LUKUVI AZINDUA OFISI YA ARDHI MKOA WA MANYARA.

 Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameziataka ofisi za ardhi za mikoa
zilizozanzishwa hivi karibuni kuwa na daftari maalum lenye orodha ya migogoro
ya ardhi ili kurahisisha ufuatiliaji sambamba na utatuzi wa migogoro kwenye mikoa.

Akizungumza wakati wa
uzinduzi wa Ofisi ya Ardhi ya Mkoa juni 23,2020 mkoani Manyara, Lukuvi alisema kila
ofisi ya ardhi ya mkoa inatakiwa kuwa na daftari zuri lenye orodha ya migogoro
yote ya ardhi kwenye mkoa husika ikiwa ni mkakati wa kushughulikia migogoro ya ardhi.
‘’Sasa hivi
hatutegemei migogoro mipya maana migogoro tunayoshughulika nayo sasa ni ile ya
miaka ya nyuma hivyo muorodheshe migogoro yote iliyopo wilayani na kuanza
kuishughulikia’’ alisema Lukuvi.
Waziri Lukuvi
ameshangazwa na ofisi za ardhi katika halmashauri za wilaya nchini kushindwa
kutatua migogoro ya mipaka baina ya wilaya na wilaya wakati halmashauri hizo
zina wataalamu wa sekta ya ardhi wanaoweza kuitafsiri GN.
Katika hatua nyingine Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi William Lukuvi ameagiza kufanyika ukaguzi wa mashamba makubwa
yaliyomilikishwa kwa wawekezaji kwenye mkoa wa Manyara ili kubaini mashamba
yasiyoendelezwa.
Hatua hiyo inafuatia
kuelezwa na Mkuu wa mkoa wa Manyara Alexzander Mnyeti kuwa, mkoa huo una
mashamba makubwa yasiyoendelezwa kwa muda mrefu wakati uhitaji wa mashamba kwa
wananchi wa mkoa huo ni mkubwa kutokana na ongezeko la idadi ya watu.
‘’Hatujatoa ardhi kwa
ajili ya kuweka akiba, kazi ya ukaguzi mashamba ni ya kwenu hivyo myaangalie
kama yameendelezwa, yana faida gani na yanalipa kodi’’ alisema Waziri Lukuvi.
Kwa upande wake Mkuu
wa mkoa wa Manyara Alexzander Mnyeti aliwapongeza watumishi wa sekta ya ardhi
katika mkoa wake kwa kufanya kazi kwa utii na nidhamu  tofauti na
ilivyokuwa huko nyuma kwa watumishi wa sekta hiyo.
Mnyeti aliongeza kwa
kusema kuwa, mkoa wa Manyara umekuwa na tatizo la wananchi kuvamia maeneo ya
umma ambapo alisema uvamizi huo unachangiwa na kukosekana hati miliki za maeneo
hayo na hivyo kutoa mwanya maeneo hayo kuvamiwa.
Naye Katibu Mkuu Wizara
ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo alisema Wizara yake
imefanikiwa katika suala la usimamizi rasilimali ya ardhi huku lengo likiwa
kutaka kupima kila kipande cha ardhi na kuwamilikisha wananchi jambo
alilolieleza itapunguza migogoro na wakati huo kuiingizia serikali mapato
yatokanayo na kodi ya pango la ardhi.

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )