TCCIA Manyara watoa ushauri TRA kufuatia Malalamiko ya wafanyabiashara.

Na John
Walter-Manyara
Baadhi ya
wafanyabiashara mjini Babati mkoa wa Manyara wakitoa maoni yao juu ya utendaji
wa mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) mkoani hapo,wameonyesha kutoridhishwa na
namna wanavyohudumiwa.
Wakizungumza na kituo hiki bila kutaja majin yao, wamesema kuwa
baadhi ya watumishi katika mamlaka hiyo wamekuwa na tabia ya kukadiria mapato
makubwa kwa wafanyabiashara ili  kutengeneza meza ya mazungumzo, hatua  inayopelekea kutengeneza mazingira ya Rushwa.
Wameipongeza
TAKUKURU mkoa wa Manyara kwa kuanza kufuatilia utendaji wa Mamlaka ya Mapato (TRA)
huku wakiomba viongozi wa ngazi mbalimbali za serikali, kuwa na utaratibu wa kusikiliza
kero zinazowakabili wafanyabiashara.
Katibu wa chama cha
wafanyabiashara,wakulima na wenye viwanda (TCCIA) Mkoa wa Manyara Mwanahamisi
Hussein amesema ni muda mrefu wafanyabiashara wamekuwa wakiilalamikia mamlaka
hiyo.
Katibu huyo ameiomba mamlaka hiyo kuwa na tabia
ya  kuwatembea wafanyabiashara mara kwa
mara na kufuatilia mienendo ya watendaji wao wanaowatuma akieleza kuwa hatua
hiyo itasaidia kupunguza kero za muda mrefu za kodi ambazo zimekuwa kikwazo
katika ukuaji wa shughuli za biashara nchini.
Katika hatua nyingine Mwanahamisi ameeleza kuwa
wameandaa utaratibu maalum wa kusikiliza kero mbalimbali za wafanyabiashara
mkoani hapo  na kuwapatia ushauri,ambapo
huwashirikisha pia Mamlaka ya Mapato Manyara.
Kwa madai ya kusumbuliwa na Mamlaka hiyo
taarifa zinaeleza kuwa imepelekea wengine kupata shinikizo la damu huku baadhi
wakifunga biashara zao.
Mkuu  wa Taasisi ya
kuzuia na kupambana na Rushwa mkoa wa Manyara (TAKUKURU) Holle Mkungu, mwezi
Mei,2020 waliwafikisha katika Mahakama ya hakimu mkazi Manyara  maafisa wawili wa TRA kwa makosa ya kudai na
kupokea Rushwa ya shilingi Milioni kumi.
Aliwataja watuhumiwa hao
kuwa ni Subilaga Mwangama na Ojungu Mollel,  na kwamba 
walifanya  makosa hayo  kinyume cha kifungu cha 15 cha sheria ya
kuzuia na kupambana na Rushwa namba 11/2007.
Waziri wa Fedha na
Mipango, Dk Philip Mpango akizungumza bungeni 
Juni 13, 2019  wakati akiwasilisha
bajeti ya Serikali Kuu kwa mwaka 2019/2020, alisema ili kupunguza malalamiko ya
wafanyabiashara, Serikali imeamua kuanzisha 
kitengo huru cha kupokea malalamiko ya taarifa za kodi dhidi ya Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) na  kusimamiwa
na kuratibiwa na wizara yake ili kuhakikisha kinakuwa na ufanisi wa
kushughulikia kero za wafanyabiashara.
Alisema  majukumu ya kitengo hicho ni kupokea
malalamiko ya rushwa dhidi ya watumishi wa TRA ambao wamekuwa wakijipatia fedha
kinyume na sheria na kuwakandamiza wafanyabiashara. 

Aidha,
kitengo hicho kinahusika kupokea malalamiko ya ukadiriaji wa kodi na uthaminishaji
wa bidhaa husika pasipo kufuata taratibu zilizowekwa na malalamiko ya matumizi
ya nguvu katika ukusanyaji wa kodi dhidi ya TRA.
CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )