DC Babati Apokea Vifaa Vya Kujikinga Na Corona Kutoka kwa wafanyakazi wa shirika la Pharm Access Manyara.


Na John Walter-Babati,Manyara
Katika kuunga mkono jitihada za serikali za kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa Corona,wafanyakazi wa shirika la Pharm Access mkoa wa Manyara,  wametoa misaada ya vifaa kwa Mkuu wa Wilaya ya Babati, Elizabeth Kitundu.

Vifaa vilivyotolewa na shirika hilo  ni Miamvuli 50 na  Barakoa zipatazo 2,750,  huku elfu moja (1,000)  zikiwa zimetolewa na wafanyakazi wa shirika hilo kwa kujichanga kile walichojaliwa ili kuisaidia jamii katika kujikinga na Ugonjwa wa Covid 19.
Akizungumza baada ya kupokea vifaa hivyo, Mkuu wa wilaya amewashukuru Pharm Access kwa kujitoa kwao katika mapambano hayo huku akiahidi kuvigawa vifaa hivyo kwenye maeneo yanayopokea watu wengi ikiwemo hospitali ya mji wa Babati na ile ya  wilaya.

“Huu ni moyo wa ajabu sana ndugu zangu, niwapongeze kwa namna mlivyoguswa na mkaona ni vema kutoa mchango wenu kwenye mapambano haya ya ugonjwa huu wa Corona.
Niwasihi wadau wengine, kuguswa kama Pharm Access walivyoguswa na kushirikiana kwa pamoja katika kudhibiti maambukizi haya, siyo lazima kwa kutoa vifaa lakini hata kutoa elimu kwa wananchi wetu ya namna ya kujikinga na maambukizi ni msaada mkubwa pia,” Amesema Kitundu.
Kwa upande mwingine mkuu wa wilaya amepokea barakoa 150 kutoka taasisi ya kifedha inayoutwa “Hatua” kwa ajili ya kuwasaidia wajasiriamali wadogo katika soko kuu la Babati.

Kwa upande wake Mratibu wa shirika la Pharm Access kanda ya Kaskazini  Dr. Johnson Mali,  ameipongeza serikali kwa namna ambavyo imekua ikipambana na corona tangu ugonjwa huo uingie nchini na kuahidi kuendelea kushirikiana na serikali katika mapambano ya ugonjwa huo kwa kuchangia vifaa na pia kutoa elimu kwa wananchi ya kujikinga na maambukizi.

Hili ni jukumu letu sote kama Taifa, Hatupaswi kuiachia serikali ipambane yenyewe, uzalendo ni pamoja na kuungana kama Nchi kwenye mambo kama haya, tuwaombe wadau wengine wajitokeze kuiunga mkono serikali na ninaamini kwa pamoja tunaweza kuzuia na kudhibiti maambukizi ya Corona, ” Amesema Dr. Mali.
CATEGORIES
Share This

COMMENTS

Wordpress (0)
Disqus ( )