SERIKALI KUTUMIA ZAIDI YA SH. MILIONI 100 KUIMARISHA KITUO CHA KUTOTOLESHA VIFARANGA VYA SAMAKI CHA RUHILA

Afisa Mfawidhi, Kituo cha kutotolesha Vifaranga vya Samaki cha Ruhila, Emmanuel Maneno (wa kwanza kushoto) akimueleza jambo Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (katikati) alipotembelea Kituo hicho kilichopo Mkoani Ruvuma jana.  Wa kwanza Kulia ni Mkurugenzi, Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji WMUV), Dkt. Nazael Madalla.

  1. Mkurugenzi, Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji (WMUV), Dkt. Nazael Madalla (wa kwanza kushoto) akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (wa tatu kutoka kushoto) alipotembelea Kituo cha kutotolesha Vifaranga vya Samaki cha Ruhila kilichopo Mkoani Ruvuma jana.
  1. Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akinawa maji ya Ziwa Nyasa alipotembelea Kituo cha Udhibiti wa Rasilimali za Uvuvi Ziwa Nyasa kilichopo Mbamba Bay, Wilayani Nyasa, Mkoani Ruvuma jana. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi, Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji (WMUV), Dkt. Nazael Madalla.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (wa tatu kutoka kulia – aliyevaa koti) akieleza jambo wakati akiangalia moja ya Mabwawa ya kufugia Samaki alipotembelea Kituo cha Kutotolesha Vifanga vya Samaki cha Ruhila kilichopo Mkoani Ruvuma jana. Wa pili kutoka kulia ni Mkurugenzi, Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji (WMUV), Dkt. Nazae.


 

Na Mbaraka Kambona, Ruvuma

 

Katibu Mkuu, Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah amesema kuwa Serikali imepanga
kutumia Shilingi Milioni 110 kwa ajili ya kuimarisha miundo mbinu ya Kituo cha Kutotolesha
Vifaranga vya Samaki cha Ruhila ili kiweze kuzalisha vifaranga vitakavyokidhi
mahitaji yaliyopo sasa.
 

Dkt. Tamatamah aliyasema
hayo alipotembelea kukagua shughuli zinazofanywa na kituo hicho kilichopo
Mkoani Ruvuma jana.
 

Alisema kuwa kwa mwaka huu
wa fedha 2020/2021 Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepanga
kuzalisha vifaranga Milioni 22, na kati ya hivyo, vifaranga Milioni 16
vitazalishwa na vituo vya kutotolesha vya watu binafsi na vifaranga Milioni 6 vitazalishwa
na vituo vya Serikali.
 

Dkt. Tamatamah aliongeza
kuwa hivi karibuni Wizara itatangaza zabuni kwa ajili ya kuimarisha na
kuboresha kituo hicho ili kiweze kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuzalisha
vifaranga utakaowezesha kukidhi mahitaji yaliyopo sasa.
 

“Baada ya kukiimarisha
kituo hiki mwaka huu, mwaka ujao wa fedha tutafanya ukarabati mkubwa na
ukarabati huo ukikamilika tunatarajia uwezo wa uzalishaji wa kituo hiki kuongezeka
mara tatu zaidi ya sasa na hivyo kutaongeza uhakika wa upatikanaji wa vifaranga
vya samaki,’’alisema Dkt. Tamatamah.
 

Naye, Mkurugenzi wa Idara
ya Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Nazael Madalla alitoa rai
kwa Watanzania hasa wale wanaoishi mbali na vyanzo vikubwa vya maji kama maziwa
kujihusisha na shughuli za ufugaji wa samaki kwani kwa kufanya hivyo
kutawasaidia kupata kipato na lishe bora.
 

“Naomba Watanzania watembelee
kituo hiki ili waweze kujifunza kwa vitendo namna ya kuchimba mabwawa makubwa
na kufugaji samaki ili kujiongezea kipato na lishe bora kwa ajili yao na Watoto
wao,” alisema Dkt. Madalla.
 

Kaimu Katibu Tawala
anayeshughulikia Uchumi na Uzalishaji, Mkoani Ruvuma Deogratius Sibula alisema
kuwa Ruhila kimekuwa kituo muhimu sana kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa
sababu wafugaji wengi wanategemea kituo hicho kupata vifaranga vya samaki kwa
ajili ya kufuga.
 

“Katika Mkoa wa Ruvuma kuna
Wafugaji wa Samaki takriban Elfu nne (4000) na kuna mabwawa ya Samaki zaidi ya
Elfu Sita (6000) na wote wamekuwa wakitegemea kituo hiki kwa ajili ya kupata
mbegu na kupata elimu ya ugani, hivyo ni kituo muhimu sana katika kuchagiza ongezeko
la ufugaji wa samaki na upatikanaji wa lishe bora kwa Wananchi,” alisema Sibula.
 

Naye, Afisa Mfawidhi wa
Kituo cha Ruhila, Emmanuel Maneno alisema kuwa baadhi ya Mikoa ya Nyanda za Juu
Kusini inakabiliwa na Utapiamlo hivyo fursa ya uhakika ya kuondokana na tatizo
hilo ni kufuga samaki ambao watawahakikishia kupata lishe bora na kipato cha
kujikimu kimaisha.
 

Maneno aliongeza kuwa Mikoa
ya Nyanda za Juu Kusini ina mazingira mazuri ya kufuga samaki kwa sababu hali
ya hewa ni nzuri, maji yapo ya kutosha lakini pia malighafi kwa ajili ya
kutengenezea chakula cha samaki inapatikana kwa urahisi na hivyo kufanya
gaharama za ufugaji wa samaki kuwa chini.

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )