DKT. KYARUZI: TUNA UMEME WA KUTOSHA KULIKO MAHITAJI

 

Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Chini ya Mwenyekiti wake Dkt. Alexander Kyaruzi imeendelea na ziara yake ya kikazi ya kukagua vituo vya kuzalisha umeme, ambapo leo Jumatano Februari 10,2021 imevitembelea vituo vya kuzalisha umeme vya Ubungo l na Ubungo ll jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua vituo hivyo, Mwenyekiti wa Bodi hiyo Dkt. Alexander Kyaruzi amesema, katika kituo cha Ubungo l chenye mitambo 12 ya kuzalisha umeme ambapo kila mtambo unazalisha megawati 8.5, mitambo 10 kati yake inafanya kazi huku mitambo miwili ikiwa inafanyiwa matengenezo.

“Leo tumetembelea mitambo ya kuzalisha umeme ya Ubungo I na Ubungo ll na kimsingi tumefarijika sana na maendelea yake katika uzalishaji, Ubungo l ina mitambo 12 na kila mtambo unazalisha megawati 8.5, mitambo kumi inafanya kazi na miwili iko katika matengenezo na mwishoni mwa mwezi Machi mmoja utakuwa umekamilika” alisema Dkt. Kyaruzi

Kuhusu matengenezo ya mitambo hiyo miwili ya kuzalisha umeme katika kituo hicho katika Dkt. Kyaruzi amesema

“Kuna mitambo ambayo imefikia wakati wa kufanyiwa matengenezo kinga, na unapofika wakati wa matengenezo kinga na ni lazima matengenezo kinga yafanyike, usipofanya matengenezo kinga maana yake utafanya matengenezo haribifu ya mitambo kwa maana mtambo utaharibika”

Akielezea kwa kifupi hali halisi ya kituo cha kuzalisha umeme cha Ubungo ll, Mwenyekiti huyo amesema, Kituo hicho kina jumla ya mitambo mitatu na kila mtambo unazalisha megawati 43 ambapo kwa sasa mitambo miwili inaendelea na uzalishaji na mtambo huo mmoja unafanyiwa matengenezo kinga. 

Mbali na hayo, Dkt. Kyaruzi ameweka wazi hali ya umeme nchini kwa hivi sasa, ambapo amesema TANESCO inazalisha umeme wa kutosha kuliko mahitaji au matumizi ya nishati hiyo nchini na kuwataka wananchi waondoe hofu kuhusu hali ya umeme. 

Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Ufuaji umeme TANESCO, Mhandisi Steven Manda amesema, matengenezo kinga ya mitambo ya kuzalisha umeme inaendelea vizuri ambapo tayari matengenezo ya baadhi ya mitambo yamekamilika na mitambo imerejea katika uzalishaji huku akisisitiza kuwa, suala la matengenezo ni jambo la kawaida kwa mitambo au vifaa.

“Matengenezo ya mitambo yanaendelea vizuri, mitambo mingine inaendelea na matengenezo na mingine tayari imesharudi kwenye uzalishaji. Matangenezo ni jambo la kawaida kwa mtambo au kifaa chochote kile” alisema Mhandisi Manda

Aidha, Mhandisi Manda amebainisha kuwa, suala la umeme kukatika eneo fulani si kwamba TANESCO ina upungufu wa umeme unazolishwa, bali ni tatizo linalotokea katika eneo tu fulani ambalo husababishwa na vitu vingi ikiwemo nguzo kuanguka au kasoro kwenye nyaya na sababu nyingine.

“Suala la umeme kukatika ni muunganiko wa viti vingi, umeme tunao wa kutosha,mfano kwa leo Jumatano Februari 10, 2021 tuna ziada ya megawati 128, hivyo umeme unapokatika ni kutokana na changamoto ya eneo husika, na unapopata changamoto yoyote kuhusu huduma ya umeme ni vyema kuwasiliana na ofisi za TANESCO katika eneo lako” alisema Mhandisi Manda

Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO ipo katika ziara ya ya kutembelea vituo vya kuzalisha umeme nchini kujiridhirisha ufanisi wake na kukagua shughuli mbalimbali za uzalishaji katika vituo hivyo sanjari na kutekeleza maagizo waliyopewa na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani Februari 06, 2021 alipofanya kikao cha pamoja na bodi hiyo katika ofisi ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam.

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )