SERIKALI YAZINDUA CHANJO ZA KIMKAKATI 13 ZA MIFUGO, WAZIRI MPINA AWAWEKA KITANZINI WAKURUGENZI

 WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akiwa
na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhandisi Jackson Masaka wakishuhudia uzinduzi wa
Kampeni ya Kitaifa ya utoaji chanjo 13 za kimkakati  za magonjwa ya mifugo katika Kijiji cha
Kinyangiri Mkalama Mkoa wa Singida. Picha Mpiga Picha Wetu

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina
akiswaga ngombe ili wapatiwe chanjo wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Kitaifa ya
uchanjaji mifugo kitaifa katika Kijiji cha Kinyangiri Wilaya ya Mkalama Mkoa wa
Singida. Picha na Mpiga Picha Wetu.


NA MWANDISHI WETU, SINGIDA

SERIKALI imezindua zoezi la chanjo za kimkakati 13 za mifugo kitaifa huku Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akionya wadau wote wanaojishughulisha na uzalishaji, usambazaji na uchanjaji wa mifugo kuzingatia bei elekezi zilizotangazwa na Serikali na kwamba atakayekwenda kinyume atakuwa amevunja Sheria na Kanuni za nchi na hivyo atakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Waziri Mpina amesema juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Pombe Magufuli haziwezi kupotea bure na kuonya halmashauri zitakazozembea katika usimamizi wa zoezi la utoaji chanjo za mifugo.

Mpina amesisitiza kuwa zoezi la utoaji chanjo ya mifugo sio la hiari tena bali ni jukumu la kisheria kupitia Kanuni ya Chanjo na Uchanjaji ya Mwaka 2020 The animal Diseases (Vaccines and Vaccination) Regulation 2020 chini ya Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Namba 17 ya mwaka 2003 ambayo inamtaka kila mfugaji kuchanja mifugo yake dhidi ya magonjwa ya kipaumbele kulingana na kalenda ya chanjo iliyotolewa na Wizara.

Akizungumza wakati wa uzinduzi Kampeni ya Chanjo ya Mifugo Kitaifa katika Kijiji cha Kinyangiri Wilaya ya Mkalama Mkoa wa Singida, Waziri Mpina amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri 82 za wilaya ambao hawajaanza zoezi hilo na zile zinazosuasua kuanza mara moja vingine hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao kwa kurudisha nyuma jitihada za Serikali ya awamu ya tano katika kuleta mageuzi makubwa ya sekta ya mifugo.

Pia Waziri Mpina ameagiza wataalamu wote wa mifugo ngazi ya Wizara, Mikoa, Wilaya na Kata kuhakikisha uchanjaji wa mifugo unatekelezwa kikamilifu kulingana na kalenda ya chanjo kwani jukumu hilo ni la kisheria na kumuagiza Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo(DVS) kusimamia kikamilifu na kuwasilisha taarifa ya chanjo kila mwezi kwa Waziri na kwamba maafisa ambao wameshindwa kusimamia utoaji wa chanjo hatua kali zichukuliwe dhidi yao ikiwa ni pamoja na kufutiwa usajili.

Aidha Waziri Mpina ameziagiza Halmashauri zote ambazo hazitoi huduma ya chanjo kwa mifugo kufanya hivyo mara moja kuanzia mwezi huu wa Julai ripoti ya idadi ya mifugo na aina ya chanjo inayotolewa iwasilishwe kwa Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kila wiki na kwamba halmashauri itayoshindwa ichukuliwe hatua na jukumu hilo kukabidhiwa kwa halmashauri ya jirani.

Kuhusu madeni ambayo Halmashauri zinadaiwa na Wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) yanayokaridiwa kufikia shilingi milioni 125 Waziri Mpina ameagiza ifikapo tarehe 30 Agosti wawe wamelipa na wakishindwa kufanya hivyo halmashauri hizo zifikishwe mahakamani huku Serikali ikimfuatilia mkurugenzi husika uwezo wake wa katika kusimamia majukumu ya Serikali.

Waziri Mpina amesema katika mwaka 2019/ 2020 Halmashauri 103 kati ya 185 sawa na asilimia 56 ndiyo ambazo zimekuwa zikitoa huduma ya baadhi ya chanjo kwa mifugo ambapo dozi 53,851,850 zilichanjwa kwa mwaka 2019/2020 na kwamba idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya mifugo na chanjo za kipaumbele zinazotakiwa kutolewa.

Alisema katika kipindi hicho Mbuzi na Kondoo 2,557,870 zilichanjwa dhidi ya ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo, Ngombe 6,444,871 zilichanjwa dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu ya ngombe (CBPP), Ng’ombe 1, 393, 869, Mbuzi 680,906 na kondoo 192,906 dhidi ya ugonjwa wa Kimeta, Ng’ombe 163, 468 dhidi ya ugonjwa wa kutupa mimba, Ngombe 12,419 dhidi ya ugonjwa miguu na midomo na mbwa 812,712 na Paka 4,152 dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa.

Pia ameagiza Bodi ya Nyama na Dawati la Sekta Binafsi la Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwezesha kujengwa kwa kiwanda cha kuchakata nyama ya kuku na kuupongeza Mkoa wa Singida kwa kuzalisha kuku wa kienyeji milioni 2.6 huku akiagiza kiwanda hicho kiwe kimekamilika kabla ya Disemba mwaka huu.

Kuhusu ombi la kuwepo maabara ya Mifugo wilayani Mkalama, Waziri Mpina amekubali ombi hilo na kwamba kati ya maabara 30 zitakazojengwa mwaka huu wa fedha Wilaya ya Mkalama itapata maabara ili kuwawezesha wafugaji kupata huduma za kitatibu kwa mifugo yao.

Aidha Waziri Mpina amezipongeza Halmashauri kumi zilizofanya viziri katika zoezi la uchanjaji mifugo na idaadi ya dozi walizotoa kwenye mabano ambazo ni Halmshauri ya Tabora Manispaa ambayo (2,703,359), Nyamagana (1,638,550), Dodoma Jiji (620,575), Bariadi Dc (600,100), Igunga Dc (560,000), Nzega (449,675), Shinyanga Manispaa (496,100), Mpimbwe (400,000), Kahama dc (381,100) na Kauliua Dc (346,000).

Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhandisi Jackson Masaka amemshukuru Waziri Mpina kwa juhudi kubwa alizofanya kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya mifugo na uvuvi na kuingia kwenye rekodi ya kuwa moja ya mawaziri walioiwezesha Serikali ya awamu ya tano kuingia kwenye uchumi wa kati kutokana na uchapakazi wake na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya mazao ya mifugo na uvuvi.

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Profesa Hezron Nonga amesema wizara tayari imeshaanda kalenda ya chanjo ambayo ni lazima na kwamba kuanzia mwezi Juni mpaka Agosti ni msimu wa chanjo ya za Homa ya Mapafu ya Ng’ombe, Homa ya Mapafu ya Mbuzi, Sotoka ya Mbuzi na Kondoo, Kimeta, Ugonjwa wa kutupa mimba na ugonjwa wa miguu na midomo hivyo kuwataka madaktari wa mifugo wote nchini kuhakikisha chanjo hizo zinatolewa kikamilifu na kumhakikishia Waziri Mpina kuwa maagizo yote aliyotoa atayasimamia kikamilifu.

 Kiongozi wa Wafugaji Kijiji cha Kinyangiri, Edward Magala ameshukuru Serikali kwa uamuzi wake wa kuzindua chanjo ya mifugo kwani mifugo mingi ilikuwa inakufa kwa kukosa huduma na kwamba sasa watapata ahueni kubwa itakayowezesha kuongezeka kwa uzalishaji.

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )