UHABA WA WATAALAMU WENYE UJUZI KILIO KWA WAWEKEZAJI

Mkuu wa Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester, Dkt. Umapati Dasgupta (kulia) akimueleza jambo Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) alipotembelea kukagua kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani jana.


 1. Mtaalam wa Kuendesha Mitambo katika Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester, Geofrey Mahende (kulia) akitoa maelezo ya namna anavyofanyakazi yake kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto)alipotembelea kukagua kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani jana.
 2. Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wataalam wa Kitanzania wanaofanyakazi katika Kiwanda cha kutengeneza Chanjo cha Hester alipotembelea kiwanda hicho kilichopo Mkoani Pwani jana. Wa kwanza kushoto ni Mratibu na Mkurugenzi wa Operesheni, Tina Towo Sokoine.

  1. Katibu
   Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel
   (kulia) akibadilishana mawazo na Mkuu wa Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo
   cha Hester, Dkt. Umapati Dasgupta (kushoto) muda mfupi baada ya kumaliza
   kutembelea kiwanda hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani jana.

    


   Na Mbaraka Kambona, Pwani

    

   Mratibu na Mkurugenzi wa
   Operesheni, Kiwanda cha Kutengeneza Chanjo cha Hester, Tina Towo Sokoine
   amesema kuwa lengo la kiwanda hicho ni kutumia Wataalamu wa ndani lakini uhaba
   wa Wataalam wa masuala ya sayansi wenye ujuzi hasa wa vitendo unaelekea   kukwamisha dhamira yao hiyo.
    

   Towo aliyasema hayo alipokuwa
   akitoa taarifa ya utekelezaji wa kiwanda hicho kwa Katibu Mkuu, Wizara ya
   Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel alipotembelea kiwanda
   hicho kilichopo Wilayani Kibaha, Mkoani Pwani jana.
    

   Alisema kuwa kwa sasa wana
   wataalamu watatu tu kutoka nje nchi ambao wamewaajiri katika Kiwanda hicho
   lakini   kwa hali ilivyo wanaona watashindwa na labda
   wanaweza kuomba vibali vingine vya kuajiri wataalamu kutoka nje.
    

   “Nia yetu ni kufanyakazi na
   Watanzania tu lakini bado vijana wengi tunaowafanyia usahili wanakosa ujuzi hasa
   wa vitendo, tunaiomba Serikali na Vyuo vinavyoandaa hawa Wataalam kuhakikisha wanajikita
   katika elimu ya vitendo na sio nadharia peke yake ili kukidhi mahitaji ya sasa
   na kulinda ajira za Watanzania,” alisema Towo
    

   Kuhusu uzalishaji, Towo alisema
   kuwa wanatarajia kuzalisha chanjo ya kwanza mwezi wa nne mwaka huu, huku
   akiiomba Serikali kuona uwezekano wa taasisi zinazohusika na kusimamia
   uwekezaji kuunganishwa ziwe na lugha ya pamoja ili kumfanya muwekezaji aweze
   kupata huduma zote sehemu moja bila kuhangaika kama ilivyosasa.
    

   Naye Katibu Mkuu, Wizara ya
   Mifugo na Uvuvi (mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel aliutaka Uongozi wa
   Kiwanda hicho  kuhakikisha wanazalisha
   chanjo zenye ubora ili nchi iweze kuondokana na utegemezi wa chanjo na bidhaa
   nyingine za mifugo kutoka nchi za nje.
    

   “Lengo la Wizara ni
   kuhakikisha kuwa nchi inaondokana na uagizaji wa chanjo kutoka nje, tunatamani
   kuwa na chanjo tunazoweza kudhibiti ubora wake na tuwe na uhakika nayo, hivyo
   uwepo wa kiwanda hiki kutatusaidia kuzalisha chanjo hapa hapa nchini ili
   kukidhi mahitaji ya Wafugaji wetu na Watanzania kwa ujumla,” alisema Prof. Ole
   Gabriel.
    

   Aliongeza kwa kusema kuwa
   Serikali inaweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili mahitaji ya wafugaji na
   wananchi yawe yanashughulikiwa ndani ya  nchi.
    

   Aidha, Prof. Ole Gabriel
   aliwaomba Wafugaji na Watanzania kuanza kujenga utamaduni wa kuthamini bidhaa
   za ndani na waondokane na ile dhana ya kwamba bidhaa bora ni ile inayotoka nje,
   wakithamini vya ndani wataongeza pato la Taifa na kukuza uchumi wa nchi.

   CATEGORIES
   Share This

   COMMENTS

   Wordpress (0)
   Disqus (0 )