Wakili: Mtuhumiwa Mauaji ya George Floyd Hana Hatia.

WAKILI Early Gray anayemtetea  Thomas Lane, mmoja wa maofisa wanne wa polisi wanaohusika katika kifo cha Mmarekani mweusi, George Floyd, amesema mteja wake huyo alifanya kila kitu alichofikiri kilikuwa sahihi wakati wa kumkamata Floyd.


“Hakuishia hapo tu.  Wakati wa kumpeleka mtuhumiwa (Floyd) yeye ndiye aliyekuwa amemwekea (Floyd) mashine ya kurudisha mapigo ya moyo wakiwa katika gari la wagonjwa.  Ni mtu mwenye upendo, si mkorofi,” alisema Gray.

Lane alikuwa ni mmoja wa polisi wawili walioonekana kwenye video wakimsaidia aliyekuwa polisi mwenzao, Derek Chauvin, aliyekuwa amemgandamiza Floyd chini kwa kumwekea goti shigoni kwa karibu dakika tisa.  Polisi wa nne alikuwa amesimama pembeni wakati hilo likifanyika.

Lane na polisi wengine wawili waliosaidia katika kumkamata Floyd, ambao ni J. Alexander Kueng na  Tou Thao, walifunguliwa mashtaka ya kushiriki katika mauaji hayo.

Meya wa Jiji la Mineapolis, Jacob Frey, amesema, “njia waliyotumia polisi hairuhusiwi; si njia ambayo  maofisa wetu wa polisi wamefundishwa.”

Moja ya video zilizochukuliwa na wapita njia na mashahidi waliokuwepo wanasema Floyd aliyekuwa kando ya barabara, hakufanya vurugu yoyote ya kukataa kukamatwa na polisi.

Kuuawa kwa Mmarekani huyo mweusi wiki karibu mbili zilizopita, kumezua tafrani kubwa nchini Marekani na sehemu mbalimbali duniani kupinga njia hiyo ya kikatili iliyotumika kumkamata na kusababisha kifo chake.

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )