Kigwangala amwaga pikipiki, baiskeli, vijana wampinga

Sehemu ya Pikipiki 38 aina ya “Boxer” na Baiskeli 780 ambazo Mbunge wa Jimbo la Nzega Vijijini, Dkt. Hamis Kigwangala aliwakabidhi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jimbo la Nzega Vijijini ikiwa ni ahadi aliyowaahidi mwaka 2017. (Picha na Suleiman Abeid)
Na Suleiman Abeid,
MBUNGE wa Jimbo la Nzega Vijijini mkoani Tabora, Dkt. Hamisi Kigwangala, amekabidhi msaada wa Pikipiki 38 na Baiskeli 780 kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jimbo la Nzega Vijijini ikiwa ni moja ya utekelezaji wa ahadi alizozitoa kwa wajumbe hao mwaka 2017.
Hata hivyo hafla hiyo iliingia dosari mwishoni baada ya kuibuka kundi la vijana wengine wa CCM (Green Guard) waliopinga kitendo kilichofanyika na mbunge huyo, wakidai ni mbinu za kutoa rushwa kwa wapiga kura za maoni ikizingatiwa muda mfupi umebakia kuelekea upigaji kura za maoni.
Dkt. Kigwangala amekabidhi pikipiki na baiskeli hizo juzi mjini Nzega wakati wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Wajumbe wa Jimbo la Uchaguzi la Nzega, vijijini ambapo pia aliwasilisha taarifa yake ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 – 2020 katika jimbo lake.

Mlezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Tabora na mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Afadhali Twali (wa tatu kutoka kulia) akimkabidhi Pikipiki mmoja wa wajumbe wa Mkuu wa Jimbo la Nzega Vijijini mkoani Tabora ambazo zimetolewa na mbunge wa Jimbo hilo, Dkt. Hamis Kigwangala wa kwanza kulia. (Picha na Suleiman Abeid)

Kutokana na tafrani iliyojitokeza ikisababishwa na vijana hao, Polisi walilazimika kuingilia kati na kukamata baadhi ya vijana. Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Afadhali Twalib aliyemwakilisha, Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashir Ally, wakiwemo pia wabunge wa viti maalum Mkoa wa Tabora, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Mwenyekiti wa CCM mkoani Tabora, Hassan Wakasuvi.
Dkt. Kigwangala amesema ameamua kutoa msaada huo ikiwa ni kutekeleza ahadi yake aliyoitoa kwa wajumbe hao mwaka 2017 na kwamba lengo lake wajumbe Watazitumia kuifanyia kampeni CCM wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
“Mheshimiwa mgeni rasmi, ninayo heshima kubwa kumalizia hotuba yangu hii kwa kukushukuru kukubali kuja kuwa mgeni rasmi kwenye hafla yetu, na nilitoa ahadi mwaka 2017 kwenye ukumbi huu mbele ya Katibu Mkuu wa Chama ya kuendelea kuwafadhili watendaji wa ngazi ya kata na matawi,”
amesema na kuongeza; up
“Ninafahamu viongozi wetu wa ngazi ya chini hawana posho wala mishahara , lakini wanajitolea kuimarisha chama chetu, hivyo mimi leo hii nitakabidhi hapa Pikipiki 38 kwa wenyeviti wote wa CCM wa kata, makatibu wenezi wote watapata Pikipiki, lakini pia nitakabidhi baiskeli 780 kwa wajumbe wangu wote wa mkutano mkuu wa Jimbo la Nzega Vijijini.”
Kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Jimbo lake la Nzega Vijijini, Dkt. Kigwangala amesema amejitahidi kutekeleza ahadi nyingi alizozitoa mwaka 2015 ikiwemo kuboresha miundombinu ya barabara, maji, elimu na huduma za afya.
“Mheshimiwa mgeni rasmi, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, tumefanikiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za maji, ujenzi wa miundombinu mipya ya maji katika kijiji cha Ngukumo, Mwambaha, Nkiniziwa na vinginevyo na tumepata maji kutoka Ziwa Victoria, changamoto ya maji kwenye jimbo letu itakuwa historia,” alifafanua.
Awali katika hotuba zao viongozi mbalimbali wa CCM mkoani Tabora akiwemo mlezi wa mkoa huo, Afadhali Twalib walimpongeza Dkt. Kigwangala kwa kazi kubwa aliyoifanya katika jimbo lake ikiwemo msaada alioutoa kwa wajumbe wake wapiga kura wa Jimbo la Nzega Vijijini.
Wabunge wa viti maalumu, Mwanne Nchemba na Munde Tambwe  mbali ya kumpongeza Dkt. Kigwangala pia waliwaomba wajumbe wote watakaopiga kura za maoni kuhakikisha hawampotezi mbunge huyo pamoja na wabunge wa majimbo ya Bukene, Seleman Zedi na Nzega mjini, Hussen Bashe.
Katibu wa CCM wa mkoa wa Tabora, Solomon Kasaba pamoja na kumpongeza mbunge huyo alikemea tabia ya kuwa na msururu wa wagombea wengi na kwamba kama kuna mtu ameweza kuwaletea watu maendeleo hakuna sababu za kumvuta miguu , kwani itakuwa ni wao wenyewe kutaka kujicheleweshea maendeleo.
“Akitokea hapa mtia nia mwingine yeyote kunilalamikia eti nimempongeza Dkt. Kigwangala nikiwa ni mkurugenzi wa uchaguzi, huyo hata shetani hatamuunga mkono kwa sababu yaliyofanywa yameonekana na niseme kitu kimoja kwamba, kusema haya si kwamba tunaminya demokrasia,” amesema na kuongeza;
“Mtu mwingine yeyote kabla ya kuchukua fomu, ajitathimini kwanza ajiulize sifa anazo? Maendeleo yaliyofikiwa je, mimi ninaweza kuyaendelea au tukarudi nyuma? Sasa ukiona ni ngoma nzito kutokuchukua fomu ni sehemu ya ustaarabu, kuwa na utitiri wa wagombea wakati mwingine siyo demokrasia wakati mwingine ni fujo.”
CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )