GEKUL AMSIMAMISHA KAZI MKUU WA KITUO CHA UKAGUZI WA MIFUGO RUVU DARAJANI

   Msimamizi  wa Ujenzi wa Bwawa la Kunyweshea Mifugo
  la Chamakweza, Robert Baltazar akimuonesha michoro ya bwawa hilo, Naibu
  Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (wa kwanza kulia) alipotembelea
  kukagua maendeleo ya ujenzi wa bwawa hilo lililopo Chalinze, Wilayani
  Bagamoyo, Mkoani Pwani Februari 24, 2021. Wa pili kutoka kulia ni Mkuu wa
  Mkoa wa Pwani, Mhandisi, Evarist Ndikilo.

   Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul akijadiliana jambo na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo (kushoto) na Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (kulia) alipofanya ziara kukagua Kituo cha Ukaguzi wa Mifugo cha Ruvu Darajani kilichopo Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani jana.
   Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Mifugo, Rogers Shengoto akijibu moja ya hoja ziliyoibuliwa katika ziara ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul aliyoifanya Mkoani Pwani. 

    


   Na Mbaraka Kambona, Pwani

    

   Naibu Waziri wa Mifugo na
   Uvuvi, Pauline Gekul amemsimamisha kazi Mkuu wa Kituo cha Ukaguzi wa Mifugo cha
   Ruvu Darajani, Gabriel Lyakurwa kwa tuhuma za kutorosha mifugo na kusababisha
   upotevu wa mapato ya Serikali, huku akimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi,
   Evarist Ndikilo kuwachukulia hatua Watumishi waliochini ya Mkurugenzi wa
   Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ambao walikuwa wanashirikiana na Mkuu huyo wa
   kituo.  
    

   Gekul alitoa maamuzi hayo
   baada ya Mkuu huyo wa Mkoa wa Pwani kuibua tuhuma hizo katika ziara yake
   aliyoifanya kwenye kituo hicho kilichopo Ruvu Darajani, Wilayani Bagamoyo jana.
    

   Mhandisi Ndikilo alisema uchunguzi
   alioufanya umebaini kuwa Mkuu wa kituo hicho amekuwa akishirikiana na wenzake wasiowaaminifu
   kutorosha mifugo inayopelekwa katika kituo hicho kwa ajili ya kukaguliwa kabla ya
   kuruhusiwa kupelekwa katika maeneo mengine ya minada.
    

   “Mhe. Naibu Waziri nimefanya
   uchunguzi wa kina na kugundua kuwa utoroshaji huu unahusisha mtandao wa watu
   wengi wakiwemo baadhi ya Wananchi, Wafanyabiashara na Watumishi wa Serikali…, kwa
   mfano tarehe 17 mwezi huu wa pili kuna Magari matano yalileta ng’ombe katika
   kituo hiki kwa ajili ya kukaguliwa lakini ni gari moja tu lililokwenda Dar es
   Salaam kama kawaida ilivyo, huku mengine yaliyobaki yakichepushwa na mifugo
   ilipelekwa Kisarawe, Kibaha na Kijiji cha Kidogozero kinyemela,” alisema
   Mhandisi Ndikilo.
    

   Kufuatia tuhuma hizo, Naibu
   Waziri Gekul alitoa maagizo hayo ya kusimamishwa kazi mkuu huyo wa kituo huku akisema
   kuwa Wizara itaunda tume maalum kwa ajili ya kwenda kuchunguza tuhuma hizo
   ikiwemo kupitia mahesabu yote ili kubaini ni kwa kiasi gani mapato ya Serikali
   yamepotea na wale wote watakaoonekana kuhusika katika upotevu huo watachukuliwa
   hatua kali.
    

   “Hatuwezi kucheza na
   maduhuli ya Serikali, haiwezekani tuwe na ng’ombe zaidi ya milioni 33 lakini
   mchango wa sekta ya mifugo katika pato la taifa hauzidi asilimia 7, ni kwa
   sababu ya michezo kama hii, hatutakubali, na tutakwenda kukagua katika maeneo
   yote ya minada,” alisema Gekul.
    

   Naye, Mbunge wa Chalinze,
   Ridhiwani Kikwete alisema kuwa katika jambo ambalo wamekuwa wakilisemea sana ni
   kituo hicho kukithiri kwa vitendo vya ubadhilifu ambavyo vimekuwa vikichangia
   Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kupoteza mapato.
    

   Ridhiwani alimuomba Naibu
   Waziri huyo kuhakikisha anachukua hatua madhubuti za kudhibiti vitendo hivyo
   vya ubadhirifu ikiwemo kuondoa mtandao wote wa waharifu ili halmashauri iweze kupata
   mapato yanayostahili.

   CATEGORIES
   Share This

   COMMENTS

   Wordpress (0)
   Disqus (0 )