Hukumu Ya Zitto Kabwe, Hatma Yake kujulikana leo.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, leo  Ijumaa, tarehe 29 Mei, inatarajia kusoma hukumu ya kesi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe

Hukumu hiyo ya kesi namba 327/2018 ya uchochezi, inayotarajiwa kuvuta hisia za watu mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania, itatolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi. 

Kesi hiyo iliyofunguliwa tarehe 2 Novemba 2018 na Jamhuri, itahitimishwa leo kwa Zitto ambaye ni Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, ama kutupwa gerezani, kupigwa faini, kufungwa au kuachiwa huru
 

Katika kesi ya msingi, Zitto anadaiwa Oktoba 28, 2018 akiwa katika mkutano na waandishi wa habari, uliofanyika katika makao makuu ya ofisi ya Chama cha ACT –Wazalendo, alitoa maneno ya uchochezi yenye kuleta hisia ya hofu na chuki.

Ilidaiwa kuwa mshtakiwa alinukuliwa “…watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya Nguruka, polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua…”

Katika shitaka ya pili ilidaiwa Oktoba 28, 2019 eneo la Kijitonyama katika makao makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam, alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi akisema “…lakini tumefuatilia kwa kina jambo hili, taarifa ambazo tumezipata kutoka kijijini Mpeta-Nguruka, Uvinza ni mbaya, ni taarifa ambazo zinaonyesha wananchi wengi sana wameuawa na jeshi la Polisi pamoja na kwamba afande Sirro amekwenda kule, haijatoa taarifa yoyote kuhusu wananchi…kama hawa Wanyantuzu walivamia eneo la Ranchi kuna taratibu za kisheria za kuchukua na sio kuwauwa, wananchi wengi sana wamekufa…”

Ilidaiwa kuwa katika tarehe hiyo hiyo, Zitto alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi akisema “… Tumekuwa tukifuatilia kwa kina yanayojiri yote huko Uvinza tunasikitika kusema kuwa taarifa tunazozipata kutoka Uvinza zinaogofya mno, kwani tunaambiwa kuwa wananchi zaidi ya 100 wa kabila la Wanyantuzu wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi na polisi, wengine wakisema kuuawa hata wakiwa kwenye matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa kwenye purukushani na jeshi la polisi…’’

Katika shauri hilo, upande wa mashitaka uliwasilisha mashahidi 15, huku Zitto akiwasilisha mashahidi nane.

Upande wa mashtaka uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka akisaidiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nassoro Katuga; huku Zitto akitetewa na mawakili watatu wakiongozwa na Jebra Kambole.

Mawakili wengine waliomtetea Zitto, ni Frank Mwakibolwa na Bonifacia Mapunda.

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )