DC IKUNGI AIAGIZA HALMASHAURI KUWAACHIA WANANCHI MASHAMBA YA KUPANDA KOROSHO

Mkuu wa Wilaya ya Ikungi,  Edward Mpogolo (kushoto) akizungumza na wananchi wa Vijiji vya Ulyampiti na Mwau katika eneo lenye mgogoro.

Wananchi wa Vijiji vya Ulyampiti na Mwau wakiwa katika eneo lenye mgogoro.

Na Dotto Mwaibale, Singida


MKUU wa Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida, Edward Mpogolo ameagiza Halmashauri  kuwaachia mashamba yao wananchi zaidi ya 36 ambayo walimpa mkulima mmoja mgeni bila ya kufuata utaratibu ili apande korosho.

Katika hatua nyingine Mpogolo ameiagiza halmashauri ya kijiji  na Idara ya Kilimo ya Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kumpatia eneo lingine mkulima huyo ili aweze kuliandaa na kuanzisha kilimo hicho badala ya kuyachukua mashamba ya wananchi hao waliyo yaendeleza na kupanda mazao ya chakula.

Mpogolo amechukua hatua hiyo baada ya kutokea mgogoro wa kugombea mashamba baada ya mkulima mgeni kupewa mashamba ya wananchi waliyoyafyeka na kuyatumia kwa kilimo.

Mpogolo alisema kama halmashauri imetenga eneo hilo kwa kilimo cha korosho ni vyema na wananchi hao wakawezeshwa na wao kunufaika na zao hilo la korosho badala ya kuwafukuza.

Vijiji vilivyokuwa na mgogoro huo ni Ulyampiti na Mwau huku kila upande ukiomba kuangaliwa upya wa mipaka ya maeneo yao ya ardhi.

Mpogolo ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo alitoa agizo hilo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo lililotengwa na Halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo cha zao la korosho.

Aidha mkuu huyo wa wilaya  alisisitiza  kwamba kutokana na mgogoro wa mipaka uliopo katika eneo hilo ni marufuku kwa viongozi wa serikali za vijiji hivyo kuendelea kukata na kugawa maeneo kwa wananchi au wawekezaji wenye ni ya kulima zao hilo la kibiashara bila kufuata taratibu.

“Sasa ndugu zangu pambaneni mlime, wewe ambaye hujapalilia nenda ukapalilie usije ukauwa watoto lakini kwenda kujikatia maeneo  mengine wenyewe ni marufuku kwa sababu kuna mgogoro kwenye maeneo  ya mipaka.” alisema Mpogolo. 

Mpogolo alitaja mkulima huyo mgeni aliyepewa ekari 300 kwenye maeneo ya wananchi kutoziendeleza kutokana na  mgogoro uliyopo.

Hata hivyo Mpogolo alitumia fursa hiyo pia kuuagiza uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi kwa kushirikiana na kamati za watu Tisa za ugawaji ardhi na usuluhishi migogoro kutoka katika vijiji vya Mwau na Ulyampiti na kuunda kamati ya kushughulikia mgogoro wa mpaka wa vijiji hivyo. Alisema wakati zoezi hilo likiendelea wananchi kwa upande wao wataendelea na shughuli za kilimo kwenye maeneo yao waliyokuwa wakiyatumia awali.

“Sasa katika kipindi hiki natoa maagizo kwanza kwa mtaalamu  ardhi wa Wilaya kwa kwa kushirikiana na Halmashauri za vijiji vyote viwili mtatengeneza kamati jumuishi na wajumbe tisa kutoka katika kila kijiji kushughulikia mipaka.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye eneo lenye mgogoro wa mipaka baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mwau, walisema kwamba mgogoro huo wa mpaka umetokana na uongozi wa Kijiji cha Ulyampiti kugawa eneo kwa wageni bila kuushirikisha uongozi wa Kijiji cha Mwau.

“Kwa sababu migongano ya mipaka siyo la hapa tu bali wengi  tunagongana kwa sababu ya kutoshirikishana, sasa mimi nakuomba mheshimiwa DC kwa kuwa leo umekanyaga ardhi hii tupe uamuzi kama si watu wa Ulyampiti utuambie kama ni wa Mwau we angalia mwenyewe Ulyampiti mpaka uko wapi na Mwau vile vile? alihoji kwa Shabani  Kijanga.

CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )