TAKUKURU Manyara yawaburuza Mahakamani watumishi wa TRA Manyara kwa Rushwa

Na John Walter-Manyara
Taasisi ya Kuzuia na  Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Manyara imewafikisha watu wawili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Manyara kwa tuhuma ya kuomba na kupokea rushwa ya shilingi Milioni  kumi (10,000,000) kinyume cha sheria ya kuzuia rushwa namba 11/2007.
Akisoma Shitaka hilo mbele ya Hakimu mkazi Mfawidhi Wilaya ya Babati  V.J. Kimario, Mwanasheria wa TAKUKURU Bw. Izdory Kyando aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Bi. Subilaga Mwangama na Bw. Ojungu Mollel wote wakiwa watumishi wa Mamlaka ya Mapato (TRA).
Bwana Kyando aliiambia Mahakama kuwa mlalamikaji ni mfanyabiashara wa Wilayani Mbulu na ni mlipa kodi katika mamlaka ya mapato kituo cha Mbulu, ambapo kwa kipindi cha mwaka wa  2018 alilipa kodi ya Tsh.(9,145,263.90).
Pia aliiambia Mahakama hiyo kwamba  Machi 2020 mlalamikaji alipigiwa simu na watuhumiwa akitakiwa  afike katika ofisi za (TRA) Babati wakimjulisha kuwa wamefanya ukaguzi wa biashara yake na kubaini kuwa alikadiriwa vibaya hivyo kumtaka aongeze Tsh 5,812,544.00.
Wakili Kyando aliendelea kutoa maelezo kwamba watumishi hao walimtambulisha tena kwamba kuna ongezeko tena kwenye biashara yake hivyo kutakiwa alipe Tsh.45,000,000/= ama atoe rushwa ya 10,000,000/= na ndipo tasisi hiyo ikaweka mtego na kuwanasa.
Washitakiwa wamekana shitaka na wako nje baada ya kutimiza masharti ya  dhamana ya  shilingi laki saba (7,000,000)  na wadhamini wawili kila mmoja, na kwamba watatakiwa kurudi Mahakamani hapo tarehe 11 Juni 2020 kwa ajili ya shauri hilo  kutajwa.
CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )