Hospitla ya Wilaya Chamwino yatakiwa kujiandaa kwa dharura ya Korona

Nteghenjwa Hosseah, Mlowo
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemani Jafo ameutaka uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kukamilisha mahitaji muhimu ya Hospitali ya Wilaya hiyo ambayo iko katika hatua za ukamilishaji wa ujenzi kwa tahadhari ya kupokea wagonjwa wa Korona endapo hali isipotengemaa.

Jafo ameyasema hayo mapema leo alipotembelea Hospitali hiyo inayojengwa katika eneo la Mlowo Wilayani Chamwino na kukuta ujenzi katika hatua za ukamilishaji kisha kutoa rai hiyo kwa viongozi kujiandaa mapema na Janga hili la Kidunia.

Amesema kutokana na Jiografia ya hospitali hii kuwa imejitenga kabisa na maeneo ya makazi ya watu ninashauri muandae jengo moja maalumu na mlikamilishe kwa kila kitu kinachohitajika ili endapo janga hili likiendelea jengo hilo litumika kwa ajili ya kutoa huduma kwa wagonjwa wa Korona.

“Kwa hali tuliyonayo sasa hatutakiwa kukaa kusubiria mpaka hali iwe mbaya zaidi tunatakiwa kuendelea kujikinga na kuchukua tahadhari za awali kabisa ikiwa ni pamoja na kuandaa maeneo ya kutolea huduma kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huu hatari na hospitail yetu hii naona inafaa kabisa kwa kuwa ina sifa zote” alisisitiza Jafo.

Wakati huo huo Waziri Jafo aliwapongeza viongozi wa Halmashauri ya Chamwino kwa kusimamia kwa makini ujenzi wa Hospital hiyo na kuhakikisha kuwa inakamilika kwa ubora wa hali ya juu na kwa wakati.

“Nimefurahi kukuta ujenzi umefikia katika hatua hii ya ukamilishaji, vitu vidogo sana ndio vimebakia kumalizia kabisa ujenzi na majengo yote yanaonekana kuwa na ubora wa hali ya juu hakika nimefurahishwa na hatua hii na hongereni sana” Alisema Jafo.

Haya kwangu mimi naona kama ni mafanikio kwani mwanzoni hali ilikua mbaya,  ujenzi ulikua unasuasua nilitumia nguvu kufuatilia na kusimamia lakini kwa sasa wote tunajivunia mafanikio haya huu ndio uongozi wa pamoja unaotakiwa katika utekelezaji wa miradi.

Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ni miongoni mwa HospitaIi za Halmashauri 71  zinazoendelea kujengwa Nchini Kote kupitia mpango wa Maboresho wa Huduma za Afya unaosimamiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI.

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )