Serikali Yaridhishwa Na Zoezi La Kuwadhibiti Nzige

 

 Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda ameridhishwa na kazi ya kuangamizwa makundi ya nzige kwenye wilaya za Simanjiro, Siha na Longido kufuatia ndege maalum kunyunyizia kiuatilifu na kuua nzige hao wa jangwani. 


Akiwa kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa zoezi la kuangamiza makundi ya nzige jana (24.02.2021) kwenye wilaya za  Simanjiro na Siha Prof. Mkenda alishuhudia makundi ya nzige waliokufa baada ya kupuliziwa kiuatilifu (sumu) kazi iliyofanywa na wataalam wa wizara ya kilimo kwa ushirikiano na wataalam wa wilaya hizo. 


“Tunawashukuru watalaam wetu wa kilimo kwa kazi nzuri ya kudhibiti makundi ya nzige licha ya ugumu wa mazingira ya kuingia vichakani na kuangamiza nzige porini .Nimeshuhudia nzige wengi wamekufa” alisema Waziri Mkenda  


Akiwa kwenye kijiji cha Landanai kata ya Lokosonoi wilaya ya Simanjiro Prof. Mkenda alijionea makundi ya nzige waliokufa kufuatia zoezi la kuwapulizia dawa kwa njia ya ndege pia mabomba ya kupulizwa kwa mikono iliyofanywa na wataalam wa kilimo. 


Akizungumza kuhusu mikakati ya kudumu ya kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao ikiwemo nzige na kwelea kwerea, Waziri Mkenda alisema wizara itaanzia Idara ya Kilimo Anga ambapo kwenye bajeti ya mwaka huu itatenga fedha za kununua ndege (drones) kwa ajili ya kunyunyizia viuatilifu pale makundi ya wadudu waharibifu yatakapotokea nchini. 


Amewahakishia wakulima na wafugaji nchini kuwa serikali iko makini kuhakikisha nzige na visumbufu vingine vya mazao na malisho ya mifugo vinaangamizwa  na kuwa viautilifu kwa ajili ya kazi hiyo vipo nchini. 


“Suala la kupambana na nzige wa jangwani ni kama vita lazima tushirikiane wote ikiwemo nchi jirani ya Kenya kuwateketeza hivyo nitawasiliana na wenzetu kujua namna wanavyofanya kazi ya kuangamiza nzige ili wasije kuingia kwenye mipaka yetu” alisisitiza Prof. Mkenda 

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )