VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA WATAKIWA KUWACHUJA WAGOMBEA, MAGUFULI AMWAGIWA SIFA

 Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uimarishaji wa Maadili na Usaidizi Katika Utumishi wa Umma na wa Binafsi (WoLaOTa) Samwel Olesaitabau akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya uzinduzi wa taasisi hiyo iliyofanyika mkoani hapa jana.
Waandishi wa habari wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa taasisi hiyo. Na Dotto Mwaibale, Singida

VIONGOZI wa vyama vya kisiasa wametakiwa kuhakikisha wote wanaoomba nafasi ya uongozi wanachujwa ipasavyo ili kusaidia kupunguza viongozi wala rushwa nchini.

Ombi hilo limetolewa na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uimarishaji wa Maadili na Usaidizi Katika Utumishi wa Umma na wa Binafsi (WoLaOTa) Samwel Olesaitabau wakati wa hafla ya uzinduzi wa taasisi hiyo iliyofanyika mkoani hapa jana.

Katika hatua nyingine Olesaitabau amewaomba viongozi wa dini kote nchini kutenga muda katika ibada zao hata kwa dakika tano kuiombea Nchi na Uchaguzi Mkuu wa 2020 hata kwa wale wasio na dini rasmi wanaoabudu mawe au milima nao wafanye hivyo.

“Mwaka huu kuna uchaguzi na niwaombe sana viongozi wote wa vyama vya kisiasa kikiwemo chama Tawala cha CCM kuhakikisha wote wanaoomba uongozi wamechujwa ipasavyo na wasiwe na huruma na wakifanya hivyo basi kwa vyovyote vile tutapunguza viongozi wala rushwa Serikalini” alisema Olesaitabau.

Akizungumzia kusudi la kuanzisha taasisi hiyo alisema ni kusaidia uongozi wa nchi yetu kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli kama aalivyoonesha Rais John Magufuli. 

Aidha Olesaitabau alisema dira ya taasisi hiyo ya kipekee hapa nchini ni utoaji wa elimu ya kuimarisha maadili kwa waajiri, na watumishi wa sekta za umma na binafsi Tanzania Bara ili watumie Ueledi na Taaluma zao kwa kuleta matokeo chanya.

Olesaitabau akizungumzia baadhi ya sifa kati ya 35 alizoziona za utendaji kazi wa Rais Dkt. John Magufuli alisema ni kiongozi ambaye ana uwezo wa kuamua jambo na kulisimamia kuanzia mwanzo hadi mwisho na kuwa hayumbishwi na kelele  ama za ndani ya nchi au hata nje kwa jambo ambalo amelianzisha kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

Alitaja sifa nyingine kuwa anaichukia rushwa na anapenda kila mtu afanye kazi ya kujipatia kipato kwa jasho lake mwenyewe bila ya kumdhulumu mwingine na kuwa ana uwezo wa kuweka kumbukumbu/ takwimu kiusahihi katika kichwa chake kwa muda mrefu bila ya kusahau.
CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )