo kuna watu wameomba kutengenezewa na kila barakoa anauza sh.1000.Hata hivyo amesema anatengeneza lakini anahofu kubwa kutokana na ugonjwa wenyewe kuwa tishio.” Nachukua hela za watu wanaohitaji barakoa lakini ukweli sizifurahii maana watu wanachukua kwa ajili ya kuokoa maisha na so kwasababu ya fasheni.”

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )