Mkurugenzi wa Jandu Constructions and Plumber Ltd kizimbani kwa uhujumu uchumi

Mkurugenzi
wa Kampuni ya Jandu Constructions and Plumber Ltd, Khairoon Jandu, na
wenzake watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka kumi na moja
likiwemo la wizi na utakatishaji fedha zaidi ya  Sh bilioni moja.


Washtakiwa
wengine katika kesi hiyo binti yake Khairoon, Zainabu Tharia, Wakili wa
kujitegemea Mohamed Majaliwa na Meneja wa benki ya Exim Inrahim
Sangawe.

Katika
hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo Wakili wa Serikali
Mwandamizi Mkunde Mshanga akisaidiana na Wankyo Simon imedai kuwa, kati
ya Januari na Desemba 2010 hadi 2017 jijini Dar es Salaam washtakiwa kwa
kudhamiria waliunda genge la uhalifu ili kuweza kutenda kosa la
kughushi na kuiba fedha.

Mbele
ya Hakimu Mkazi Mkuu Kasian Matembele imedaiwa katika shtaka la pili
kuwa, Januari 16, 2017 jijini Dar es salaam, mshtakiwa Khairoon
alighushi saini ya Inderjit Jandu katika nyaraka zilizoonesha kuwa ni
nyaraka halali za kikao cha Kampuni ya Jandu huku akijua si kweli.

Pia
Khairoon anadaiwa kughushi saini ya Inderjit Jandu katika nyaraka za
kampuni zinazoonesha amechaguliwa kuwa Mkurugenzi wa kampuni hiyo
akionesha ni nyaraka halali huku akijua kuwa si kweli.

Imeendelea
kudaiwa kuwa, Mei 25, 2019 mshtakiwa  Khairoon akiwa na nia ya
udanganyifu alighushi saini ya Inderjit Jandu akionesha kuwa Inderjit
amehamishia hisa za kampuni kwake huku akijua si kweli huku pia akidaiwa
kughushi nyaraka za wosia ulioandikwa na Inderjit akionesha ni wosia
halali huku akijua si kweli.

Wakili Mshanga aliendelea kudai kuwa katika shtaka la sita, saba
na nane Khairoon alitoa nyaraka za uongo kwa BRELA zilizoonesha kuwa ni
nyaraka halali za vikao vya kampuni ya Jandu zilizoonesha kuwa
amechaguliwa kuwa Mkurugezi wa kampuni hiyo na pia amehamishiwa hisa za
kampuni huku akijua kuwa nyaraka hizo si za kweli.


Shtaka
la tisa linalomkabili Khairoon lilisomwa na Wakili Serikali Mwandamizi
Wankyo Simon ambaye alidai katika tarehe tofauti mwaka 2020 aliiba Sh
1,033,860,100 mali ya Kampuni ya Jandu Constructions and Plumber.

Aidha
katika kosa la kumi linalomkabili mshitakiwa wa tatu Ibrahim Sangawe,
wakili Simon alidai katika tarehe tofauti mwaka 2019 ndani ya Jiji na
Mkoa wa Dar es Salaam akiwa ni Meneja wa benki ya Exim Sangawe
alishindwa kuzuia wizi wa kiasi hicho cha fedha kilichokuwa
kimehifadhiwa katika benki hiyo.

Katika
shtaka la kumi na moja, mshtakiwa Khairoon na Tharia  wanadaiwa
kutakatisha fedha Sh 1,033,860,100 ambapo  walijipatia fedha hizo mali
ya Kampuni ya Jandu huku wakijua fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la
wizi.

Baada
ya kuwasomea mashtaka Wakili Simon alidai upelelezi wa shauri hilo bado
haujakamili hivyo aliomba tarehe nyingine ha kutajwa.

Hakimu
Matembele ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 20, 2020 itakapokuja kwa
ajili ya kutajwa. Washtakiwa hawakurusiwa kujibu chochote na wamepelekwa
rumande
CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )