DC MBONEKO AZINDUA RASMI MRADI WA MAJI UZOGORE SHINYANGA.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko amezindua Rasmi Mradi
wa Maji ya Bomba kijiji cha Uzogore kata ya Ibadakuli katika Manispaa ya
Shinyanga uliojengwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA)
wilaya ya Shinyanga, Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Shinyanga
(SHUWASA) na wananchi ukigharimu jumla ya shilingi milioni 88.8.
Akizungumza wakati wa kuzindua Mradi huo leo Alhamis Juni 18,2020,
Mboneko amewataka wananchi wa Uzogore kutunza miundo mbinu ya maji ili iweze
kudumu kwa kipindi kirefu na kuwasisitiza viongozi wa eneo hilo wasimamie
wananchi wapate huduma ya maji muda wote.
“Wananchi wa kijiji hiki wakiongozwa na Mwenyekiti wa kijiji walikuja
ofisini kwangu wakileta kilio cha Wana Uzogore,nami nikaamua kuja mwenyewe
Uzogore kuwasikiliza Septemba 16,2019 kutokana na kwamba serikali ni sikivu na
inatekeleza yale wananchi wanayataka.
Niwapongeze SHUWASA na RUWASA ambao nao baada ya kuwaambia kuwa wananchi
wanahitaji maji wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mnapata maji na leo
mnaanza kupata huduma ya maji safi na salama”,alisema Mboneko
“Kufanikiwa kwa mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi
ya CCM mwaka 2015 ya kumtua ndoo mwanamke kichwani na kumpunguzia umbali mrefu
kutafuta maji”,alisema Mboneko.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa wilaya alisema baada ya maji kufika
Uzogore sasa awamu inayofuata na kufikisha maji katika kijiji cha Bugwandege.
Kaimu Meneja wa RUWASA wilaya ya Shinyanga, Emael Nkopi alisema ujenzi
wa mradi wa Maji Uzogore ulioanza Februari 5,2020 na kukamilika Juni 5,2020 ni
sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa wanakijiji wa Uzogore
uliofanyika Septemba 16,2019 ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa wilaya ya
Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko.
Alisema Katika mkutano huo uliojadili namna ya kuwapatia wananchi huduma
ya maji safi na salama,wananchi walikubaliana kutoa maeneo yao bila gharama
yoyote katika njia za bomba na sehemu ya kujenga vituo (DP) ya magati ya
kuchotea maji pamoja na kujitolea nguvu kazi katika uchimbaji wa mitaro ya
kupitisha bomba.
“Gharama halisi zilizotumika katika ujenzi wa mradi wa Maji katika
Kijiji cha Uzogore utakaonufaisha wakazi 3,778 ni shilingi 88,830,000/= ambapo
kati ya hizo, RUWASA wilaya ya Shinyanga imetoa shilingi 50,400,000/=, SHUWASA
shilingi 31,690,000/= na nguvu kazi ya wananchi (kuchimba mitaro na kufukia) shilingi
6,740,000/=”,alieleza
“Katika utekelezaji wa mradi wa kusambaza maji ya bomba katika kijiji
cha Uzogore jumla ya mita 6720 za mtandao wa mabomba zimelazwa,Stand Pipe mbili
katika taasisi za umma (shule ya msingi Uzogore 1 na shule ya sekondari Uzogore
1) na vituo vya kuchotea maji/maghati matano yamejengwa katika vitongoji vya
Uzogore Centre,Majengo A,Majengo B,Shimarulwe na Ikulilo”,alieleza Nkopi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa SHUWASA, Bi. Flaviana Kifizi alisema
SHUWASA kwa kushirikiana na RUWASA walitoa hadi ya kupeleka maji Uzogore na
wametekeleza ili kumtua mwanamke ndoo kichwani.
“Kazi ya RUWASA ni kujenga miundo mbinu ya maji kuelekea maeneo ambayo
hajafikiwa na huduma ya maji,RUWASA wamemaliza kazi yao,tumejenga sehemu za
kuchotea maji (vioski),tumeleta maji hapa kutoka Ziwa Victoria ili kumtua ndoo
mwanamke kichwani. Tunaomba wananchi muunge maji majumbani mwenu kwa gharama
zenu na tutawaungia maji ndani ya muda mfupi”,alisema Kifizi.
Nao wakazi wa Uzogore wameeleza kufurahia kuanza kupata huduma ya maji
safi na salama na kuondokana na adha ya muda mrefu ya kusafiri umbali mrefu
kufuata maji.

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )