VIJANA WAHAMASISHWA UFUGAJI WA KUKU, KUJIKWAMUA KIUCHUMI


Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo na Usalama wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi akimkabidhi Bi. Leah Tesha vifaa kwa jili ya  Salma Chihota vifaranga vya kuku.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo na Usalama wa Chakula na Lishe kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi akimkabidhi Bi. Salma Chihota vifaranga vya kuku.

Picha ya baadhi ya vifaranga vilivyokabidhiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi  kwa Bi. Leah Tesha mmoja wa vijana katika kikundi cha wajasiriamali wa kuku ili kuhamasisha vijana kujikita katika ufugaji huo
Na. Edward Kondela

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imewapa vifaranga vya kuku 540 kikundi cha vijana wajasiriamali ili kuhamasisha ufugaji utakaosaidia kuziba pengo la uhaba wa nyama ifikapo mwaka 2022 pamoja na kukuza sekta ya kuku nchini.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo na Usalama wa Chakula na Lishe wa wizara hiyo, Bw. Gabriel Bura amekabidhi vifaranga hivyo mwishoni mwa wiki kwa wawakilishi wa kikundi cha vijana watatu wajasiriamali hafla ilifanyika Mbweni jijini Dar es Salaam.

Bw. Bura amesema hatua hiyo inatokana na mkutano uliofanyika kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel na wadau wa tasnia ya kuku kilichoketi Machi 7 mwaka huu katika ofisi ndogo za wizara hiyo zilizopo jijini Dar es Salaaam

Kwa mujibu wa Bw. Bura, Prof. Gabriel alimsikiliza mdau mmoja mmoja, lakini alishawishika zaidi na uwepo wa vijana  wenye umri wa chini ya miaka 35 walioonyesha nia ya dhati ya kuwekeza katika tasnia ya ufugaji wa kuku.

Mbali na hilo, Bw. Bura amesema hatua hiyo pia ni  sehemu ya kutekeleza mpango mkakati wa wizara hiyo ya kuhamasisha ufugaji wa kuku kwa vikundi vya vijana na kina mama.

Aidha amesema vijana hao wameonyesha uthubutu na wameonekana kupenda tasnia hiyo ili kukabiliana na hali halisi ya soko la ajira akisema baadhi yao wamesomea fani ya sheria na habari na mawasiliano.

Amefafanua kuwa mpango wa kuwahamasisha ufugaji wa kuku katibu mkuu aliamua kuanza na vijana watatu ambao watakuwa chachu kwa wenzao kujifunza.

Amesema serikali imeamua kuwapatia vifaranga vya kuku 540, pamoja na vyakula vya mwezi mmoja, chanjo, vilishio na vinywesheo ambapo msaada huo umegharimu Shilingi milioni 6.1

Kwa mujibu wa Bw. Bura, mpango kabambe wa miaka 15 wa  kuendeleza sekta ya mifugo umeonyesha kuwa kutakuwa na upungufu wa nyama  unaokaridiwa tani ya zaidi ya 100,000 ifikapo mwaka 2022 kadri kipato cha wananchi  kinavyoongezeka.

“Tumeona huu upungufu wa nyama tunaweza kuufidia katika ufugaji wa kuu ambapo ndani ya miezi 2 au 3 nyama inapatikana, ndiyo maana serikali imeamua kuongeza nguvu na kuchukua hatua za uhamasishaji zaidi  kwa vikundi vya vijana.

Ameongeza kuwa hatua nzuri ya kuigwa kwa vijana hao kujihusisha na ufugaji ili kuondokana ile dhana ya kuwa mchakato huo unafanywa na wazee na watu waliostaafu.

Amesema wameanzia Mkoa wa Dar es Salaam, kisha watakwenda wilayani Mkuranga , mikoa ya Mbeya , Morogoro na Dodoma akisema ni mchakato endelevu wa kutoa vifaranga kwa vikundi vya vijana wajasiriamali.

Sarah Urio  ambaye ni msambazaji wa viranga hivyo kutoka kampuni ya AKM Glitters, amewashukuru vijana kwa kuonyesha utayari na uthubutu wa kufuga kuku, akisema licha ya kupewa vifaranga hivyo lakini uongozi wa kampuni hiyo utakuwa bega kwa bega  kwa kuwapa elimu ya namna ya kuendeleza mchakato huo.

“Tukishawapa vifaranga na mahitaji husika hatutawaacha  bali tutaendelea kutoa ushirikiano katika mchakato huu. Tutawasimamia mwanzo hadi mwisho ili wafuge kwa ufanisi,” alisema

Bi. Leah Tesha ambaye anaunda kikundi hicho  ameishukur serikali kwa kuwapatia vifaranga hivyo akisema wametimiza ahadi yao na kwamba kuku hao itakuwa kama ajira kwao kwa sababu suala hilo limekuwa changamoto hivi sasa.

Amesema wameamua kuthubutu kwa kuandaa mpango mkakati  waliouwasilisha katika ofisi ya katibu mkuu wa wizara namna walivyojipanga katika mchakato wa ufugaji wa kuku.

“Sisi tumeonyesha njia ni fursa kwa vijana wengine wanaotembea na bahasha mkononi wajitokeza kufuga kuku. Sisi ni mfano vijana wenzetu wanaweza kuiga na kuachana na ile dhana wote lazima tupate kazi.
CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )