EWURA Yaipongeza Makambako kwa utoaji huduma

Na Esther Macha, Mbeya

MAMLAKA ya Maji safi na Usafi wa Mazingira katika Mji wa Makambako Mkoani Njombe imeibuka kinara katika utoaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira katika ripoti ya mwaka 2018/19 kwa upande wa mamlaka za maji za Wilaya na Miji midogo 83.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za Ewura kanda,Meneja wa kanda ya nyanda za juu kusini wa mamlaka ya udhibiti wa huduma za Nishati na maji (EWURA )Karim Ally alisema kuwa kwa upande wa mamlaka za miji ya Wilaya na Miji midogo zilizofanya vizuri iliyoshika nafasi ya kwanza ni mamlaka ya maji katika Mji wa Makambako .

Aidha Ally alisema nafasi ya pili ilichukuliwa na mamlaka ya maji Mikumi huku mamlaka ya maji Biharamulo ikishika nafasi ya tatu .

Akielezea zaidi Meneja huyo wa Kanda alisema Mamlaka ya majisafi na usafi wa Mazingira Makambako imekuwa ikifanya vizuri zaidi katika kufikia malengo ya kiutendaji katika utoaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira na kuwa miongoni mwa mamlaka za miji 83 za Wilaya na Miji midogo.

“Leo hii nawakabidhi rasmi mamlaka ya majisafi na usafi mna mazingira Makambako Tuzo mbili na vyeti vitatu kwa katika utoaji huduma bora za majisafi na usafi wa mazingira”alisema Meneja huyo.

Ally alisema kwamba tuzo hizo na vyeti kwa mamlaka bora katika utoaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira kwa mwaka wa fedha wa 2018/19 ni miongoni mwa mamlaka 83 za maji za Wilaya na Miji midogo .

Aidha alisema kuwa tuzo na cheti ya mamlaka bora kwa kufikia malengo ya kiutendaji katika utoaji wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa mamlaka 83 za wilaya,cheti cha kuwasilishwa kwa wakati Tozo ya EWURA kwa mwaka 2018/19

Kwa upande wake Mkurugenzi wa mamlaka ya maji Makambako , Mhandisi Lufyagile Oscar alisema tuzo na vyeti vilivyotolewa na EWURA wataendelea kuvitetea tena kwa mwaka 2020/ 2021 , wizara ya maji imekuwa ikuiwazesha kuwapa fedha katika kufikia malengo.

Akishukuru kwa Tuzo na Vyeti ,Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Makambako ,Paulo Malala alisema kuwa ofisi yake inashukuru sana EWURA kutambua mchango wao mkubwa katika kutoa huduma kwa wananchi.

Malala alisema Tuzo na vyeti vilivyotolewa na EWURA vitasaidia mamlaka ya Mji Makambako kujijenga zaidi kwa mwaka unaokuja na kujipanga zaidi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )