WADAIWA KUKAIDI AGIZO LA SERIKALI KUTOZURURA OVYO WAKATI WA LIKIZO

Soko la Vitunguu la Kimataifa –Misuna mjini Singida, eneo linalodaiwa wanafunzi kwenda kujipatia ajira za kuchambua vitunguu wakati huu wa likizo yao ya dharura 
 Meya wa Manispaa ya Singida, Gwae Chima Mbua akihutubia Baraza la Madiwani wa Manispaa hiyo katika Ukumbi wa Mwenge Sekondari mjini Singida
Mmoja wa Madiwani wa Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Singida akichangia hoja wakati wa Kikao cha Baraza hilo hivi karibuni
………..
Wadaiwa kukaidi Agizo la Serikali kutozurura ovyo wakati wa  likizo
Singida, Jumatatu Aprili 13, 2020
Na Abby Nkungu, Singida.
IMEBAINIKA kuwa likizo ya dharura ya siku 30 iliyotolewa na Serikali kwa shule za Awali, Msingi, Sekondari na Vyuo vya elimu ya Juu kutokana na mlipuko wa COVID 19 nchini, inatumiwa vibaya na baadhi ya wanafunzi; hivyo kujiweka katika hatari zaidi ya kuambukizwa virusi vya gonjwa hilo.
Uchunguzi uliofanywa na Mwandishi wa habari hizi umebaini kuwa badala ya kukaa nyumbani kama ilivyoelekezwa na Serikali, baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakizurura ovyo mitaani huku wengine wakifanya shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato, zikiwemo biashara ndogondogo  kwenye misongamano ya watu mitaani.
Baadhi ya wanafunzi hao waliohojiwa walidai kuwa wameona sio vyema kukaa bure nyumbani badala yake wameamua kujitafutia japo fedha kidogo za matumizi yao hapo shule zitakapofunguliwa.
Hata hivyo, Wataalamu wa Afya wanaonya kuwa hatua hiyo ni hatari kwa kuwa baadhi ya wanafunzi wanaozurura ovyo mitaani ni wenye umri chini ya miaka minane (8) ambao hawajitambui; hivyo sio rahisi kwa wao kuzingatia Kanuni za kujikinga dhidi ya maradhi hayo ikiwa ni pamoja na kunawa mikono yao mara kwa mara.
Akifunga Kikao cha Kawaida cha Baraza la Madiwani la Manispaa ya Singida, Meya wa Manispaa hiyo, Gwae Chima Mbua alilaani tabia ya baadhi ya wazazi na walezi kuwaacha watoto wao wakizurura ovyo mitaani huku wengine wakiichukulia likizo hiyo kuwa ni fursa kwao kujipatia kipato kwa kuwatumikisha wanafunzi kwenye biashara mbalimbali.
Meya huyo alitaja baadhi ya maeneo yaliyokithiri kwa watoto kufanya shughuli za kujiingizia kipato kuwa ni pamoja na uvuvi Ziwa Kindai na Singidani, kuchambua vitunguu Soko la Kimataifa Misuna mjini hapa na kuuza karanga na mayai mitaani.
Alisema kuwa hali hiyo haikubaliki  katika  kipindi  hiki na kuzitaka Mamlaka husika; hususan watumishi wa Idara ya Kazi, kuacha kukaa ofisini badala yake waende maeneo ya Maziwa, Migodi, Minadani na kwenye Masoko mbalimbali kukagua aina ya watoto wanaofanyishwa kazi maeneo hayo na kuchukua hatua  stahiki.
Aidha, alitoa mwito kwa wazazi na walezi kutambua kuwa nia ya Serikali kufunga shule na Vyuo ni kuwanusuru wanafunzi kutoka kwenye maambukizi ya virusi vya gonjwa hilo; hivyo haikubaliki watoto wadogo kiasi hicho kufanya majukumu ya kuwatafutia wazazi wao riziki ya kila siku badala ya kutulia nyumbani wakijisomea.
Wakichangia hotuba hiyo, baadhi ya madiwani walidai kuwa kwa kufanya hivyo wazazi au walezi wa watoto hao wanakwepa wajibu wao wa msingi kuwalinda na kuwatunza watoto huku wengine wakiitaka Serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria wazazi wa aina hiyo.
Taarifa ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaonesha kuwa  hadi Aprili 12 mwaka huu jumla ya watu 32  walikuwa wamethibitika kuambukizwa virusi vya Corona hapa nchini, watano kati yao wakipona maradhi hayo huku watatu wakiripotiwa kupoteza maisha.
MWISHO

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )