RUFAA YA MBOWE NA WEZAKE KUANZA KUSIKILIZWA MEI 13,2020

RUFAA iliyokatwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake saba katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kupinga hukumu dhidi ya kesi ya uchochezi na mashtaka mengine iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, itaanza kusikilizwa Mei 13, mwaka huu.

Kesi hiyo iliitwa leo Aprili 23, 2020 kwa ajili ya kutajwa mbele ya Jaji Mfawidhi, Lameck Mlacha ambaye pamoja na mambo mengine ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 28, mwaka huu huku pia akipanga ianze kusikilizwa Mei 13 mbele ya Jaji Ilvin Mgeta Mei 13.

Katika rufaa hiyo namba 76 ya mwaka 2020 wakata rufani ni Mbowe na wenzake wanaiomba mahakama iamuru hukumu na adhabu iliyotolewa dhidi yao ifutwe kwa kuwa kuna mambo kadhaa yalikosewa

Mbali na Mbowe, warufani wengine ni Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu-Zanzibar, Salum Mwalimu,  Mbunge wa Iringa Mjini,  Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, Halima Mdee (Kawe), John Heche (Tarime Vijijini) na Ester Bulaya (Bunda).

Machi 10, 2020 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwahukumu warufani pamoja na  Dk.Vicent Mashinji ambaye alihamia CCM akitokea Chadema kulipa faini ya jumla ya Sh milioni 350 au kifungo cha miezi mitano jela baada ya kuwatia hatiani kwa makosa 12 kati ya 13 yaliokuwa yakiwakabili.
Hata hivyo, warufani hao kwa nyakati tofauti walilipa faini hiyo na kukwepa kifungo.

Katika rufaa hiyo, warufani wamewasilisha sababu mbali mbali wakidai kuwa  Mahakama ya Kisutu imefanya  makosa ya kisheria kufikia maamuzi ya kesi ya msingi bila ya upande wa mashitaka kuthibitisha pasipo shaka.

Wanadai Mahakama ya Kisutu ilikosea kisheria  kushindwa kufanya mchanganuo mzuri kwa kufuata ushahidi uliotolewa huku pia wakudai mahakama ilishindwa  kuainisha viini vya makosa dhidi ya Mashtaka na kuwahukumu bila kuzingatia utetezi wa washtakiwa.

Pia katika rufaa hiyo wanadai mahakama imeshindwa kuzingatia ushahidi kwa kushindwa kuangalia uwepo au ushiriki wa baadhi ya washitakiwa kwenye mkutano na kuwahukumu kwenye mashitaka ya  2,3 na 4.

 Warufani hao wanadai mahakama hiyo ilikosea kupokea vielelezo vya kielektroniki ambavyo ni video, imekosea kisheria kuzingatia mashitaka ya 11,12 na 13 yamewafanya washitakiwa washindwe kujitetea na kwamba ilikosea kisheria kuangalia maneno yaliyotolewa katika mashitaka ya 5,6,7,8,9,10 kwamba hayawezi kuhesabika kuwa makosa ya jinai kwa mujibu wa maamuzi yaliyotolewa katika kesi ya Hussein Katanga dhidi ya Jamhuri (1974) ukurasa wa 97 wa hukumu hiyo.

Aidha wanadai hakukuwa na maelekezo ya awali yaliyofanyika sambamba na  kupuuzwa kwa haki ya uwakilishi ma kuongeza kuwa mahakama ilikosea katika kutoa adhabu dhidi ya warufani ya  kulipa faini ambayo  ilikuwa inajitegemea wakati adhabu ya kifungo ilikuwa inaenda kwa pamoja hali hiyo imesababisha kuleta mkanganyiko wa kisheria.
CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )