MILIONI 90 ZA EP4R ZAJENGA MADARASA SEKONDARI SOKON II     Serikali katika kutekeleza mikakati ya kuboresha miundombinu ya shule zake za serikali, imefanikiwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa, shule ya sekondari ya Sokon II, halmashauri ya Arusha, wilaya ya Arumeru kwa gharama ya shilingi milioni 90.
    Akielezea utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Saad Mtambule alipotembelea mradi huo, amesema kuwa, kiasi hicho cha fedha kimefanikisha ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na matundu ya vyoo, huku ukiwa tayari umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 na upo kwenye hatua za mwisho za ukamilishaji.
    Mkurugenzi Mtambuka, ameweka wazi kuwa, ujenzi huo umetekelezwa kwa wakati, ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Ubalozi wa Japan, katika mkataba wa ujenzi wa  jengo la ghorofa 2 lenye vyumba 12, katika shule hiyo ya sekondari Sokon II, huku Ubalozi wa Japani ukiwa umeshakamilisha ujenzi wa msingi wa jengo wenye vyumba vinne vya madarasa, vyoo, pamoja na samani za madarsa hayo, kwa gharama ya shilingi milioni 196.
     Umakini wa Serikali katika utekelezaji wa mikataba kati yake na serikali ya Japani, umewezesha ujenzi wa jengo la ghorofa mbili lenye vyumba vya madarasa 12 na matundu ya vyoo, huku msingi wa ghorofa na vyumba vinne vya madarasa vikiwa vimekamilika kwa ufadhili wa Ubalozi wa Japan na ghorofa ya kwanza, ikiwa kwenye hatua za mwisho kupitia fedha hizo za EP4R.
       “Tulikubalina na wenzetu wa Ubalozi wa Japani, kujenga jengo hilo, ambalo tayari Ubalozi huo, ulianzisha msingi na kukamilisha vyumba vinne na vyoo, mwanzoni mwa mwaka huu, na wanafunzi wanatumia vyumba hivyo, Serikali yetu nayo imetoa shiligi milioni 90 zilizojenga vyumba vinne vya ghorofa ya kwanza, na tunategemea kumalizia vyumba vinne vya ghorofa ya mwisho” amesema Mkurugenzi huyo.
     Naye Mkuu wa shule ya sekondari Sokon II, mwalimu Prisca Mbele, amethibitisha kuwa, uboreshaji huo wa miundombinu ya shule, unawezesha mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia kwa wananfunzi na walimu, jambo linalofanikisha kuimarika kwa utoaji wa taaluma na kupandisha kiwango cha ufaulu
      “Shule inapokuwa na mazingira mazuri ya kujifunzia,  hasa madarasa, yanahamasisha tendo zima la kufundisha na kujifunza kwa walimu na wanafunzi wanakuwa na amani, mazingira mazuri yanarahisisha tendo la kujifunza na kufundisha kwa wanafunzi na walimu pia” amesema Mkuu huyo wa shule.
       Aidha mkuu huyo wa shule amefafanua kuwa, kukamilika kwa ujenzi huo, kutafikisha jumla ya vyumba 21 vya madarasa katika shule hiyo, huku kukiwa na upungufu wa vyumba vitano, ambavyo tayari vipo kwenye mkakati wa kutekeleza ujenzi wake, ili shule hiyo kuwa na vyumba vya kutosha vya madarasa kwa wanafunzi wote wa shule hiyo.
          Shule ya sekondari ya Sokon II ni miongoni mwa shule za kata zinazokuwa kwa kasi, ilianza mwaka 2015 na ina jumla ya wanafunzi 988 ikiwa na wasichana 528 na wavulana 462 wa kidato cha kwanza mpaka cha nne.

Mkuu wa shule ya sekondari Sokon II mwalimu Prisca Mbele, akimuonyesha majengo ya shule hiyo, Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, alipotembelea shuleni hapo,mkukagua shughuli za maendeleo ya shule hiyo.
Jengo la ghorofa mbili lenye vyumba 8 vya madarasa, lililojengwa kwa ushirikino wa  Serikali na Ubalozi wa Japani nchini Tanzania.

Vyumba vinne vya madarasa na vyoo, sekondari Sokon II  vilivyojengwa na serikali kupitia miradi ya EP4R kwa gharama ya shilingi milioni 90.
Muonekano wa juu wa jengo la ghorofa sekondari Sokon II
CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )