Kutumia mitishamba bila utaratibu kunaweza kuharibu figo, maini – Profesa Mgaya.

TANGU kuingia kwa ugonjwa wa Covid- 19 ulioanzia nchini China, Desemba mwaka jana, watafiti mbalimbali duniani wameendelea kufanya tafiti ili kubaini dawa au kinga ya ugonjwa huo.


Miongoni mwa tafiti zinazoendelea ni pamoja na zile zinazofanywa hapa nchini, ikiwamo inayofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).

HISTORIA YA NIMR

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya NIMR, Profesa Yunus Mgaya, anasema kuwa taasisi hiyo ilianzishwa kwa sheria ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, namba 23 ya    mwaka 1979 na kuanza kufanya kazi rasmi mwaka 1980, ikiwa na wafanyakazi wanasayansi 13 sasa wameongezeka na kufikia 400.

NIMR ni taasisi iliyo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, huku kazi yake kubwa ikiwa ni pamoja na kufanya utafiti, inaratibu, inakuza na kusimamia tafiti za afya zinazofanyika nchini na kukuza matumizi ya matokeo ya tafiti hizo.

Hadi sasa, ina idara ya tafiti za Tiba Asili ambayo jukumu lake ni kufanya utafiti juu ya dawa za miti shamba, ambazo nyingine zimekuwa zinatumika miaka mingi tangu enzi za bibi na babu zetu.

LENGO LA NIMR

Ni kuondoa mzigo wa magonjwa hasa yasiyopewa kipaumbele, pia kushirikiana na Serikali kufanya tafiti za kisayansi za afya na kuziratibu.

Kufanya udhibiti na tafiti za tiba za asili na kushauri serikali au Wizara ya Afya kwenye tafiti zinazofanyika na zina matokeo ya kisera hupeleka wizarani ili izitumie katika afua mbalimbali, utungaji sera na miongozo ya kitiba.

“Tunashukuru Mungu hadi sasa tuna miaka 40 katika utendaji kazi wetu lakini kuna tafiti 100 zinaendelea na nyingine tulizofanya zimeleta matokea mazuri katika jamii,” anasema Profesa Mgaya.

MATOKEO YA TAFITI

Akitolea mfano wa teknolojia ya uwekaji dawa kwenye vyandarua ulizinduliwa na taasisi hiyo, Amani mkoani Tanga.

Anasema pia usugu wa dawa ya malaria ya Chloroquine ni matokeo ya taasisi hiyo ambapo ilifanya utafiti kwa watu wengi na kubaini watu 10 wanaotumia dawa hiyo hawaponi.

Mgaya anasema pia amefanya tafiti mbalimbali kwenye magonjwa ya Kifua Kikuu, vimelea vya Ukimwi na magonjwa yasiyoambukiza.
“NIMR imedhamiria kupunguza vifo kwa wagonjwa wenye maambukizi ya fangasi (Cryptococcus Neofroman) na kusababisha homa ya UTI ya mgongo (Cryptococcal Meningitis) kwa wagonjwa walioathirika na Ukimwi,” anasema Profesa Mgaya.

Anasema utafiti wao wa awali walibaini kuwa kati ya watu 10 wenye Ukimwi wakipata fangasi wa UTI ya mgongo saba  hufariki.

“Yaani katika watu 10 wakipata ugonjwa huu, asilimia 70 walikuwa wanakufa, lakini sasa hivi dawa hizi zimesaidia kupambana na virusi hivyo vya homa ya UTI wa mgongo,” anasema Profesa Mgaya.

Anasema waligundua mchanganyiko wa dawa mbili ambazo zinatolewa kwa sasa,  zinazosaidia mgonjwa wa Ukimwi wakipata fangasi wapone. “Sasa hivi tumetoka asilimia 70  ya awali hadi kufikia 30, ambapo ilibainika baada ya kufanyika utafiti na miongozo ikatolewa,” anasema.

Anasema pia wanaendelea na tafiti za tiba nyingine ikiwamo zile zinazoikabili jamii ya watu wenye kipato cha chini mfano matende, mabusha, usubi na vikope. 

MAFANIKIO

Mgaya anasema hadi sasa, NIMR imefanikiwa kuzalisha dawa mbalimbali ikiwamo ya tezi dume, seli mundu, malaria na dawa lishe ya NIMRCAF inayotumika kuimarisha kinga ya mwili.

Anasema bado wanaendelea na tafiti 100 ambazo zipo kwenye hatua mbalimbali.

Akizungumzia mchango wa NIMR katika kupambana na virusi vya corona, anasema walibaini dawa lishe ya NIMRCAF itokanayo na viungo asilia na kuleta  matokeo bora katika kutibu dalili za awali za ugonjwa hatari wa COVID-19.UTENGENEZAJI

Anasema dawa hiyo inatengenezwa kwa kufuata vipimo maalum kulingana na wingi wake, ambapo mchanganyiko wake unajumuisha tangawizi, pilipili kichaa, kitunguu maji chekundu, kitunguu swaumu na limao la kijani.

Anasema unaweza kutengeneza dawa hiyo kwa kutumia tangawizi punje tano, kitunguu maji kimoja, punje za kitunguu swaumu kumi, malimao mawili na pilipili kichaa ambapo unakatakata na kuzisaga pamoja kwenye mashine ya kusagia, kisha unaichuja na kuchanganya na maji nusu lita.

“Dawa hii kwa sasa ipo kwenye utafiti ili iweze kutoa ushuhuda wa kile kinachosemwa kama ina uwezo wa kutibu dalili za ugonjwa huo,” anasema Mgaya.

Anasema dawa hiyo mtu anaweza kuitumia kama chakula cha kawaida kwani inaweza kusaidia kuzuia kushambuliwa na ugonjwa huo na hata mtu akipata asione dalili kabisa.

Anasema tiba lishe hiyo imesheheni kemikali za kumsaidia mtu kumkinga na magonjwa ikiwamo kifua kubana (pumu) na hata magonjwa ya saratani.

Anasema NIMR wameamua kuandika vitu vyote vinavyotumika katika uandaaji wa dawa hiyo ili hata wale wasio na kipato waweze kutengeneza wakiwa majumbani kwao hatimaye kupambana na ugonjwa huo.

Anasema watoto wenye umri wa miaka mitano na kuendelea wanaweza kuitumia dawa hiyo, na wale wenye vidonda vya tumbo wanapaswa kuitumia kwa tahadhali.

Anasema kwa sasa wameongeza uwezo wa kuzalisha dawa hiyo kutoka chupa 3,000 hadi kufikia 7,000 kwa siku.

Anasema dawa hiyo uhifadhi wake unatakiwa usizidi nyuzi joto 30 au kuigandisha, na kwamba kwa wale wanaohitaji kununua badala ya kutengeneza majumbani wanaweza kuipata katika ofisi za idara zilizopo Mabibo jijini Dar es Salaam.

Anasema dawa hiyo ikihifadhiwa vizuri inaweza kukaa bila kuharibika hata kwa muda wa mwaka mzima.

KUJIFUSHA

Akizungumzia suala la kujifusha na mvuke anasema matibabu hayo yalianza miaka ya nyuma ambapo tafiti zinaonyesha asilimia 70 ya Watanzania hutumia njia hiyo ikiwa ni tiba asili.

“Dawa hizi wengi wanazitumia kwa miongozo maalum kwani ukizidisha kipimo unaweza kuathiri figo na maini,” anasema Profesa Mgaya.

Anasema nchi mbalimbali wanajifusha na ndio maana mataifa mengine wana Sauna ambazo mtu anaingizwa kwenye chumba chenye joto na kutoka kwa dakika kadhaa.

“Ukitoka kwenye joto hilo ambalo lingine linafika nyuzi joto 40 hadi 45, inasaidia kulegeza mishipa ya damu na kujisikia vizuri,” anasema Mgaya.

MITI INAYOFAA KUJIFUSHA

Anaitaja miti inayofaa kwa kujifusha kuwa ni pamoja na mkaratusi, mchaichai, kifumbasi (kashagwala), miembe na mipera, huku akitoa tahadhali kwa baadhi ya miti ukiwamo mwarobaini akidai si mzuri kutumika kwa sababu una kemikali zenye sumu.

Anasema si lazima utumie miti hiyo yote, bali unaweza mmojawapo na kujifusha kwa wiki mara tatu au moja kulingana na muda wa mhusika.

Mgaya anasema unaweza kuchemsha maji kisha ukachukua majani yao ya miti uliyoandaa na kuyaloweka kisha kujifusha, ambapo haitakiwi kuzidi dakika kumi wakati wa kujifusha.

Anasema mimea hiyo ina sifa nyingi ikiwamo mafuta muhimu (mafuta tete),  yanayosaidia mwili kujiskia vizuri na kuimarisha kinga za mwili, ambapo harufu ya mimea hiyo ndio dawa yenyewe.

Anasema ni muhimu kuondoa mawazo hasa katika kipindi hiki cha kukabiliana na Covid-19 kwa sababu ndio chanzo kikubwa cha magonjwa na vifo vingi.

MJAMZITO

Kuhusu wajawazito kujisha anasema wanaweza kufanya hivyo kwa kutumia mimea hiyo ilimradi wazingatie tahadhali mbalimbali za muda na mengineyo.

Mgaya anasema hata hivyo, taasisi hiyo itaanza utafiti wa kujifusha huku akisisitiza kujifusha kwa kuacha mdomo wazi na pua ndio tiba sahihi ya kuua vimelea na kuimarisha kinga mwilini.

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )