DC JOKATE AWATOLEA UVIVU WANAOTAPELI KWA KUTUMIA JINA LAKE

 


 Atoa maagizo kwa Jeshi la polisi 

Na Said Mwishehe

MKUU wa Wilaya ya Kisarawe Mkoani Pwani Jokate Mwegelo amesema anasikitishwa na tabia ya baadhi ya watu wanaotumia jina lake kuwatapeli wananchi fedha zao huku akivitaka vyombo vya ulinzi na usalama na hasa Jeshi la Polisi nchini kupitia kitengo chake cha kukabili uhalifu mtandaoni kuchukua hatua dhidi ya watu hao.

Amesema ni kwa muda mrefu sasa amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wananchi mbalimbali ambao wamekuwa wakichukuliwa fedha zao kwa njia hiyo ya utapeli kwenye mitandao ambapo kuna watu wamekuwa wakifungua akaunti zisizo rasmi(akaunti feki) kwa kuwaaminisha wananchi kuwa ni yeye na kuchukua fedha.

Akizungumza leo Februari 15,2021, Jokate ameweka wazi kwamba amekuwa akitoa taarifa mara kwa mara kwa Jeshi la Polisi kuhusu utapeli huo, hivyo anaviomba kufanya uchunguzi haraka ili kuwezesha kubaini wanaojihusisha na vitendo hivyo kwani anaamini jeshi hilo linao uwezo mkubwa kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni.

“Nimewaita ndugu zangu waandishi wa habari kuzungumza nanyi leo, ili mfikishe ujumbe huu kwa Watanzania,kuna watu wanatumia vibaya majina ya viongozi na watu mashuhuri ili kurubuni na kutapeli watu mbalimbali, binafsi kuna kikundi cha watu ambacho kimekuwa kikitumia jina langu na picha zangu wanafungua akaunti feki.

“wanaongea na umma wa Watanzania wakijifanya kama mimi, huko nyuma nimewahi kuzungumzia hili, kuna watu wanafungua akaunti mtandaoni, wanawapa watu namba za simu na wanawaambia kuna mikopo inapatikana wilaya ya Kisarawe ambayo inatolewa na Mkuu wa wilaya Jokate Mwegelo, na wakishawapa namba ya simu wanaingia Whatsap wakiwarubuni kwa kutumia ujanja ujanja.

“Na watu hao wakishapigiwa wanaamini wanaongea na mimi, binafsi naomba niwaambie umma wa Watanzania , mimi sina huduma yoyote ya kutoa mikopo, nimeliweka wazi kwenye kurasa zangu rasmi ambazo ninazitumia kwenye mitandao ya kijamii lakini bado linaendelea, narudia tena kuwaambia, sifanyi kazi ya kutoa mkopo wala huduma yoyote ya mkopo, sijawahi kufanya, sijafanya na wala sitafanya kwa siku za hivi karibuni hiyo huduma ya kutoa mikopo,”amesema Jokate.

Aidha amewaomba Watanzania kwamba mtu akitumiwa nyaraka ajiridhishe kwani ametoa mfano kuna nyaraka anayo inayoonesha Focus Vicoba inayoonesha wamesajiliwa kisheria lakini wameghushi, na wakati huo huo nyaraka hiyo inaonesha zinatambulika na Bunge jambo ambalo si kweli.

“Ukiangalia kwa haraka haraka hizi nyaraka ni za kughushi, naomba nitoa rai tena kwa wananchi kuwa makini, watu siku hizi ni wajanja sana, siku za karibuni nimepata kesi moja kuna mtu ametapeliwa fedha na anaamini kabisa ameongea na mimi, jamani mimi sina huduma ya mikopo, sijawahi kuwa na hiyo huduma.

“Nimeamua kusema ili kutoa tahadhari dhidi ya hao watu ambao mnaongea nao mtandaoni, watu wameamua kutumia mitandao kufanya utapeli, na hili jambo si kwangu tu bali kuna viongozi wengi majina yao yanatumiwa na matapeli. Kibaya zaidi watu wakishatapeliwa wanaamini ni viongozi, mimi kuna mtu anang’ang’ania kabisa kwamba amezungumza na mimi na amenipa hela yake.

“Narudia tena kutoa ombi kwa jeshi la Polisi na vyombo vya ulinzi na usalama kusaidia kuharakisha uchunguzi wao, hawa watu wanaofanya utapeli wanatumia namba za simu, hivyo ni rahisi kueleweka walipo, wachukuliwe hatua kwa mujibu wa kisheria, kwani kuna kitengo maaluma ambacho kinahusika na kukabiliana na uhalifu katika mitandao,”amesema Jokate.

“Niombe pia watu ambao wamefanyiwa utapeli huo kwenda kwenye vyombo vya ulinzi na usalama kutoa taarifa, kuna wananchi wengi wanatapeliwa kwa njia hiyo, kitengo kinachohusika na uhalifu wa mtandaoni wasikae kimya, wananchi wanaumia na viongozi tunaumia kwani majina yetu yanachafuka sana, mwananchi anaamini kabisa ametoa hela kwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe.

“Leo hii tunaoekana viongozi tunaibia wananchi jambo ambalo si kweli na linachafua viongozi wa Serikali, niombe tena kwa jeshi la polisi kuchukua hatua na ikiwekana wale ambao wametapeliwa fedha zao zirudishwe,”ameongeza Jokate na kusisitiza “Yanaoendelea mtandaoni hausiki nayo, ni mabaya na hayavumiliki, hivyo wenzetu wanaohusika na kupambana na uhalifu mtandaoni watusaidie, inatuumiza sana viongozi bila sababu yoyote.”

Aidha amesema kuna wananchi wamekuwa wakifika kwenye ofisi yake kwenda kuuliza mikopo inayotolewa na Mkuu wa Wilaya lakini wamekuwa wakiwaelimisha na hakuna kutu cha aina hiyo.”Matapeli wanakwenda mbali zaidi wanapiga video call na wanaonesha picha yangu hivi kwa sekunde kadhaa na watu wanaamini.Tuendelee kuelimishana kuwa huo unaofanyika ni utapeli mtupu.”

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )