MBUNGE LEMA APANDISHWA KIZIMBANI SINGIDA ATUHUMIWA MAKOSA 15

 Mbunge wa Arusha Mjini na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)  Kanda ya Kaskazini, Godbles Jonathan Lema akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mjini Singida ambapo alisomewa mashitaka akituhumiwa kwa makosa 15.

Mbunge wa Arusha Mjini na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)  Kanda ya Kaskazini, Godbles Jonathan Lema akizungumza na wanasheria na makada wa chama hicho baada ya kusomewa mashitaka.


Na Ismail Luhamba, Singida

MBUNGE wa Arusha Mjini na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)  Kanda ya Kaskazini, Godbles Jonathan Lema, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini hapa jana, akituhumiwa kwa makosa 15.
Mapema mwendesha mashitaka mwanasheria wa serikali kutoka jijini Dar-es-salaam Monica Mbogo, alidai mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama Mkazi, Consolata Singano, kuwa mshitakiwa Lema ametenda makosa hayo 15 Februari 29 mwaka huu  wilayani Manyoni mkoani Singida. Mshitakiwa ametenda makosa hayo  huku akijua wazi ni kinyume na sheria namba 16 ya makosa ya mitandao.
Mwendesha mashitaka Monicha alisema kuwa shitaka la kwanza linalomkabili Lema ni kusababisha taharuki kwa jamii baada ya kusambaza taarifa za upotoshaji.
Akifafanua, alisema kuwa wakati akihudhuria mazishi ya kiongozi wa Chadema wilaya ya Manyoni, Alex, mshitakiwa Lema alisema ‘nina wasi wasi mkubwa sana nimepewa listi ya watu ambao wameisha uawa kuanzia mwaka jana mwezi wa nane 2019 hadi sasa ya kuchinjwa watu 14’.
Alisema nukuu nyingine ya Lema iliyosababisha taharuki ni, ‘hii issue is very serius na kama hamtachukua hatua…wote nyie hapa mtaongezeka kuchinjwa, na bahati mbaya watanzania wameanza kuzoea taabu na mauti kama sehemu ya maisha yao ya kawaida’.
Monica ametaja watu ambao Lema  amewataja kuuawa kwa kuchinjwa na makazi yao kwenye mabano,ni Sechelela Moses,(Manyoni mjini), Abdalah Lyanga (Itigi), Rajabu Abas (Itigi), Martiner Mtekwa (Manyoni mjini)
Ametaja wengine kuwa ni Hamad Hussein (Aghodi), Emmanuel Messo (Maweni), Mika Saimoni (Mkoko), Nyembelele Njezo (Mitundu) John Lugion) (Makale) Michael Charles )Mwamagembe) Issa Abdala (Sajalanda).Jumanne Ndelemo (Sajilila),Heri Mambo (Solya) Alex Jonas (Manyoni mjini) John Lugion) (Makale) Michael Charles )Mwamagembe) Issa Abdala (Sajalanda).
Alisema makosa mengine 14 yanayomkabili mshitakiwa ni kwamba huku akijua na akiwa na nia ya kupotosha jamii, alitoa taarifa za uongo juu ya mauaji ya watu 14 kwa nyakati tofauti.
Mwendesha mashitaka huyo, alisema katika upotoshaji huo, mshitakiwa alitumia mfumo wa kompyata kwenye akaunti yake ya twitter yenye jina lake la Godbles Jonathan Lema, kusambaza upotoshaji huo kwenye mitandao.
Mshitakiwa ambaye anawakilishwa na wanasheria wa kujitengemea wa mkoa wa Singida Mwiru Amani na Hemed Nkulungu, alikana makosa yote hayo.
Hakimu Singano alitoa masharti ya dhamana kuwa mshitakiwa anapaswa kuwa na wadhamini wawili wanaoaminika na kutoa ahadi ya dhamana ya shilingi milioni tano kila mmoja.
Mshitakiwa Lema alimudu kutimiza sharti hilo la dhamana, na yupo nje hadi aprili 15 mwaka huu, kesi yake itakapotajwa tena.
Katika kesi hiyo,mwanasheria wa serikali anasaidiwa na wanasheria wa serikali mkoani Singida, Rose Chilogola, Michael Ng’hoboko na Karem Marando.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Singida, Emmanuel Jingu, alisema kuwa wametekeleza agizo la Rais Magufuli la katazo la umati mkubwa wa watu, ndio maana kesi ya Lema imehudhuriwa tu na viongozi wachache,.
CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )