SHEIKH KISUKE: USHIRIKIANO BAINA YA WAISLAMU, WAKRISTO UTADUMU MILELE

 Mwenyekiti wa Baraza la Waislamu Manispaa ya Singida, Alhaji Sheikh Hamisi Kisuke.

Na Dotto Mwaibale, Singida

UMOJA na ushirikiano uliopo baina ya Waislamu na Wakristo utaendelea kudumu milele hapa nchini.

Hayo yalisemwa mjini hapa jana na Mwenyekiti wa Baraza la Waislamu Manispaa ya Singida, Alhaji Sheikh Hamisi Kisuke, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika sherehe ya Idd Pili.

Kisuke alisema kushirikiana, kupendana na kuheshimiana baina ya Waislamu na Wakristo ndio kunadumisha hali hiyo hapa nchini.

Alisema Waislamu na Wakristo wamekuwa wakijumuika pamoja katika sherehe zao mbalimbali kama za Idd na Krismas na kila upande ukiona shehere hizo kama ni zake.

” Wakati wa sherehe hizo Waislamu wamekuwa wakiwaalika wakristo na wakristo nao wamekuwa wakiwaalika waislamu” alisema Kisuke.

Kisuke alisema jambo hilo  liliasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere ambaye alisema Serikali ya Tanzania haina dini ila wananchi wake ndio wanadini.

Akizungumzia kuhusu ugonjwa wa Corona Kisuke alimpongeza Rais John Magufuli, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu na viongozi wengine kwa hatua walizozichukua za kukabiliana na ugonjwa huo.

Alisema wao katika ibada ya Idd walifuata maelekezo yote ya kuchukua tahadhari yaliyotolewa na  Mufti Mkuu wa Tanzania, Aboubakary Bin Zubeir, ambapo kila Muislamu aliswali katika msikiti wake badala ya kukusanyika katika viwanja maalumu kama ilivyozoeleka.

“Wakati wa ibada ya Idd tulichukua tahadhari zote kama kunawa mikono kwa maji tiririka, kuvaa barakoa na kuswali kwa kuzingatia umbali wa mita moja huku wakiwepo maafisa afya ambao walikuwa wakisimamia zoezi hilo la kuchukua tahadhari” alisema Kisuke ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Misuna.
CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )