Mbunge Jituson wa Babati Vijijini agawa Miti 5,100 ya Matunda Jimboni.

Na John Walter-Babati
Mbunge wa Jimbo la Babati vijijini Jituson Vrajilal,  ameendelea kutekeleza ahadi zake katika jimbo hilo ambapo katika awamu hii amewapelekea wananchi wake miti ya matunda ya muda mfupi kutoka chuo kikuu cha Kilimo Morogoro (SUA).

Mheshimiwa Jituson amesema katika jimbo hilo lenye vijiji 102  amegawa miti ya matunda mbalimbali 5,100  ambapo kila kijiji kimepata miti 50 yenye thamani ya shilingi 2,500 kila mmoja.

Akizungumza akiwa katika kijiji cha Mandi kata ya Dabil na kijiji cha Bermi, amesema Manyara ni miongoni mwa mikoa inayokabiliwa na tatizo la utapiamlo na udumavu kwa asilimia 36, hivyo miti hiyo ya matunda ikitunzwa vyema  itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo hilo kwa kuwa ni kati ya vitu muhimu katika lishe.

Ameeeleza kuwa mbali na matunda kusaidia katika kuupatia mwili vitamin,lakini pia itawasaidia wananchi hao kupata kipato pamoja na kuboresha Mazingira.

Mheshimiwa Jituson amewaambia  wananchi hao wahakikishe  wanaitunza miti hiyo ili kuhifadhi mazingira pamoja na kuingiza kipato kwa kuwa soko la matunda duniani ni kubwa.

Katika hatua nyingine Jitu  amewataka viongozi watakaosimamia ugawaji wa miti hiyo kuandika jina  na namba ya simu ya mpokeaji  na kufanya ukaguzi, na endapo itatokea mti umekufa, aliekabidhiwa awajibike kurudisha gharama ambapo mche mmoja itatakiwa kulipiwa shilingi elfu tano (5000).

Nao wananchi wamemuahidi mbunge huyo kuwa wataitunza miti hiyo  kwa kuwa watakaonufaika nayo ni wao na familia zao.

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )