Dkt. Kawambwa akikabidhi kikundi pikipiki tatuNa Omary Mngindo, Bagamoyo.


Mbunge wa jimbo la Bagamoyo Mkoa wa Pwani Dkt. Shukuru Kawambwa, amekikabidhi kikundi cha Umoja wa Madereva wa Bodaboda Stendi Geti namba 4 (UMABOS G4) Kitongoji cha Benki Kata ya Dunda pikipiki tatu.

Dkt. Kawambwa amemkabidhi pikipiki hizo Katibu wa kikundi hicho Abdallah Jongo, zilizotokana na mkopo kutoka halmashauri ya Wilaya, ambapo walipokea kiasi cha shilingi milioni 4, zilizowezesha kupatikana kwa bodaboda hizo.


Akizungumza na wana-Kikundi hao, Dkt. Kawambwa alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli, inawajali wananchi wa hali ya chini ndio maana halmashauri zote zina mfuko kwa ajili ya kukopesha na wajasiriamali kisha kurejesha pasiporiba.

“Hatua hii ni faraja kwangu, kwani nami ni miongoni mwa washauri toka kuanzishwa kwake mpaka hapa kilipofikia, hii inathibitishwa na mshikamano mliokuwa nao, nimeamini kuna vijana wanaopenda kujituma wenyewe kwa shughuli halali,” alisema Dkt. Kawambwa.

Aidha Dkt. Kawambwa ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wana-Bagamoyo kuchangamkia fedha hizo, na kwamba serikali haiwezi kumfuata mtu mmoja mmoja kumpatia fedha, huku akiwahamasisha jiunga vikundi ikiwa ni njia rahisi ya kuwafikia wenye uhitaji kwa wakati mmoja.


Aliongeza kuwa, kikundi hicho kitavyoongeza pikipiki kitawaongezea fursa vijana wenzao wataoziendesha, ambao kwa namna moja au nyingine watakuwa wanapata ridhiki itayowasaidia wao pamoja na familia zao, kwa kujipatia kipato.

Diwani wa Kata ya Dunda Dickson Makamba aliwapongeza vijana hao, huku akimshauri Dkt. Kawambwa kama ikiwezekana watafutiwe Bajaj ili waweze kuendelea na kazi zao, hata kipindi cha mvua, huku akikipongeza kwa kusema ni kikundi cha mfano wa kuigwa katani humo.

“Hiki kikundi hakina muda mrefu toka kianzishwe, lakini kimekuwa na mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake ukilinganisha na vikundi vingine ambavyo vina muda mrefu,” alisema Makamba.

Taarifa ya kikundi iliyosomwa na Katibu Jongo imeelezea malengo yao ni kupata pikipiki tano, na kwamba kwa sasa wamepata tatu, hivyo watashukuru wakipatikana wadau watakaowaunga  mkono katika kufikia malengo yao.

“Mheshimiwa Mbunge wetu, kwa niaba ya kikundi tunakushuku binafsi pamoja na uongozi wote wa Halmashauri ya Bagamoyo, kwa kutupatia pikipiki hizi tatu kupitia mkopo wa shilingi milioni nane zilizotuwezesha kupata pikipiki hizi,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus (0 )